Habari za Punde

Wananchi watolewa hofu nafasi ya Masheha baraza, bunge la katiba



Na Mwantanga Ame
MWENYEKITI wa taasisi ya utafiti na sera za kijamii (ZIRPP) Mohammed Yussuf Mshamba, amesema wananchi hawapaswi kuwa na wasiwasi juu ya nafasi ya Masheha katika kuunda mabaraza ya bunge la katiba ya Jamhuri ya Muungano wakati utakapowadia.
 Mshamba  alitoa tamko hilo baada ya washiriki kuonesha mashaka kwamba iwapo Masheha watatumika kwa kazi hiyo mabaraza hayo huenda yakawa na sura ya chama kimoja.
Mwenyekiti huyo aliyasema hayo baada ya baadhi ya wadau wa taasisi hiyo waliojitokeza kutoa maoni yao juu mtazamo wao katika katiba mpya kikao ambacho kilifanyika Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Aliwaambia washiriki wa mkutano huo kwamba masheha watakuwa na jukumu dogo sana katika utekelezaji wa kazi hizo.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo alijikuta katika wakati mgumu kujibu maswali juu ya uamuzi wa tume hiyo kuyafanya siri
maoni juu ya Katiba mpya yanayotolewa na viongozi.
Wadau wa taasisi hiyo waliotaka kufahamu sababu za tume kufanya siri maoni ya viongozi wastaafu na wajumbe wa tume kuvuruga mtazamo wa wananchi kwa kuwaingilia wanapotoa maoni.
“Jambo hilo ni gumu kwangu, siwezi kulitolea maelezo,”  alisema na kuongeza “mimi nazungumza hapa kama mtendaji  wa ZIRPP.”
Abbas Juma Mhunzi, Mwakilishi wa zamani wa jimbo la Chambani  alisema utendaji wa tume unatia shaka hasa pale viongozi wake wanawapoingilia kwa kutokubaliana moja kwa moja na baadhi ya maoni yanayotolewa  na  wachangiaji mbele ya tume hiyo.
Mapema washiriki katika mkutano huo walilalamika kwamba katika mikutano kadhaa, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba  hakuwatendea haki wananchi kwa kuwaingilia watoa maoni akionyesha wazi kutokubaliana na mtazamo wao.
Maeneo yaliyotajwa kutokea kwa hali hiyo ni pamoja na Singida ambako Jaji Warioba alibishana na mtoa  maoni kwa kumwambia, mfumo wa serikali tatu anaotaka una gharama kubwa, hasa kwa kuzingatia tatizo la gharama za uendeshaji zinazoukabili hata huu wa serikali mbili.
Akimtetea Muhammed alisema kimsingi moja ya kazi za tume ni  kuwaongoza wananchi ili waweze kutoa maoni kwa usahihi na kuyaheshimu mawazo yao na kwamba anaamini hivyo ndivyo anavyofanya Jaji Warioba.

1 comment:

  1. Mimi naamini wasiwasi wa wananchi kwa masheha sio kua inaleta sura ya chama kimoja bali unatokana na iwango kidogo cha elimu walichonacho masheha.

    Z'bar imebaki sehemu pekee duniani ambapo elimu haipewi kipao mbele,...sasa wacha sisi tupeleke masheha, wenzetu wapeleke watu waliosoma baadae tuje tuseme tunaonewa.

    Waswahili husema "wajinga ndio waliwao"

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.