Habari za Punde

Speech ya Mkurugenzi wa Save the Children kwenye uzinduzi wa kampeni ya Mpira mmoja

HOTUBA YA MKURUGENZI WA SAVE THE CHILDREN NCHINI TANZANIA, RACHEL POUNDS KWENYE UZINDUZI WA KAMPENI YA “MPIRA MMOJA”YENYE LENGO LA KUPAMBANA NA UKATILI DHIDI YA WATOTO KUPITIA MCHEZO WA MIPIRA, TAREHE 10 JANUARI 2013
 
Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein; Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais,
ndugu Seif Sharif Hamad;
Waheshimiwa Mawaziri,
Waheshimiwa Naibu Mawaziri,
Waheshimiwa Wawakilishi wa balozi na wadau wa maendeleo;
Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa,
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya,
Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi,
Makatibu wakuu,
Wafanyakazi wa Save the Children na UNICEF,
Watoto,  mabibi na mabwana, itifaki imezingatiwa
 
Asalaam alekum
 
Kwanza kabisa, napenda kutumia fursa hii kuwapongezeni kwa kuadhimisha mwaka wa 49 wa mapinduzi ya Zanzibar. Nina furaha kubwa kushiriki katika uzinduzi wa kampeni ya kupambana na ukatili dhidi ya watoto na ugawaji wa mipira 20,000 kwa watoto na vijana wa Zanzibar ambayo itachangia katika kuzuia ukatili dhidi ya watoto.
 
Tanzania ni nchi ya kwanza barani Afrika kufanya utafiti wa kitaifa juu ya Ukatili dhiti ya Watoto-Kwa mara ya kwanza ikipima aina zote za ukatili (kingono, kimwili na kihisia) miongoni mwa wasichana na wavulana na kutoa makadirio kiwango cha ukatili kitaifa.
 
Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa ukatili dhidi ya watoto ni tatizo kubwa nchini Tanzania: yapata wasichana watatu kati ya 10 na yapata mvulana mmoja kati ya saba nchini Tanzania wamewahi kufanyiwa ukatili kabla ya kutimiza miaka 18.


Vilevile, karibu theluthi tatu ya wasichana na wavulana wamewahi kutendewa ukatili wa kimwili na watu wazima kabla ya kutimiza miaka 18 na theluthi moja wamewahi kutendewa ukatili wa kihisia na watu wazima wakati wa utoto wao.
 
Ingawa viwango vya ukatili kwa watoto Zanzibar ni vya chini (yapata asilimia 6 hadi 9 ya wavulana), ukatili wa kingono kwa watoto bado ni suala linalohitaji kutiliwa maanani haraka. Matokeo ya utafiti yana mantiki muhimu kwa kuandaa na kutekeleza mpango mahsusi wa kuzuia na kuitikia katika kushughulikia unyanyasaji na ukatili dhidi ya watoto.
 
Kuwa na takwimu fasaha na sahihi kwa ajili ya kutunga sera madhubuti, kwa kuzingatia athari na mahitaji, inaweza kusaidia sana katika kuimarisha mikakati ya kukinga na kuzuia ukatili kwa watoto, ikiwemo huduma bora na pana kutolewa kwa watoto walioathirika, pamoja na familia zao.
 
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeonesha utashi kushughulikia ukatili dhidi ya watoto na imefanya juhudi zaidi kutambua na kufuatilia sababu zinazochangia tatizo katika maeneo ambako matukio mengi yalitokea.
 
Mpango wa Taifa wa Zanzibar katika kuitikia kwenye Ukatili Dhidi ya Watoto wa mwaka 2011 hadi 2015 unatamka wazi dhamira yake kuwa ni kuandaa jamii isiyokuwa na ukatili kwa watoto. Chini ya uongozi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto, Kikosi kazi kinachojumuisha sekta mbalimbali kiliundwa ili kuratibu utafiti wa ukatili dhidi ya watoto.
 
Kikosi kazi hiki kinajumuisha wajumbe kutoka sekta ya umma, sekta binafsi, wizara na taasisi za serikali na asasi za kiraia.
 
Majukumu ya kikosi kazi yamekuwa si tu kuwa chombo cha kuratibu katika kupanga na kutoa mwongozo katika kutekeleza utafiti wa kitaifa, bali pia kusaidia kuweka msukumo kuweka matokeo ya utafiti katika vitendo.
 
Ulinzi wa mtoto dhidi ya ukatili na unyanyasaji unahitaji ushiriki wa sekta mbalimbali. Hakuna sekta moja wala mtaalam mmoja mwenye ujuzi, maarifa na rasilimali muhimu katika kutimiza mahitaji yote ya ulinzi wa mtoto.
 
Ni jambo muhimu kuwa na mwitikio ulio ratibiwa, ukihusisha sekta na taaluma zote katika kufanya kazi na watoto na familia zinazohitaji uangalizi na ulinzi. Mpango wa Mwitikio wa Taifa unaelekeza hatua za kuchukua katika sekta mbalimbali ikiwemo, mahakama, polisi, afya, elimu, ustawi wa jamii, asasi za kiraia, jamii na vyombo vya habari.
 
Sasa kuna maendeleo na uwekezaji wa kuridhisha katika kuboresha hali ya watoto wa Zanzibar na ni kutokana na malengo na afua hizi, ulinzi wa watoto katika MKUZA 2010 na 2013 utaelekeza juhudi zake.
 
Hayo ni pamoja na kuanzisha kitengo cha ulinzi wa mtoto katika idara ya Ustawi wa Jamii, kuandaa sera na miongozo ya taifa ya ulinzi wa mototo, kuanzisha Vituo vya Huduma kwa watoto (One Stop Centers) katika hospitali mbalimbali, madawati ya jinsia na watoto katika vituo vya polisi, Kozi ya Stashahada ya Ulinzi wa Mtoto katika Chuo Kikuu cha Zanzibar na kuandaa na kutekeleza sheria zenye mwelekeo wa kuboresha na kulinda haki na utashi wa watoto wa Zanzibar.
 
Na ndio maana leo hii tuna wadau wenzetu One World Futbal, Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar, UNICEF na Wizara ya Michezo na Habari, kushuhudia azimio la Zanzibar bora kwa watoto na kugawa mipira 20,000 ambayo itatumika katika kuchangia kupunguza ukatili dhidi ya watoto.
 
Mradi huu utanufaisha watoto 330,000 walioko mashuleni Pemba na Unguja na zaidi ya watoto na vijana 8800 katika vituo vya marekebisho, vituo vya kulelea yatima, mabaraza ya watoto na vikundi vya kijamii. Mheshimiwa; Kabla ya kuhitimisha, ningependa kuhuisha ahadi ya Save the Children kwa watoto wa Zanzibar na katika kufanya kazi kwa ushirikiano na serikali na wadau wengine katika kuendelea kutoa ulinzi kwa watoto wa Zanzibar.
 
  Napenda kukushukuru wewe Mheshimiwa Rais, kwa ushirikiano ambao Save the Children imekuwa ikiupata kutoka kwa Serikali ya Zanzibar na pia kuwashukuru watoto na wadau wetu kwa ushirikiano na kujitoa kwao.
 
Asante Sana

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.