Habari za Punde

Mwanafunzi kuukwaa urais ZFA?

Anamalizia digrii ya sheria Tunguu
Anapambana na Mwanasheria, Mhasibu, 
 
Na Salum Vuai, Maelezo
MWANAFUNZI Rajab Ali Rajab anayetarajia kumaliza masomo ya digrii ya kwanza ya sheria katika Chuo Kikuu cha Tunguu, amepania kuibuka na matokeo ya kushangaza katika uchaguzi mdogo wa urais wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA). 
Akizungumza na gazeti hili jana, Rajab (32), alieleza kuwa, wanamichezo wa Zanzibar wamechoka na uendeshaji usioridhisha ndani ya ZFA, hivyo wanahitaji Rais mpya na asiyetokana na kamati za chama hicho ambazo zimeishiwa na fikra mpya za kimaendeleo.
Rajab anayetarajia kuhitimu baada ya wiki mbili, alikiri kuwa yapo mazuri kadhaa yaliyofanywa na uongozi wa ZFA, lakini akasema wamefeli katika mambo mengi ya msingi, ikiwemo kuwa na kamati tendaji mbili hali inayoibua mtengano kati ya Unguja na Pemba.
Alieleza kuwa, iwapo atachaguliwa, atahakikisha kunakuwa na ZFA moja kitaifa, na uongozi wake na wadau watafanya kazi pamoja ili kurejesha haiba ya soka la Zanzibar.
Amesema ingawa wengi wanamuona ni mgeni kwa kuwa hawamfahamu, lakini ana uzoefu katika soka, akiwa miongoni mwa wachezaji waliippandisha ligi kuu timu ya Zimamoto mwaka 2006 wakati akiwa mwanafunzi wa sekondari, kabla hajaanza masomo ya sheria mwaka 2009.
Katika kinyang’anyiro hicho, Rajab anapambana na Ravia Idarous Faina (42), mwenye taaluma ya mambo ya fedha na akiwa Mhasibu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), ambaye juzi Jumamosi alianza na kumaliza kunadi sera zake kisiwani Pemba katika wilaya zote nne.
Mgombea huyo ambaye ni mjumbe wa Kamati Tendaji ya ZFA kwa miaka saba sasa, aliahidi mambo tafauti ikiwa pamoja na kuhuisha uhusiano wa ZFA na Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar, aliodai kuwa imeanza kuingia sumu kutokana na utendaji mbovu wa uongozi wa sasa wa chama hicho.
Ravia alitarajiwa kurejea Unguja jana kuendelea na kampeni kwa wapiga kura wa hapa, katika kujisafishia njia ya kunyakua urais wa ZFA uliobaki bila mwenyewe baada ya kujiuzulu kwa Amani Ibrahim Makungu mwishoni mwa Januari mwaka huu.
Mjumbe mwengine wa kamati tendaji ya ZFA na  Mwanasheria wa chama hicho Abdallah Juma Mohammed, juzi alikutana na wapiga kura wa wilaya zote sita za Unguja na kumwaga yale anayokusudia kuyafanya endapo atachaguliwa.
Juma (53), ameahidi kuwafuta machozi wadau wa soka kwa kuhakikisha katiba ya ZFA inafanyiwa marekebisho makubwa ili iendane na wakati na kwa maslahi ya nchi na wanamichezo wote.
Mgombea huyo mwenye taaluma ya sheria ambaye amepata umaarufu mkubwa kwa kutoa mchango wake wa utetezi kwenye kesi nyingi hapa nchini, aliahidi kuijenga ZFA ili kiwe chama kinachoaminika kitaifa na kimataifa.
Aidha alisema kwa kipindi chake kifupi cha kuwemo kwenye kamati tendaji ya ZFA baada ya kuvutwa na Rais aliyejiuzulu Amani Makungu, ametoa mchango mkubwa katika kuendeleza soka la Zanzibar.
“Ingawa nimekuwa ZFA kwa kipindi kifupi, niliyofanya ni mengi na yanaonekana na kila mmoja, ninawaomba wapiga kura wanichague ili tuendeleze tuliyoanza na wenzangu”, alisema.
Hata hivyo, alisema anatarajia uchaguzi utakwenda kwa uadilifu, na kwamba pamoja na matarajio ya a kushinda, lakini hali ikitokea vyenginevyo, amesema  atakubali matokeo na kumpongeza mshindi.
Uchaguzi mdogo wa Rais wa ZFA, umepangwa kufanyika Jumamosi ya Juni 8, mwaka huu katika hoteli ya Zanzibar Ocean View Kilimani mjini Zanzibar.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.