Habari za Punde

Dk Shein aomboleza mauaji ya Padri Mushi

Na Rajab Mkasaba, Ikulu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, amepokea kwa mshtuko mauaji ya Padri Evaristitus Mushin na kutoa pole kwa waumini, ndugu jamaa, marafiki na wananchi wote wa Zanzibar kufuatia kifo hicho.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mhe. Mohamed Aboud ameeleza hayo na kusisitiza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi itawasaka hadi kuwatia mikononi na hatimaye kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale wote waliohusika na mauaji hayo.

Waziri Aboud aliyaeleza hayo leo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Vuga, kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kufuatia mauaji ya Padri Evaristitus Mushi wa Kanisa Katoliki Zanzibar Parokia ya Mtakatifu ST.Joseph,Shangani.


Hapo jana Dkt. Shein alikutana na Askofu Shao huko katika Ikulu ndogo Migombani na kueleza masikitiko yake kutokana na kifo hicho cha hafla cha Padri Evaristitus wa Kanisa Katoliki la Zanzibar, na kuelezea haja ya kuwepo kwa uvumilivu katika kipindi hichi cha msiba.

Katika mazungumzo na Waandishi wa Habari, Waziri Aboud alisema kuwa Serikali imejipanga vizuri kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha kuwa watu wote waliohusika na mauaji hayo wanakamatwa mara moja .

“Kutona na jiografia ya Zanzibar,Tunaelewa kwamba zipo sehemu katika kisiwa cha Zanzibar ambazo wahalifu wanaweza kuzitumia, hivyo Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo husika vitaziba mianya yote ili kupambana na uhalifu “, alisema Aboud.

Alisema matendo ya uhalifu yanafanywa katika mazingira ya usiri mkubwa kwa hivyo ili wahalifu hao wakamatwe wananchi hawana budi kutoa mashirikiano kwa Jeshi la Polisi pale wanapohitajika.

Akijibu suali la Mwandishi, Mhe.Aboud alikanusha taarifa zilizozagaa mitaani za kuwepo silaha nyingi mikononi mwa watu wasiohusika na kuwataka wananchi kuondoa hofu. 

Sambamba na hayo, Mhe. Aboud amewataka viongozi wa dini mbali mbali pamoja na waumini wa dini zote hapa Zanzibar kuwa wastamilivu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezi.

Aidha, Waziri Aboud alisisitiza haja ya kuwepo uvumilivu kwa waumini wa dini zote ili kuirejesha Zanzibar katika historia yake ya kutokuwa na migongano ya kidini.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.