Habari za Punde

Juhudi zaidi zahitajika kupambana na UKIMWI, Malaria

Na Khamis Salum
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Fatma Ferej, amesema ingawa Zanzibar imepiga hatua katika kudhibiti ugonjwa wa malaria, lakini bado juhudi zinahitajika kuhakikisha ugonjwa huo unatokomezwa kwa vile ni kikwazo kwa ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii nchini.

Hayo aliyaeleza katika ufunguzi wa uwasilishaji wa taarifa za awali ya hali ya malaria nchini kutokana na utafiti wa viashiria vya ukimwi na malaria wa mwaka 2011-12 huko Zanzibar Beach Resort.

Alisema, ugonjwa wa malaria huua watu wengi katika nchi nyingi zinazoendelea ikiwemo Tanzania na hususani watoto na akinamama wajawazito, mikakati ya lazima inapaswa kuwekwa katika kupunguza maambukizi ya malaria.

Hata hivyo, Waziri Fatma, alisema serikali imefanya juhudi kubwa kupunguza kiwango cha maambukizi ya malaria.

"Lazima tuhakikishe kwamba tunaendelea kuyalinda mafanikio na tudhamirie kukamilisha kabisa uangamizaji wa malaria," alisema.

Juu ya hali ya ukimwi, alisema, nchi ikiwa na wagonjwa wengi ni dhahiri kuwa uzalishaji utapungua na gharama za matibabu zitakuwa kubwa.

Aidha, alisema ugonjwa wa Ukimwi unasababisha mgogoro mkubwa kijamii na umasikini kwa familia kutokana na gharama kubwa za kuuguza muda mrefu na kuongeza watoto yatima pamoja na wazee wasiokuwa na msaada.

Madhumnuni makuu ya utafiti huo yalikuwa ni kupata takwimu sahihi na sasa juu ya ufahamu na tabia kuhusiana na ukimwi na malaria, kiwango cha maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa wanawake na wanaume wenye umri wa miaka 15-49 na kupata kiwango cha maambukizi ya malaria na upungufu wa damu kwa watoto wenye umri wa miezi 6-59.

Kwa mujibu wa utafiti huo, umeonesha kwamba kiwango vya maambukizi ya VVU Tanzania, kwa wanawake na wanaume wenye umri 15-49 kwa mwaka 2011-12, kimepungua hadi kufikia asilimia 5-1.

Kwa upande wa Zanzibar, kiwango cha maambukizi ya VVU ni asilimia 1% ambapo wanawake ni asilimia 1.1 na wanaume asilimia 0.9.

Kiwango cha maambukizi ya ukimwi kwa upande wa Zanzibar kimepanda kutoka asilimia 0.6 kwa takwimu zilizopatikana kwa utafiti uliofanyika mwaka 2007/08 mpaka asilimia 1% mwaka 2011/12.

Alisema, ongezeko hilo ni kubwa, hivyo jitihada zinahitajika kupambana na sababu na vishawishi vyote vilivyopelekea kuongezeka kwa ugonjwa huo.

Alisema kiwango kikubwa cha maambukizi ni kikubwa zaidi katika mkoa wa Mjini Magharibi, ambapo una kiwango cha asilimia 1.4 miongoni mwa wanawake na wanaume wenye umri wa miaka 15 hadi 49.

Kwa upande wa malaria, utafiti umeonesha kiwango cha maambukizi ya malaria kwa wototo wenye umri miezi 6-59 Zanzibar ni chini ya asilimia 1%.

Mikoa inayoongoza kwa asilimia kubwa (asilimia moja) ni mkoa wa Mjini Magharibi na Kusini Unguja.

Hivyo, alisema, takwimu hizo zinatoa faraja kwa vile maambukizi yanaonekana ni madogo, na hiyo inatokana na jitihada za serikali kufanikiwa kupambana na malaria hasa watoto wadogo na akinamama wajawazito.

Zaidi ya upimaji wa malaria, watoto pia walipimwa damu ili kuweza kujua kiwango cha upungufu wa damu, ambapo utafiti umeonesha kwamba asilimia 4 ya watoto Zanzibar wenye miezi 6-59 wana wastani wa upungufu wa damu na upungufu mkubwa wa damu.

Mkoa unaoongoza kwa kuwa na watoto wengi wenye upungufu wa damu ni Kaskazini Unguja kwa kuwa na asilimia 9.

Mikoa ya Mjini Magharibi na Kusini Pemba imeonekana kuwa na asilimia ndogo za watoto wenye upungufu wa damu (asilimia 3 tu).

Waziri Fatma, alisema, matokeo ya utafiti huo ni changamoto kwa taifa katika juhudi zake za kupunguza na kutokomeza malaria kwa watoto pamoja na kuboresha lishe ya watoto na kupunguza maambukizi ya VVU.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.