Na Mwandishi Wetu
TUME ya Mabadiliko ya Katiba imesema haimzuii mwananchi, asasi au taasisi yoyote kufungua kesi mahakamani kupinga au kuzuia mchakato unaoendelea wa katiba mpya.
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba ametoa ufafanuzi huo kwa baadhi ya waandishi wa habari waliofika ofisini kwake jijini Dar es Salaam kutaka ufafanuzi wa masuala mbalimbali yaliyotolewa na Jukwaa la Katiba jijini Dar es Salaam juzi.
Katika tamko lake, Jukwaa la Katiba kupitia kwa Mwenyekiti wake, Deus Kibamba alieleza nia ya asasi yake kufungua kesi mahakama kuu ndani ya siku saba kusimamisha mchakato wa katiba mpya kutokana kile ilichodai ni kasoro zinazojitokeza katika mchakato wa katiba unaoendelea.
Hata hivyo, Jaji Warioba alisema Tume yake haina tatizo na mtu au asasi kwenda mahakamani kwa kuwa hiyo ni haki yao ya kikatiba.
“Nimesoma tamko lao na niseme tu halina jipya. Hii si mara ya kwanza kusikia hili (la kwenda mahakamani), na jibu letu lilikuwa waende na ndio jibu letu hadi sasa,” alisema Jaji Warioba anayeongoza Tume hiyo iliyoanza kazi Mei 2 mwaka jana.
“Mimi nasema waende ili tujue Jukwaa haswa ni nani, kwa sababu ninafahamu ni mkusanyiko wa asasi mbalimbali na baadhi ya asasi hizo hizo zimetuletea maombi ya kuunda mabaraza ya katiba ya taasisi na asasi,sasa jukwaa hili ni nani haswa?,” alisema Jaji Warioba.
Kuhusu marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba, Jaji Warioba alisema ingawa marekebisho ya sheria hiyo sio jukumu la Tume, wanafahamu kuwa serikali ipo katika mchakato wa kurekebisha sheria hiyo kama ilivyoahidiwa.
“Hili la marekebisho ya sheria ingawa sio jukumu letu, lakini nalo sio jipya. Wote tulimsikia Waziri Mkuu hivi karibuni kule Bungeni akisema serikali inaandaa marekebisho ya sheria hiyo yatakayowasilishwa bungeni, sasa hawa wanataka nini?,” alihoji Jaji Warioba.
Kuhusu, mchakato wa katiba kukosa uongozi madhubuti, Mwenyekiti huyo alisema Tume yake imeundwa na watu wenye sifa, weledi na uadilifu mkubwa ambao wametokana na mapendekezo ya wadau mbalimbali yakiwemo makundi, vyama, asasi mbalimbali za kijamii na kiraia.
“Mimi najivunia kuongoza Tume yenye watu wenye weledi na uadilifu mkubwa na wananchi wanalifahamu hili na kwa kweli wanatuunga mkono,” alifafanua Jaji Warioba.
Katika mahojiano hayo, Jaji Warioba pia alifafanua kuhusu muda ambao Tume yake inatarajia kutoa Rasimu ya Katiba kwa lengo la kujadiliwa na kutolewa maoni katika mabaraza ya katiba.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, hivi sasa Tume inaendelea kuandaa rasimu ya katiba na wananchi watapata muda wa kutosha kuijadili na kutoa maoni yao.
“Mpango wa Tume ni kukamilisha kazi zake ndani ya muda uliopangwa na sheria, tutatoa rasimu ya katiba katika muda ambao utatosha kuwafanya wananchi na wajumbe wa mabaraza ya katiba kuisoma,” alifafanua Jaji Warioba.
Jaji Warioba pia alielezea kushangazwa kwake na kauli za wadau mbalimbali kuhusu utendaji kazi wa Tume na kusisitiza kuwa wananchi na wadau wengine wasubiri rasimu ya katiba itolewe ndipo watoe maoni.
“Nadhani itakuwa ‘fair’ (sawa), tukishatoa rasimu ndiyo watu watuhukumu,” alifafanua Mwenyekiti huyo ambaye pia alishawahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kuhusu madai kuwa wananchi waliochaguliwa kuwa wajumbe wa mabaraza ya katiba ya Wilaya hawana uwezo na weledi wa kujadili na kutoa maoni kuhusu rasimu ya katiba, Jaji Warioba alisema madai hayo hayana msingi na yanabeza maamuzi ya wananchi.
Alisema uamuzi wa Tume kushirikisha wananchi kuanzia ngazi ya mitaa, vijiji, vitongoji na shehia ulilenga kuwapa fursa ya kuchaguana na kuongeza kuwa wananchi walitumia fursa hiyo vizuri.
“Wanaosema haya wanawabeza wananchi waliowachagua hao wajumbe,” alisema Mwenyekiti huyo na kuongeza kuwa taarifa ambazo Tume yake imezipata zinaonesha katika wajumbe hao kuna wananchi wasomi na wenye weledi wa kutosha kujadili rasimu ya katiba.
Warioba usidanganye wananchi sema ukweli yale yaliyotokea zanzibar wakati wa uchaguzi wa mabaraza ilikua Luna yako pale au ndio unajikosha na jamaa zako wa kihafidhina nyama ww
ReplyDeletebara'baraa , kabisa kabisaaa
ReplyDeleteKatiba hiyooooooo!!!Wapi uwamsho na wafuasi wao wanaotaka 'nkataba'?
ReplyDeleteHawana haya mkataba, ukowapi? mapanga yako wapi? wamebaki na fitinatu...Nkataba haupo
ReplyDelete