SERIKALI ya Zanzibar, imesema inajiandaa kuendeleza zoezi la kuwahamisha wahasibu wakuu katika idara mbali mbali za serikali.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee, aliyasema hayo jana wakati akijibu hoja mbali mbali za wajumbe wa baraza la wawakilishi, ambao waliiomba serikali kufanya mabadiliko ya wahasibu wakuu katika idara za serikali.
Wawakilishi hao walisema wamekuwa na wasiwasi wa utendaji wa baadhi ya wahasibu wakuu kwa kuonekana kulewa madaraka na kushindwa kufanya kazi zao vizuri na kusababisha upotevu wa fedha za umma.
Waziri Yussuf alisema zoezi hilo litafanywa kwa wahasibu wote ambao bado hawajahamishwa baada tu ya kumaliza kuandaa bajeti ya wizara na idara wanazozisimamia.
Alisema zoezi hilo limeanza kufanyika katika idara mbali mbali za serikali ambapo hivi sasa wamefikia asilimia 50 ya kazi.
Alisema serikali imeamua kufanya hivyo kutokana na kupokea mawazo mbali mbali ya wajumbe hao na taasisi mbali mbali nchini ambapo pamoja na kuchukua hatua hiyo inajiandaa kuiangalia sheria inayowasimamia wahasibu.
Akizungumzia suala la urasimu katika Mamlaka ya Uimarishaji Vitega Uchumi (ZIPA), alisema serikali ilifanya makosa katika matayarisho ya taasisi hiyo kwa kuweka watu ambao hawakuwa na uwezo wa kutoa maamuzi.
Aidha, Waziri huyo, alisema masuala yanayohusu mambo ya Muungano hayahitaji kutumia nguvu bali jambo la msingi ni kwa watendaji wa serikali ya Zanzibar kujenga hoja za msingi.
No comments:
Post a Comment