Ujumbe wa UNICEF katika uzinduzi wa kampeni ya mawasiliano kwa ajili ya kupinga unyanyasaji dhidi ya watoto Zanzibar, Januari 10, 2013
Mheshimiwa Mgeni Rasmi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohammed Shein.
Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa ZanzibarMaalim Seif Sharif Hamad.
Waheshimiwa Mawaziri, Manaibu Mawaziri na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ndugu Abdalla Mwinyi.
Ndugu Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na Wawakilishi wa Idara za Serikali na Asasi za Kiraia.
Wazazi na Watoto, Mabibi na Mabwana.
Assalaam Alaikum
Mheshimiwa Mgeni Rasmi:
Ni heshima kubwa kuwa hapa leo nawewe pamoja na viongozi wa Serikali, Watoto, Wazazi, Asasi za Kiraia, na wanahabari, kushuhudia uzinduzi wa Kampeni ya Mawasiliano kwa ajili ya kupinga Unyanyasaji dhidi ya Watoto hapa Zanzibar.
Kwa kutoa kipaumbele kwa uzinduzi wa kampeni hiikunadhihirisha dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yakujenga mfumo wa kuwalinda watoto dhidi ya ukatili na unyanyasaji.
Tangu Ripoti ya Unyanyasaji dhidi ya watoto ilipozinduliwa mwaka mmoja uliopita, kumekuwa na maendeleo makubwa katika kukabiliana na vitendo hivyo.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepitisha Sheria ya Mtoto kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa watoto. Kwa hili ninaheshima kukupongeza sana Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali yako tukufu na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Pia ninaipongezasana Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watotokwa juhudi ilizochukua kuboresha huduma za kukabiliana na unyanyasaji wa watoto ikiwa ni pamoja na:
· Kuanzisha Vitengo vya Hifadhi ya Mtoto katika Idara ya Ustawi wa Jamii Unguja na Pemba,
· KuanzishaMadawati ya Jinsia na Watoto na vituo vya Mkono kwa Mkono (One Stop Centres),
na
· Kutayarisha kanuni za utekelezaji wa Sheria ya Mtoto
Mheshimiwa Mgeni Rasmi:
Hatua zaidi zinahitaji kuchukuliwa ili kukabiliana na matukio ya unyanyasaji wa watoto ambayo yanaongezeka kila siku.
Kipaumbele maalumu kinahitajika ili kuwalinda watoto wenye ulemavu na watoto wa kiume ambao matokeo ya utafiti yalionesha kuwa nao ni waathirika wakuu wa udhalilishaji wa kingono, ingawa mara nyingi jamii hukaa kimya na kesi zao haziripotiwi katika vyombo husika.
Kuzishirikisha jamii kujadili matatizo ya unyanyasaji dhidi ya watoto katika Shehia zao ni muhimu katika kujenga mazingira salama zaidi kwa watoto.
Jamii zinapaswa kuzitathmini upya desturi na imani zao ili kuona uhusiano wa desturi na imani hizo na ulinzi na uhifadhi wa mtoto ili kuweka maazimio ya pamoja juu ya ujenzi wa mfumo wa kuwalinda watoto wao dhidi ya unyanyasaji na udhalilishaji
Jamii zinapaswa pia kushirikiana na taasisi zinazotoa huduma katika kutoa ushahidi dhidi ya wale wote wanaohusika na unyanyasaji na udhalilishaji wa watoto ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Pia tunahitaji kuwahimiza wanajamii kuzungumza, na kuacha kuoneana aibu kuhusu suala la ukatili wa kijinsia. Tuache “kuoneana muhali”.
Ripoti ya Ukatili dhidi ya watoto inaonesha kuwa wahusika wa unyanyasaji ni watu ambao watoto hao wanawafahamu na kuwaamini.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi:
UNICEF iko tayari kushirikiana na Serikali ya Zanzibar ilikujenga mfumo imara wa ulinzi wa mtoto ambao utakua ni mfumo endelevu kama ulivyo mfumo wa elimu na afya
.
Jitihada zimeshaanza katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, na ni matumaini yanguzitaendelea katika Mikoa myengine.
Katika Mfumo wa uhifadhi wa mtoto, tunahitaji kujenga utaratibu madhubuti wa rufaa kwa waathirika wa vitendo vya unyanyasaji na mfumo wa mahkama za watoto.
Ili kuyafanya yote haya jamii zinahitaji taaluma na mawasiliano endelevu juu ya ulinzi wa mtoto ambao utajumuishwa katika mifumo iliyopo kama vile vikundi vya michezo, maskulini, mahospitalini na kupitia vyombo vya habari.
Nina imani kwamba mfumo huu utakuwa nguzo muhimu ya kukomesha ukatili dhidi ya watoto hapa Zanzibar.
Mwisho na mimi ningependa kusema ‘‘TUWACHE KUONEANA MUHALI, UNYANYASAJI WA WATOTO SASA BASI!”
Asanteni kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment