Na Husna Mohammed
WATOTO 1,500 kutoka Unguja na Pemba
walioacha masomo na kujishughulisha na ajira mbaya wanatarajiwa kurejeshwa
skuli mapema mwezi ujao.
Kati ya watoto hao wamo wengine walio
katika hatari ya kuacha skuli ambao wamekuwa wakitoroka mara kwa mara na kujishughulisha
na ajira kwa ajili ya kuipatia kipato cha kujiendesha familia zao.
Ofisa wa mradi wa Save the Childreen,
Hashim Pondeza, alisema hayo jana katika kituo cha Elimu Mbadala Rahaleo mjini
hapa, katika mafunzo ya waandishi wa habari juu ya kuelimisha jamii dhidi ya
madhara ya ajira mbaya kwa watoto.
Ofisa huyo alisema kufuatia utafiti
uliofanywa na taasisi mbalimbali zinazotekeleza mradi wa Save the Childreen
umebaini kuwa kati ya watoto hao 1,500 wanaume ni 984 na 516 ni wanawake.
Aliyataja maeneo ambayo watoto hao
wanatoka kuwa ni Micheweni na Majenzi katika Wilaya ya Micheweni, Kiuyu
Minungwini na Kangagani Wilaya ya Wete
ambapo jumla ya watoto 582 wamekwamuliwa katika ajira mbaya baada ya
utafiti uliofanywa na Jumuiya ya Pemba
Island Releef Organization
(PIRO).
Aidha alisema katika Mkoa wa Kusini Pemba,
imeweza kuwanasua watoto 500 katika vijiji vya Ndagoni, Wesha, Vitongoji,
Uwandani kufuatia utafiti uliofanywa na
jumuiya ya Kupunguza Umasikini na kukuza Hali ya Uchumi (KUKAHAWA).
Akizungumzia kwa upande wa kisiwa cha Unguja,
Pondeza alisema jumuiya COWPS na Chama cha Waandishi wa Habari wanawake
Tanzania Zanzibar (TAMWA), ambao walifanya utafiti katika Mikoa ya Kusini na
Kaskazini, alisema watoto 320 kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja kwenye vijiji vya
Mkokotoni, Nungwi, Pwani Mchangani na Kijini Matemwe wameweza kugundulikana
kuacha masomo.
“Watoto hawa wote tumeweza kuwanasua na
ajira mbaya ambapo wameacha masomo na wengine wako katika hatari ya kuacha
masomo tutawasaidia kwa sare za skuli na baadhi ya vifaa vya masomo ili
waendelee na masomo yao, zoezi ambalo litanza mapema mwezi ujao,” alisema.
Alisema pamoja na mambo mengine, mradi huo
pia utasaidia familia zenye mazingira magumu kwa ajili ya kuwapa mitaji ili
waweze kusaidia familia zao badala ya kutegemea watoto wao.
Naye Ofisa kutoka Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Amali katika Idara ya Elimu Mbadala na watu wazima, Halima Tawakali , alisema lengo
la wizara ya elimu ni kuhakikisha kuwa watoto wote wanapata elimu.
Alisema taratibu zote za kuwarejesha
watoto hao maskulini zimeshakamilika ikiwa ni pamoja na kuzungumza na walimu wa
skuli husika kuwapokea na kuwapa mashirikiano.
Aidha alisema pamoja na hayo lakini pia
Wizara imeandaa mpango wa kuwaelewesha wanafunzi kwa kuwapa ushauri nasaha
sambamba na kuandaa fomu za kufuatilia maendeleo ya ufahamu na elimu kwa
ujumla.
No comments:
Post a Comment