Na Kija Elias, Lushoto
HOSPITALI ya wilaya ya Lushoto, mkoani Tanga inakabiliwa na uhaba wa majengo ya wodi ya mama na mtoto hali inayosababisha wagonjwa kulala zaidi wawili katika kitanda kimoja na wengine kulala chini.
Pia hospitali hiyo inakabiliwa na upungu mkubwa wa mashuka na mablanketi hali inayowalazimu wagonjwa hao kujifunika mashuka yakiwa hayajakauka.
Hayo yamebainishwa na Ofisa Tabibu Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. Gasto Stephano wakati wa akipokea msaada wa mashuka yaliyotolewa na Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) tawi la Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (SEKOMU) na kusema hospitali hiyo inakabiliwa na uhaba wa wodi ya mama na mtoto kutokana na majengo yake kujengwa tangu mwaka 1961.
Dk. Stefano alisema majengo yaliyoko kwa sasa hayakidhi mahitaji ya wagonjwa kulingana na idadi yao kuongezeka na kuzidi kiwango kilicho kasimiwa wakati wa ujenzi.
“Asilimia 85 ya wagonjwa wanaitegemea hospitali yetu na katika wodi ya mama na watoto, wanaitegemea hopitali hii lakini kutokana na ufinyu wa majengo, inatulazimu kuwalaza wawili hadi watatu na wengine chini,” alisema.
Aidha alisema hospitali kwa sasa ina mpango mkakati wa kujenga jengo la ghorofa mbili ambalo litagharimu kiasi cha shilingi bilioni mbili ili kuweza kupunguza tatizo la rundikano wa wagonjwa katika wodi hiyo.
Alisema jengo hilo litakuwa na sehemu ya upasuaji, sehemu ya mama na matoto na matunzo kwa watoto wanaozaliwa kabla ya muda wa kawaida.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVCCM, tawi la Chuo cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (SEKOMU), Mrisho Kitunga, alisema kama wasomi wameguswa na tatizo lililoko katika wodi ya mama na mtoto hospitalini hapo.
No comments:
Post a Comment