Na Rajab Mkasaba, Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk.Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa serikali itahakikisha inapeleka huduma muhimu kwa wananchi wanaoishi katika vijiji ambavyo huduma hizo hazijafika.
Dk. Shein aliyasema hayo baada ya kuzindua skuli ya msingi Kidagoni,shehia ya Kidoti Jimbo la Nugwi,wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja.
Dk. Shein alisema miongoni mwa huduma hizo ni elimu, afya, maji, umeme na nyenginezo ambazo ni muhimu kwa wananchi wa vijijini.
Alisema hayo yote yanawezekana iwapo wananchi wataanzisha miradi yao ya maendeleo na hatimae serikali kuwaunga mkono.
Wakati huo huo, Dk. Shein alizindua SACCOS ya Potoa na kusifu juhudi zao wanazozichukua katika miradi mbali mbali wanayoiendesha ikiwemo ushonaji, ufumaji, uuzaji wa dagaa, kilimo na shuguli nyengine za kimaendeleo.
Aliwasifu kwa kuanzisha ofisi yao wenyewe ili waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi na kufurahishwa na malengo waliyojiwekea ya muda mrefu katika kukuza SACCOS hiyo ikiwa ni pamoja na kuwaendeleza watoto wao wakiwemo wanafunzi wa maeneo hayo.
Katika uzinduzi huo, Dk. Shein alifanya harambee kwa ajili ya kusaidia SACCOS hiyo ambapo viongozi mbali mbali walitoa ahadi na fedha taslim shilingi miloni 10 zilichangwa, ambapo Dk. Shein alichangia shilingi milioni 7.
Aidha, Dk. Shein alizindua ukumbi wa mitihani katika skuli ya Pwanimchangani ambapo katika risala yao wananchi wa kijiji hicho walimueleza Dk. Shein kuwa ujenzi wa jengo hilo hadi ulipofikia umegharimu shilingi milioni 7.6 zikiwa zimetoka katika mfuko wa maendeleo wa Jimbo.
Dk. Shein aliwataka wanafunzi wa skuli hiyo kusoma kwa bidii ili waweze kufanya mitihani yao bila ya udanganyifu na kuweza kuutumia ukumbi huo na kuahidi kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali itamaliza ujenzi huo.
Kabla ya kuanza ziara yake, Dk. Shein alipokea taarifa ya Mkoa wa Kaskazini Unguja na ambayo ilieleza mafanikio na changamoto zilizopo ikiwemo migogoro ya ardhi ambayo mkoa huo ulieleza kuwa inaifanya kazi.
Akiwa katika kijiji cha Nungwi, Dk. Shein alitembelea mradi wa kufuga samaki wa aina mbali mbali wakiwemo kasa ambapo alisifu juhudi hizo za vijana hao ambao wameamua kufanya shughuli hizo na kujiajii.
Dk. Shein pia, alikagua vikundi vya wajasiriamali wanaofanya kazi za mikono na kuwasifu kwa juhudi zao huku akizitaka wizara ya Kazi Uwezeshaji Wananachi Kiuchumi na Ushirika na wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko kuwatafutia soko wajasiriamali hao.
maneno yangu yale yale hata kama umeyafuta ndugu mapara, ukweli haufichiki , na walio wakweli ndio wenye kufuzu ............
ReplyDelete