Na Khamis Amani
SERIKALI
ya Mapinduzi ya Zanzibar, imewataka wananchi kuwa na ujasiri wa kuviripoti
vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wa kijinsia, ili sheria iweze kuchukua
mkondo wake.
Serikali
imefahamisha kuwa, vitendo vya aina hiyo havitoi taswira nzuri katika utamaduni
na ustaarabu wa nchi, hivyo wananchi wanapaswa kubadilika, kuachana na muhali
na badala yake wafuate sheria ili kukabaliana na vitendo hivyo.
Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, aliyasema
hayo bustani ya Victoria Vuga Mjini Zanzibar jana, katika maadhimisho ya siku
ya sheria Zanzibar.
Katika
maadhimisho hayo yaliyobeba ujumbe wa 'Kutokomeza unyanyasaji wa kijinsia', Dk.
Shein alisema, kwa mujibu wa taarifa na takwimu zilizopo suala la unyanyasaji wa kijinsia limekua ni tatizo
linaloendelea kuongezeka katika jamii, licha ya jitihada mbali mbali za
kulikemea na kulipiga vita zinazochukuliwa na serikali na washirika wengine.
Hata
hivyo, Dk. Shein alifahamisha kuwa, jamii
haipaswi kukata tamaa kwani hatua zilizochukuliwa zinatia moyo katika
kulishughulikia na ni wajibu wa jamii kuendelea kuongeza jitihada ili kulipatia
ufumbuzi wa kudumu.
"Nawasihi
wananchi wasikubali kurubuniwa na yeyote yule kwa ajili ya kuwaficha watenda
maovu haya, tukumbuke kuwa kuwaficha watu wa aina hii kunahatarisha maisha ya
watu wanaoishi karibu nao au jamii yote kwa ujumla," alitanabahisha Dk.
Shein.
Alisema
katika tafiti zilizofanywa na taasisi mbali mbali za kimataifa zimethibitisha
kuwa, tatizo la unyanyasaji wa kijinsia ni tatizo lililoenea duniani kote
ambapo waathirika wake wakubwa ni wanawake na watoto.
Alisema
Zanzibar ikiwa ni sehemu ya dunia, ni dhahiri inakabiliwa na kazi kubwa ya
kupambana na tatizo hilo, ambalo litakuwa kubwa zaidi ikiwa kutakosekana ushirikiano
katika kukabiliana nalo.
Katika
kukabiliana nalo, Dk. Shein aliwataka wananchi kuwa na imani na taasisi zao na
kuweza kujitokeza bila ya woga katika kutoa maelezo yatakayosaidia kupatikana
kwa ithibati itakayosaidia kupata ukweli, ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua
kali za kisheria.
Kwa
upande wa serikali, Dk. Shein alisema imechukua hatua mbali mbali za kuvizuwia
vitendo hivyo ikiwemo kuimarisha ustawi wa haki za watoto na wanawake nchini,
ikiwa ni pamoja na kutunga sheria ya hifadhi ya mtoto nambari 6/2011, kwa lengo
la kuzipa nguvu sheria zinazolinda haki zao hivi sasa na zile zilizokuwepo
kabla.
Aidha alisema
serikali imeweka mipango maalumu ya kuwasaidia wanawake na watoto, na kupitia
Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto pamoja na
Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika.
Alisema
serikali imeanzisha vituo maalumu vya kushughulikia vitendo vya udhalilishaji
wa kijinsia na kutoa ushauri nasaha katika hospitali ya Mnazimmoja, Chake
Chake, hospitali ya Cottage Kivunge na Makunduchi.
Hivyo alitoa
wito kwa wananchi kuzitumia huduma za vituo hivyo vinavyojulikana kama vituo
vya mkono kwa mkono, ambavyo vina wataalamu wa kushughulikia kesi za aina hiyo
wakiwemo madaktari, polisi, wanasheria na watoa ushauri nasaha.
Alisema
umefika wakati kwa vyombo vya sheria ikiwemo mahakama, waendeshaji mashitaka, polisi
na wananchi kwa ujumla kuwa pamoja na kujenga ushirikiano ulio imara zaidi kwa
lengo la kutokomeza unyanyasaji wa kijinsia.
Mapema
Dk. Shein alizindua jarida la mahakama na kuipongeza mahakama kwa juhudi zake
za kutoa elimu ya sheria kwa wananchi mbali mbali wa Unguja na Pemba, ambalo
litaweza kusaidia kueneza taaluma ya sheria kwa wananchi.
Mapema
Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu alisema vitendo vya unyanyasaji wa
kijinsia hasa ulawiti na ubakaji wa watoto wadogo vimekithiri kwa kiasi kikubwa
nchini.
Alisema
hilo linathibitishwa na takwimu za miaka mitatu kutokea mwaka 2009 ambapo kesi
38 zilifunguliwa mahakamani, kesi 50 zilifunguliwa mwaka 2010 na mwaka jana
2012 zilifunguliwa kesi 77, ambapo asilimia tatu tu ya kesi hizo washitakiwa
wake waliadhibiwa na asilimia 97 wameachiwa.
Alisema
hali hiyo haitii moyo kabisa na inawakatisha tamaa wananchi juu ya udhaifu wa
uendeshaji wa kesi hizo, na kuwaomba majaji na mahakimu kumuweka Mwenyezi Mungu
mbele wakati wa kuhukumu kesi za aina hiyo na nyenginezo, kwani mwisho wa siku
wataulizwa juu ya hukumu walizozitoa.
Nae
Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar, Awadh Ali Said alisema athari za matendo
ya unyanyasaji wa kijinsia haziishii kwa matokeo yaliyo dhahiri ya kimwili na
kiheshima tu, bali pia huambatana na athari za muda mrefu za kisaikolojia
ambazo huwa jinamizi linalomuandama muathirika na hata familia yake daima.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar (DPP), Ibrahim Mzee Ibrahim alisema
utokomezaji wa unyanyasaji wa kijinsia ni lazima uanzie kwenye malezi
yanayopatikana kwenye familia, ambazo ndio chuo kikuu cha malezi na maadili
katika jamii yoyote, na kufahamisha kuwa familia zikiharibika na jamii nayo
huharibika.
Kwa
upande wake Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Massoud kupitia hotuba yake
aliyosomwa na Mwanasheria wa ofisi yake, Hamisa Mmanga amezishauri taasisi
zinazohusika kusimamia kikamilifu sheria za nchi ili kutokomeza unyanyasaji wa
kijinsia unaoongezeka siku hadi siku.
Maadhimisho
ya siku ya sheria Zanzibar yalihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa serikali,
Majaji wa Mahakama Kuu, Mahakimu, Makadhi wa mahakama za Kadhi, Waendesha
Mashitaka, Mawakili wa kujitegemea na wadau wa sheria.
No comments:
Post a Comment