Habari za Punde

Ameir aota pembe

 
 Adai hata serikali haina ubavu kuivunja ZFA
Na Mwandishi Wetu
SIKU tano kabla ya uchaguzi mdogo wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Kaimu Rais wa chama hicho Haji Ameir Haji, amesema hakuna mtu yeyote mwenye ubavu wa kuivunja ZFA.
Ameir alikuwa akizungumza katika kipindi cha ‘Sports Michezo’ kilichorushwa juzi Jumamosi saa tatu usiku katika televisheni ya Shirika la Utangazaji Zanzibar.
Akionesha jazba na kukerwa na maoni ya wadau wa soka wa Zanzibar wanaotaka kuvunjwa kwa chama hicho, Ameir alisema hata serikali haina uwezo wa kuufuta uongozi wa ZFA.  
Alisema chama hicho kinaendeshwa kwa mujibu wa katiba yake, ingawa alikiri kuwa ina kasoro nyingi na haikidhi matarajio ya wananchi wa Zanzibar.
Alieleza kushangazwa na kelele za wadau ambao alisema walikuwa na klabu zao lakini wameziacha zimekufa kwa kuwa nao hawana upeo wa uongozi, kisha hudai soka limeporomoshwa na ZFA.
“Tumeandaa uchaguzi wa Rais ili watu wajitokeze kugombea, hawaji kuchukua fomu lakini ajabu wanakaa nje kufanya ghasia, Nasema ZFA iko imara na wala hakuna wa kuivunja”, alijigamba Ameir.
Ameir ambaye pia ni Makamu Rais wa ZFA Unguja, alikuwa akizungumza kwa ghadhabu akiwataka wadau waache maneno ya chokochoko kwamba chama hicho kina mgogoro.
Alifahamisha kuwa, ZFA iko tayari kutoa shilingi milioni kumi kwa ajili ya kugharamia mdahalo wa wadau wa soka, ili kila upande ueleze joto lake juu ya hali ya soka la Zanzibar.
Ameir aling’ang’ania kauli yake ya kila siku kwamba mpira wa miguu Zanzibar umepiga hatua kubwa ya maendeleo, kwa kuwa ligi kuu na za madaraja mengine zinaendelea kuchezwa bila ya matatizo yoyote, pamoja  na msimu uliomalizika kutolewa zawadi kwa washindi.
Alihitimisha kwa kusema, ZFA ina wanachama wake, na kuwataka wasiokuwa hao, kujiweka mbali na chama hicho ili wakiache kifanye kazi ya kuendeleza soka

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.