Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Mkuu wa Divisheni ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa Kimataifa katika Idara ya Biashara ya Jimbo Heilongjiang Nchini China Bwana Li Leyu Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Bwa Li Leyu akiuongoza Ujumbe wa Viongozi wane wa Idara hiyo upo Zanzibar kati a azma ya Idara yao kutaka kuwekeza Vitega Uchumi katika Viwanda vya mazao ya Baharini { Kamba na Samaki }.Picha na Hassan Issa na – OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Idara ya Biashara kupitia kitengo chake cha ushirikiano wa Kiuchumi wa Kimataifa katika Jimbo la Heilongjiang Nchini China inakusudia kuwekeza katika sekta ya Viwanda vitakavyozalisha Mazao ya Baharini hatua ambayo imekuja kufuatia mazingira mazuri yaliyopo ya Bahari ya Hindi iliyovizunguuka Visiwa vya Zanzibar.
Mkuu wa Divisheni ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa Kimataifa katika Idara ya Biashara ya Jimbo hilo Bwana Li Leyu alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Bwana Li Leyu aliyeuongoza Ujumbe wa Viongozi Wanne wa Idara hiyo alisema kwamba mradi huo wa uwekezaji utakwenda sambamba na utoaji taaluma kwa wavuvi wadogo wadogo ukilenga kuwa na uzalishaji wa kimataifa kwa kushirikisha pande zote mbili.
“ Mradi wetu utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kutoa ajira zisizopunguwa mia tano kwa wavuvi wazalendo na ndio maana tukasisitiza zaidi suala la Taaluma kabla ya kuanza kwa mradi na hatimae uzalishaji. Tumekusudia Mradi wetu uwe wa mfano, bora na wa mwanzo katika mwambao wa Afrika Mashariki “. Alifafanua Bwana Li leyu.
Mkuu huyo wa Divisheni ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa Nje katika Idara ya Biashara ya Jimbo la Heilongjiag Nchini China Bwana Li alifahamisha kwamba wataalamu wa kufanya utafiti wa kuendesha mradi huo watafika Nchini mara baada ya kuridhiwa pamoja na kukamilika kwa taratibu zilizowekwa za uwekezaji Nchini.
Bwana Li Leyu alieleza kuwa Zanzibar itakuwa na uwezo wa kuzalisha kiwango kikubwa cha mazao ya Baharini ikiwemo samaki na Kamba mazao ambayo yana pato kubwa katika masoko ya kimataifa hasa eneo la Bara la Asia.
Alieleza kwamba mradi huo mkubwa ulioelekezwa ndani ya kanda ya Afrika Mashariki ukiilenga zaidi Zanzibar unaweza kuwa tayari ndani ya kipichi cha kati ya miaka miwili hadi mitatu tokea utapoanza ujenzi wa Viwanda vyake.
Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliushukuru Uongozi wa Idara hiyo ya Biashara ya Jimbo la Heilongjiang Nchini China kwa mtazamo wake wa kuiona Zanzibar ndio mahali panapostahiki kuwekezwa mradi huo wa mazao ya Baharini.
Balozi Seif alisema huo ni mradi mzuri utakaoleta faraja kwa Serikali katika harakati zake za kuongeza ajira kwa wananchi na hasa lile kundi kubwa la vijana wanaomaliza masomo yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhakikishia Uongozi huo wa Idara ya Baishara ya Jimbo la Heilongjiang kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa tayari kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuona mradi huo unasimama na kufanya kazi hapa Zanzibar.
“ Bidhaa za Kamba na Samaki tumekuwa tukizishuhudia ughali wake katika masoko ya Kimataifa. Sasa kuwepo kwa mradi huu hapa Nchini kutasaidia kuongeza pato la Taifa na kupunguza ukali wa maisha kwa wavuvi watakaobahatika kufanya kazi katika kiwanda hicho “. Alisisitiza Balozi Seif.
No comments:
Post a Comment