Habari za Punde

SMZ kuwakomboa wakulima

 
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, akizungumza na Uongozi wa Wizara ya KIlimo na Maliasili, katika utekelezaji wa kazi za Wizara hiyo katika Ukumbi wa mikutano Ikulu Mjini Zanzibar,( kushoto) Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi

 Baadhi ya Watendaji na maafisa wa Idara mbali mbali katika Wizara ya Kilimo na Maliasili,wakiwa katika ukumbi wa mikutano Ikulu Mjini Zanzibar,katika kikao cha Uongozi wa Wizara hiyo, chini mwenyekiti Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,ikiwa katika mpangilio wa Rais, kuzungumzia utekelezaji wa Kazi za kila Wizara,[Picha na Ramadhan
Othman,Ikulu.]
Na Rajab Mkasaba, Ikulu
 
MAPINDUZI ya Kilimo ndio mwelekeo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambayo yamelenga kutekeleza kwa vitendo dhamira ya kuwakomboa wakulima kutokana na kilimo duni chenye tija ndogo.
Hayo yameelezwa na uongozi wa Wizara ya Kilimo na Maliasili katika mkutano wa kuangalia utekelezaji wa mpango kazi kwa kipindi cha Julai 2012 hadi Machi 2013, uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd nao walishiriki pamoja na na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.
Uongozi huo, chini ya Kaimu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Ramadhan Abdalla Shaaban ulieleza kuwa mwelekeo huo wa Mapinduzi ya Kilimo unaweka mazingira bora ya uzalishaji mkubwa ili kuongeza mchango wa sekta katika pato la Taifa na kuwa na uhakika wa chakula na lishe bora.
Waziri Shaaban alieleza kuwa katika kipindi cha mwaka wa 2012/2013 Wizara inatekeleza dhamira ya Mapinduzi ya Kilimo yatakayopelekea kutoa mchango zaidi katika kukuza uchumi wa taifa sambamba na kupunguza umasikini.
Uongozi huo ulieleza kuwa miongoni mwa mikakati iliyowekwa na Wizara ni pamoja na kuimarisha zao la karafuu ikiwemo utafiti, uzalishaji, usarifu na branding kwa kushirikiana na Wizara inayosimamia biashara.
Kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji maji na kuhamasisha uvunaji wa maji ya mvua pamoja na ku jenga uwezo wa wajasiriamali katika kusarifu mazao ya kilimo na maliasili ili kukidhi mahitaji ya soko na mengineyo.
Wizara hiyo ilieleza kuwa sekta ya Kilimo na Maliasili bado zinaendelea kuwa ni muhimili mkuu wa uchumi wa Zanzibar ambao inatoa mchango wa moja kwa moja katika kujikimu kimaisha, kuwa na uhakika wa chakula, lishe na afya za wananchi walio wengi vijijini na kwa hivyo ina faida kubwa katika maisha.
Wizara ilieleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2011/2012 sekta hizi zilichangia asilimia 30 ya pato la Taifa na inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wanategemea sekta hiyo kwa kuwapatia ajira na mapato.
Ilielezwa kuwa pamoja na umuhimu uliopo kwa ukuaji wa sekta ya kilimo katika uzalishaji wa chakula bado haujaweza kufikisha katika hali ya kujitosheleza hasa kwa mchele ambao ndicho chakula kikuu kwa wananchi wa Zanzibar.
Katika kukiimarisha Chuo cha Kilimo cha Kizimbani, Wizara kwa kushirikiana na Norway imekamilisha mchakato wa ujenzi wa jengo moja la daghalia la ghorofa nne lenye vyumba 125. Pia kwa mashirikiano na Norway Wizara inaendeleza mradi wa sensa ya miti inayojumuisha taarifa kamili za mikarafuu, miti ya matunda na miti ya misitu.
Aidha, Wizara ilieleza kuwa imefanya tathmini ya mahitaji ya asali na kugundua kuwa mahitaji yameongezeka hadi kufikia tani 10 kwa mwaka hasa katika soko la utalii.
Pia, uongozi huo ulieleza kuwa Wizara inaendelea na utafiti wa mazao ya chakula na kushajiisha uzalishaji wa mbegu bora kwa mazao ya chakula kama mpunga, migomba na mazao ya mizizi hasa muhogo, viazi vitamu, viazi vikuu na utoaji elimu kwa wakulima.
Wizara hiyo ilieleza kuwa pamoja na jitihada za Wizara na Serikali kwa ujuml, baadhi ya changamoto zilizojitokeza ni mabadiliko ya hali ya hewa ambayo inaathiri kilimo hasa cha mpunga wa kutegemea mvua kutokana na kutokuwa na miongo isiyotabirika.
Nae Dk. Shein kwa upande wake alipongeza juhudi za Wizara hiyo na kusisitiza haja ya kuimarisha kwa kilimo cha mazao ya asili ambayo hivi sasa yamepotea kabisa yakiwemo mazao ya pilipili hoho, kungu manga, pilipili doria, mibura, chenza ajili, mabalungi, midanzi, chenza kangaja, chongoma, kunazi na mengineyo.
Kwa kutilia mkazo suala hilo Dk. Shein alitoa wito kwa Wizara hiyo kutoa elimu kwa wakulima na wananchi kwa ujumla kupanda mazao hayo na kuwashajiisha kama ilivyo kwa kilimo cha machungwa na embe hivi sasa.
Alisema kuwa mbali ya matumizi ya hapa nchini mazao hayo yanaweza hata kusafirishwa nje ya nchi na kuongeza pato la taifa.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alisisitiza kuwa kilimo hufanywa mashabani hiyo elimu kubwa inahitajika itolewe kwa wakulima pamoja na kueleza mafanikio yaliopatikana katika uendelezaji wa Shamba darasa huku akieleza kusikitishwa kwake na ukataji wa miti ovyo kwa ajili ya kutengenezea makaa hasa ile miti ya asili.

1 comment:

  1. Mbona nyimbo hiyo imeimbwa zamzni tu lakini hakuna kinachoendelea ni kutafuna fedha na kwenda mbele tu.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.