Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
RAIS wa Tanzania, Dk. Jakaya Mirisho Kikwete ameiagiza
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuhakikisha wananchi wanapata
vitambulisho kabla ya mwaka 2015 kwa sababu uchaguzi mkuu ujao watu watatumia
vitambulisho vya taifa kupiga kura.
Dk.Kikwete aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa
mfumo wa usajili na utambuzi wa watu na utoaji vitambulisho katika ukumbi wa
Karimjee jijini Dar es Salaam.
Aliwataka
watendaji wa Mamlaka hiyo kuwa waadilifu na wazalendo wa kweli ili kila
muombaji wa kitambulisho apate kile anachostahiki kupata.
Epukeni
makosa ya kumpa kitambulisho asiestahiki kuweni macho na watu wa aina hiyo,”
alitahadharisha Rais Kikwete.
Alisema
serikali haitaki kuona matatizo inayoyapata katika utoaji wa hati za kusafiria
(paspoti) yanajitokeza katika utoaji wa vitambulisho vya taifa kwa sababu
paspoti za Tanzania
zimekuwa zikikamatwa mara kwa mara zikiwa mikononi mwa watu wasiohusika.
“Kwa sababu
kule kwenye paspoti watu wasiohusika wanapatiwa paspoti kwa sababu watu wanatoa
kitu chochote,” alisema Rais Kikwete, akiwa na maana ya rushwa.
Hata
hivyo, alionya kuwa serikali haitakuwa na msalia mtume na mtumishi yoyote wa
NIDA atakaekamatwa akitoa kitambulisho kwa mtu asiestahiki na kusisitiza kuwa
kutoa kitambulisho kwa mtu asiehusika ni kosa kubwa la jinai.
Aidha
aliwataka Watanzania kuacha kutoa taarifa za uongo kwa sababu kufanya hivyo ni
kosa huku akiwataka viongozi wa dini, asasi za kiraia na waandishi wa habari
kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa vitambuliso hivyo.
Aidha
alisisitiza haja kwa wananchi kushirikiana kwa pamoja na serikali na wasivutane
kama ilivyotokea katika matukio yaliyopita ya
kitaifa.
Alisema
kufanikiwa zoezi hilo kunahitimisha ndoto ya
miaka mingi waliyokuwa nayo wa Tanzania
ya kupata utambulisho wao.
Alisema
serikali inapowatambua wananchi wake popote walipo duniani inakuwa rahisi
kuwahudumia na kuongeza kuwa suala la serikali kuwajua watu wake sio jambo la
hiari tena.
Nae
Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, alisema hatimae Watanzania nao wameungana na nchi
nyengine za Afrika Mashariki kupata utambulisho wao.
Alisema
lengo la NIDA ni kuhakikisha linatoa vitambulisho kwa Watanzania wote
waliofikisha umri wa kuanzia miaka 18, wageni wanaoishi nchini pamoja na
wakimbizi.
Alisema
vitambulisho hivyo vitarahisisha ufanyaji kazi wa taasisi nyengine kama RITA,
Ofisi ya Mrajisi wa vizazi na vifo Zanzibar, Idara ya Uhamiaji, polisi na
taasisi nyengine, lakini pia vitasaidia kujenga utawala bora wa kimamlaka.
Aidha
alisema itaisaidia serikali kufahamu raia wake walipo, anafanya nini na
anamiliki kitu gani pamoja na kurahisisha utambuzi wa watu.
Vitambulisho
hivyo vimetengenezwa kwa teknolojia ya kisasa ya smart card na havitaweza kughushiwa.
Viongozi
kadhaa walikabidhiwa vitambulisho vyao katika hafla hiyo akiwemo mwenyewe Rais
Kikwete, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Rais
mstaafu wa Zanzibar, Dk. Amani Karume na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin
William Mkapa.
Wengine
ni Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali
Hassan Mwinyi, Mama Fatma Karume, Mama Salma Kikwete, Mawaziri wakuu wastaafu, Dk.
Salim Ahmed Salim na Jaji Joseph Warioba, mke wa Waziri mkuu mstaafu wa awamu
ya tatu, Esta Sumaye, Anna Mkapa, mwanasiasa mkongwe Kingunge Kumbale Mwiru,
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na viongozi wengine na wawakilishi kutoka
mikoa mbali mbali.
No comments:
Post a Comment