Habari za Punde

Spurs yaiduwaza City

 
LONDON, England
 
BAADA ya bao la Samir Nasri alilofunga dakika ya tano dhidi ya Tottenham Hotspurs jana kudumu hadi dakika ya 75 ya mchezo na kuonekana kama Spurs ingezama, upepo uliwageukia Manchester City na kujikuta wakilala kwa mabao 3-1.
 
Mabao matatu yaliyofungwa ndani ya dakika saba nyavuni mwa City, yalikuwa mwiba mchungu kwa kikosi hicho cha Mtaliana Robert Mancini baada ya kuwa na matarajio ya kushinda mchezo huo.
 
Matokeo hayo yanaifanya Manchester United kuzidi kuchekelea ikiwa na uhakika wa kutwaa ubingwa huo unaoshikiliwa na City.
 
Katika mchezo huo uliochezwa nyumbani kwa Spurs katika dimba la White Hart Lane, Nasri aliifungia timu yake bao safi katika dakika ya tano baada ya kazi nzuri ya Carlos Tevez.

Baada ya kupigana kwa nguvu kutaka kusawazisha ingawa ilikumbana na ulinzi mkali wa City.
 
Meneja wa Spurs Andre Villas-Boas, alifanya mabadiliko kwa kuwatoa na kuwaingiza wachezaji watatu kwa mpigo, hali iliyobadilisha pia kasi ya mchezo na kupelekea jahazi la City kuzama.
 
Clint Dempsey aliisawazishia Spurs katika dakika ya 75, kwa kiki murua baada ya kupokea pasi nzuri na Gareth Bale ambaye amerudi baada ya kupona majeraha.
 
Wakati City wakijiuliza kilichotokea, haikuchukua muda mrefu kwa nyavu zao kuchanwa tena, mara hii Jermain Defoe akipachika bao katika dakika ya 79 na kuwafanya wenyeji kuongoza 2-1.
 
Bao hilo lilizidi kuwachanganya matajiri wa Etihad, na kutoa mwanya kwa wenyeji wao kujifaragua kwa bao la tatu lililofungwa na Gareth Bale mnamo dakika ya 82, hali iliyoamsha furaha kwa mashabiki wa Spurs waliokuwa wameanza kukata tamaa ya kushinda.
 
Matokeo hayo yanamaanisha United itajitangazia ubingwa kama itashinda Aston Villa katika uwanja wake wa Old Trafford leo usiku.
 
Kwa ushindi huo, Tottenham imefikisha pointi 61 ikiwa katika nafasi ya tano, sawa na Chelsea iliyoko nafasi ya nne, nyuma ya Arsenal inashuka nafasi ya tatu ikiwa na pointi 63 lakini imetanguliwa kwa mchezo mmoja dhidi ya wawili hao waliocheza mechi 33 kila moja.
 
Chelsea ilikuwa ikicheza na Liverpool jana
Gareth Bale (Tottenham), akicheza mara ya kwanza baada ya kuwa nje akiuguza kifundo cha mguu, alikuwa nyota wa mchezo huo, akitengeneza bao la Dempsey la kusawazisha, kabla naye kuandika bao lake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.