Habari za Punde

Hotuba ya Katibu Mkuu wa CUF semina ya madiwani wa CUF Chake, Pemba

HOTUBA YA KATIBU MKUU WA CHAMA CHA WANANCHI CUF, MHE. MAALIM SEIF SHARIF HAMAD KATIKA SEMINA KWA MADIWANI WA CUF ZANZIBAR, UKUMBI WA MAKONYO CHAKE CHAKE PEMBA TAREHE 18, FEBRUARI, 2013
Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi,
Waheshimiwa Wenyeviti na Makatibu wa Wilaya,
Waheshimiwa Madiwani, Viongozi na waalikwa nyote katika semina hii
Assalam Alaykum
Kwanza kabisa sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu mwenye wingi wa rehema kwa kutujaalia uhai na uzima na kutuwezesha kukutana hapa Gombani Pemba, katika semina iliyoandaliwa maalum kwa Madiwani wetu kwa lengo la kukumbushana wajibu na majukumu yetu katika kuwatumikia wananchi wa Zanzibar.
Pili napenda kuchukua fursa hii kutoa shukurani za dhati kwa waandaaji wa semina hii kwa maandalizi mazuri muliyotuandalia waalikwa na viongozi wote, maandalizi ambayo yametuwezesha kukutana hapa tukiwa ni wenye furaha.Mkusanyiko huo ni wa aina yake kwa sababu unawakutanisha viongozi viongozi na baadhi ya watendaji wa chama kutoka maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.

Aidha, nitakuwa mwizi wa fadhila kama sitatoa shukurani zangu nyingi na za dhati kabisa kwa wafadhili wa semina hii, ambao si wengine bali ni Taasisi ya Friedrich Naumann Foundation (FNF), kutokana na mapenzi na moyo wao wa imani kwa chama chetu, uliowawezesha kukubali kufadhili mafunzo haya muhimu sana kwa maendeleo ya wananchi wa Zanzibar.
Waheshimiwa Viongozi na Waalikwa wa Semina
Serikali za Mitaa nivyombo muhimu vya utawala vya wananchi ambavyo huanzishwa kwa lengo la kuwapa madaraka ya Kidemokrasia kuamua kuhusu mambo ya kimsingi yanayowahusu katika ngazi ya mitaa. Jamii hupewa madaraka ya kisiasa, kiutawala, kifedha n.k. Madhumuni ya kutolewa madaraka hayo yakiwa ni kuharakisha utoaji wa maamuzi juu ya maendeleo ya wanajamii wenyewe.
Hapa Zanzibar,Historia inathibitisha kuwa Serikali za Mitaa ni taasisi zilizokuwepo kwa muda mrefu huko nyuma. Inaelezwa kuwa hata kabla ya kuja kwa Wakolini, mfumo wa Serikali za Mitaa ulikuwepo. Na hata wakati wa Ukoloni vyombo hivyo, kutokana na umuhimu wake walivitumia kurahisisha utawala wao.
Katika uchaguzi wa kwanza wa Vyama vingi Zanzibar mwaka 1957, Serikali za Mitaa zilipewa umuhimu wa kipekee katika kufanikisha uchaguzi huo. Zanzibar iligawiwa maeneo ya Serikali hizo, kufuatia Sheria ya Serikali za Mitaa yaani “Local Government Decree” ya 1957, ambapo Madiwani walichaguliwa kwa mara ya kwanza kwa maeneo ya Baraza la Mji wa Zanzibar, Chake Chake, Mkoani, Wete, Mji wa Konde na mji mingine midogo kama vile Chwaka, Mkokotoni na Makunduchi,ambayo nayo ilikuwa na Mabaraza.
Katiba ya Zanzibar ya 1984 inatambua kuanzishwa kwa Serikali za Mitaa. Katika Ibara ya 128 ya Katiba hiyo inasema, Serikali za Mitaa zitaundwa kwa Sheria zitakazopitishwa na Baraza la Wawakilishi. Mwaka 1986, Sheria No. 3 ambayo ilianzisha rasmi Serikali za Mitaa ilitungwa. Sheria hiyo ndiyo iliyoanzisha Baraza la Manispaa Zanzibar na Mabaraza ya Miji Chake Chake, Wete, Mkoani pamoja na Serikali za Majimbo kila penye jimbo la Uchaguzi.
Katika kuleta ufanisi na utendaji mzuri zaidi katika taasisi hizo, mwaka 1995 zilitungwa Sheria mbili muhimu zinazohusu Serikali za Mitaa Zanzibar. Sheria hizo ni ile Na. 3 ambayo ni kwa ajili ya Baraza la Manispaa Zanzibar na Sheria Na. 4 ambayo ni mahsusi kwa ajili ya Halmashauri za Wilaya na Mabaraza ya Miji.
Hatua hiyo imeifanya Zanzibar kuwa na Serikali za Mitaa 13 ambazo kwa upande wa Unguja ni Baraza la Manispaa la Mji wa Zanzibar na Halmashauri za Wilaya tano zilizobakia.Na kwa upande wa Pemba zinajumuisha Mabaraza matatu ya Miji yaani Chake Chake, Mkoani na Wete pamoja na Halmashauri za Wilaya nne.
Madhumuni makuu ya kuanzishwa kwa Serikali hizi za Mitaa tunaweza kuyagawa katika sehemu nne ambazoni;
. Kukasimu madaraka ya Utawala na Uendeshaji kwa viongozi wa Serikali za Mitaa waliochaguliwa na wananchi wenyewe
. Kutoa huduma endelevu kwa manufaa na faida ya wananchi katika maeneo husika
. Kukusanya mapato pamoja na ada zitakazosaidia kuchangia miradi ya maendeleo katika maeneo yao
.Kuimarisha Utawala Bora unaojali misingi ya utawala wa sheria na Uwajibikaji.
. Kubwa ni kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa mambo yanayowagusa wananchi moja kwa moja yameletwa karibu nao kupitia Madiwani waliochaguliwa na wananchi wenyewe.
Kimuondo, Serikali za Mitaa zimejengeka kwa mihimili miwili kwenye uwajibikaji wake kwa wananchi kwenye eneo lake la Mamlaka, ambayo ni Wanasiasa, yaani Madiwani wa Kuchaguliwa, Wakuteuliwa na Viti Maalum na muhimili wa Pili ni Watendaji, ambao wanaongozwa na Mkurugenzi aliyeteuliwa na Rais kwa upande wa Baraza la Manispaa na Katibu wa Baraza la Mji na Halmashauri wanaoteuliwa na Waziri dhamana wa Serikali za Mitaa.Watendaji hao huunganana watumishi wengine kwenye Idara zao kulingana na hadhi na muundo wa Serikali ya Mtaa husika kutekeleza majukumu ya taasisi hizo.
Kwa mujibu wa Sheria, Waziri dhamana wa Serikali za Mitaa ndiye anayeanzisha Mamlaka hizi kwa kutekeleza matakwa ya Sheria husika. Diwani huchaguliwa kwa kura za siri kwenye Wadi katika uchaguzi unaosimamiwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Kwa upande mwengine, katika muundo wa Serikali za Mitaa, Meya, Naibu Meya wa Manispaa ya Zanzibar, Wenyeviti na Madiwani wa aina zote tatu ni wajumbe wa Halmashauri au Baraza la Halmashauri ya Mtaa.
Kwa mfano hivi sasa Zanzibar imegawanyika katika jumla ya Wadi 141, Madiwani Wanawake asilimia 30 pamoja na Madiwani tisa wanaoteuliwa na Waziri dhamana. Aidha, Mkurugenzi wa Manispaa na Makatibu wa Halmshauri ndio Makatibu wa Mabaraza ya Madiwani ambao hupaswa kutekeleza maamuzi halali ya vikao vya Serikali zao.
Waheshimiwa Viongozi na Waalikwa wa Semina
Baada ya kuelezakwa muhtasari, dhana ya Serikali za Mitaa na utekelezaji wa kazi zake, sasa nadhani tukumbushane japo kwa kifupi vile vile, nani Diwanina wajibuwake wa kiutendaji.
Kwa maoni yangu, Diwani niKiongozi wa wananchi aliyechaguliwa kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, Kuteuliwa au kupitia Viti Maalum. Kiongozi huyo ni kiungo baina ya wananchi katika Wadi na Halmashauri au Baraza analolitumikia.
Kiongozi huyo kama walivyo viongozi wengine, anatakiwa awe mwadilifu anayeheshimika mbele ya jamii, na kwa maana hiyo kuna umuhimu mkubwa kwa chama kinachotarajia kupata Diwani kuhakikisha mgombea wa nafasi hiyo, au mteuliwa anapimwa uwezo wake na chama chake, ili kupatikana kiongozi anayefaa na atakaye kipandisha hadhi chama kwa kutumikia wananchi kikamilifu.
Kwa muktadha huo basi, Diwani ana wajibumkubwa kwa Chama anachotoka, Serikali na wananchi anaowatumikia.
Miongoni mwa wajibu muhimu wa Diwani ni;
1. Kuhakikisha Sera za chama chake, Serikali na Sheria za nchi anazisimamia na zinafuatwa
2. Anatakiwa asikilize na kupokea shida na matatizo ya wananchi katika eneo lake
3. Awe na Ushirikiano wa karibu na watendaji wa Halmashauri, ili kuhakikisha kazi na majukumu zinatekelezwa ipasavyo
4. Anatakiwa ahoji na kupata taarifa za Uendeshaji wa Menejment za Baraza au Halmashauri ya eneo lake.Kwa mfano taarifa za Fedha, Utawala na Uendeshaji kwa jumla.
5. Ana wajibu wa kupitisha, kupokea na kudadisi Sheria ndogo ndogo, taarifa za mapato na matumizi, mipango ya maendeleo na bajeti za Halmashauri
6. Ni wajibu wake kushiriki vikao vyote halali vilivyoandaliwa na Halmashauri au Baraza.
Waheshimiwa Viongozi na Waalikwa wa Semina
Ili kuepusha mkanganyiko, maingiliaji na kupiga mstari wa kiutekelezaji majukumu kati ya Watendaji wa Serikali za Mitaa ni vyema pia tuone nini wajibu, kazi naninani hasa huyu kiongozi anayeitwa Sheha wa Shehiya.
Sheha anateuliwa kwa mujibu wa Sheria Na. 1 ya 1998 inayohusu Mamlaka ya Mikoa Zanzibar.
Kwa mujibu wa Sheria hiyo kifungu cha 17 (1), Sheha katika Shehia yake anabeba dhamana zifuatazo;
1. Kutekeleza Sheria zote za Serikali, Amri, Sera na maelekezo kwa ajili ya kudumisha Sheria na taratibu za nchi
2. Kusuluhisha na kutatua migogoro ya kijamii na kifamilia katika eneo lake
3. Kuweka kumbukumbu za nyaraka kuhusiana na usajili wa ndoa, talaka, vizazi na vifo, usafirishaji wa mazao, mifugo, makaa n.k
4. Udhibiti wa wahamiaji katika Shehia na kuweka kumbukumbu hizo
5. Kupokea taarifa za kufanyika mikutano yote ya hadhara
6. Kufanya mambo yote mengine ambayo ni halali kwa mujibu wa sharia na atakayoagizwa na Mkuu wa Wilaya.
Kutokana na Sheria na taratibu tulizo jaribu kuzieleza ni wazi tutaona kuwa Diwani ni Kiongozi wa Kisiasa katika Serikali ya Mtaa anayepatikana kwa mujibu wa Sheria za Uchaguzi, wakati Sheha ni Kiongozi wa Serikali anayemuwakilisha Rais katika Shehia yake. Lakini hata hivyo, utekelezaji wa majukumu yao una mahusiano makubwa katika kuwatumikia wananchi wa maeneo yao.
Kwa upande mwengine, tumeona kuwa viongozi hao yaani Madiwani na Masheha majukumu yao makubwa na ya msingi ni kuwatumikia wananchi katika maeneo yao. Ili malengo hayo yaweze kufikiwahawana budi kufanya kazi bega kwabega, lakini pia kwa mashirikiano makubwa na Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika maeneo hayo.
Kazi zao zinalinganana zina maingiliano, kwa sababu wakati Diwani anawakilishi wananchi wa eneo lake katika Mabaraza ya ngazi za Mitaa, na Sheha katika Shehia yake, Wabunge na Wawakilishi wanawawakilisha wananchi hao hao, katika ngazi ya vyombo vya kutunga Sheria vya juu zaidi, yaani Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Na ndio maana utaona hata katika Mfuko wa Jimbo ambao hupatiwa fedha kupitia Bungeni na Baraza la Wawakilishi, wadau wakuu wa utekelezaji wa mipango yaMfuko huo ni Madiwani pamoja na watendaji katika serikali za mitaa zilizopo katika jimbo hilo.
Madiwani ndio wafanya maamuzi katika Serikali ya Mtaa. Maamuzi yao ni lazima yaheshimiwe na Watendaji. Tatizo lililopo ni kuwa mfumo uliopo sasa unatoa mamlaka makubwa kwa watendaji, hasa Katibu wa Halmashauri au Mkurugenzi wa Baraza. Hawa wote wanateuliwa na viongozi wa Serikali ambao wanatokana na Chama Cha Mapinduzi. Mara nyingi huonekana kuwa Mkurugenzi au Katibu wa Baraza au Halmashauri kupuuza maamuzi ya Madiwani. Kama hilo halitoshi wakati mwengine Makatibu wa Halmashauri au Mkurugenzi wa Baraza ndiye anayefanya maamuzi juu ya mgao na matumizi ya fedha. Hakuna uwazi katika masuala ya fedha.
Nawasihi Madiwani wa chama chetu kutokubali kuburuzwa na watendaji. Lazima muhakikishe kuwa maamuzi yenu katika Mabaraza na Halmashauri yanaheshimiwa na kutekelezwa kwa ukamilifu. Lazima mujue matumizi ya kila senti moja. Lazima muhakikishe kuwa hakuna upendeleo katika ugawaji wa rasilimali kwa Shehia zilizomo katika Halmashauri au Baraza.
Endapo Katibu au Mtendaji hafuati maagizo ya Madiwani na anafanya atakavyo, lazima mumuarifu Waziri anayehusika, na kama Waziri atapuuza wasilisheni ripoti kwa Makamu wa Pili wa Rais. Ikiwa hakuna hatua itakayochukuliwa mkataeninamsite kufanya kazi naye.
Ukweli utaratibu wa uteuzi wa watendaji hao wa Mabaraza na Halmashauri unapaswa kutazamwa upya, ili kuwe na utaratibu utakao hakikisha kuwa watendaji wanaoteuliwa wanasifa waadilifu hawana maslahi ya kisiasa na waaminifu.
Baraza la Mji au Halmashauri ni kama Bunge au Baraza la Wawakilishi katika ngazi ya Serikali ya Mtaa husika. Hivyo inavyotakiwa ni kuwa chama chenye Madiwani wengi, ndicho kiwe kinaongoza Baraza au Halmashauri hiyo. Chama chenye Madiwani wachache kiwe ndio upinzani.Sina hakika kuwa mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa uliopo katika ngazi ya Taifa unatumika katika ngazi ya Halmashauri au Mabaraza. Ni vizuri hili kuanza kutazamwa, ili kuimarisha utaratibu wa kugawana madaraka.
Isitoshe kuna haja ya kuangalia majukumu na kazi za Madiwani kwa kulinganisha na kazi na majukumu ya Masheha, ili uwepo uwiano wa kimamlaka na kimadaraka. Inavyoonekana sasa hivi, kazi zote muhimu zimo katika mamlaka ya Mashehaambao ni wateule wa Mkuu wa Mkoa. Wale wawakilishi wa wananchi wamepwaya sana.
Ni kweli Mheshimiwa Ali Mohammed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika utekelezaji wa nia yake ya kuleta mashirikiano na mahusiano mema baina ya Masheha na Madiwani amesimamia semina za pamoja za Madiwani na Masheha kwa Unguja na Pemba. Sina hakika kuwa baada ya semina hizo hali imebadilika au la.
Jambo la faraja ni kuwa, sasa hivi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imo katika mchakato wa kuleta mageuzi (Reform) katika Serikali za Mitaa Zanzibar. Ni matumaini yangu kuwa mageuzi hayo yatarekebisha hali isiyoridhisha iliyopo sasa.
Waheshimiwa Viongozi na Waalikwa wa Senima
Wito wangu kwa Waheshimiwa Madiwani ni kuchapa kazi kwa bidii kwa kila mmoja wenu, na kuhakikisha anayafahamu, kuyasimamia na kuyatekeleza ipasavyo majukumu aliyokabidhiwa.
Wananchi katika maeneo yenu wanakabiliwa nashida nyingi, wanakabiliwa na hali ya umasikini uliokithiri, wengine wanakosa haki zao za msingi kutokana na udhaifu wa kiutendaji. Kuna hali isiyoridhisha ya uchafuzi na uharibifu mkubwa wa mazingira, ikiwemo kuzagaa kwa maji machafu kwa sababu ya kukosekana miundo mbinu au kuchakaa kwa muda mrefu, bila ya kufanyiwa matengenezo, na utupwaji wa taka ovyo.
Aidha, tuhuma za ubadhirifu, rushwa na utekelezaji wamajukumu yasiyowahusu, kama vile kuuza ardhi zimekuwa zikielekezwa sana kwa viongozi wa Serikali za Mitaa wakiwemo baadhi ya Madiwani na Masheha.
Hatuna budi kujiepusha na matatizo kama hayo, na tuweka mbele suala la Utawala Bora, Uwazi na Uwajibikaji. Tukizingatia hilo ndipo tutaweza kujenga heshima kwa chama chetu,mbele ya wananchi ambo tunawahitaji watuunge mkono.
Aidha, katika kuhakikisha wananchi wote wanapata haki zao, Madiwani, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Wabunge muhakikishe wananchi wote wanaokoseshwa vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi, au wale ambao wamekuwa na ajizi katika kuvitafuta, licha ya kuwa na sifa zote wanapata haki hiyo.
Najua changamoto kubwa iliyopo katika upatikanaji wa vitambulisho hivyo, hasa kutokana na baadhi ya watendaji kama Masheha na Maafisa wa Wilaya na wa Idara ya Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi kuwa na utashi wa kisiasa au kutumiwa na baadhi ya wanasiasa. Lakini tusichoke wala kuvunjika moyo. Sote kwa pamoja tuhakikishe tuna viruka vikwazo hivyo na tuhakikishe tunazisimamia haki za wananchi wote popote pale walipo.‘Ni vyema tukumbuke haki huletewi kwenye kisahani cha chai’.
Nakukumbusheni tena kuwa mafanikio katika utendaji wenu ni mafanikio ya Chama chenu. Wananchi watakupimieni baada ya miaka mitano, pale mtakapokuwa mumeonesha uwezo wa hali ya juu na mafanikio ya kupigiwa mfano katika utekelezaji wa majukumu yenu wataendelea kukuhitajini pamoja na chama chenu kiwaongoze.
Msisahau kuwa mlipokwenda kuomba ridhaa kwa wananchi katika Wadi zenu kwa Madiwani na kwa Wabunge na Wawakilishi katika majimbo yenu, mlibeba Manifesto ya Chama. Manifesto ambayo inahubiri haki sawa, maendeleo na maisha bora kwa wananchi wote.
Naamini kwa mashirikiano ya pamoja na kwa kuendeleza moyo, ari na bidii ya kuchapa kazi na kujitolea kutumikia watu, malengo yetu hayo tutaweza kuyafikia.
Waheshimiwa Viongozi na Waalikwa wa Senima
Sasa, baada ya kusema hayo, natanguliza tena shukurani zangu nyingi kwenu kwa kunisikiliza kwa makini kabisa katika muda wote nilipokuwa nikizungumza. Na sasa nafuraha kutamka, Semina hii nimeifungua rasmi.
Ahsanteni sana.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.