Habari za Punde

Akamatwa akimbaka bibi wa miaka 70


Na Khamis Amani
KIJANA wa miaka 30 mkaazi wa Maungani Langoni, wilaya ya Magharibi Unguja, amelazwa katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja kwa matibabu baada ya kupigwa na wananchi wenye hasira, kwa tuhuma za kumbaka bibi wa miaka 70.

Kijana huyo Juma Mwandu Ngasa ambaye anasadikiwa kuwa maarufu wa vitendo vya ubakaji, alishambuliwa na kujeruhiwa sehemu mbali mbali za mwili wake, pamoja na kukatwa mishipa ya nyuma ya miguu.

Amelazwa katika hospitali kuu ya Mnazimmoja akiwa chini ya ulinzi wa Polisi na anatarajiwa kusomewa mashitaka hayo mapema wiki ijayo.

Tukio hilo lilidaiwa kutokea Juni 2 mwaka huu majira ya saa tisa usiku, wakati kijana huyo alipofika nyumbani kwa bibi huyo (jina tunamuhifadhi) kwa lengo la kutaka kumbaka.

Lengo lake hilo lilifanikiwa lakini hakuweza kumaliza matamanio yake baada ya wananchi kufika katika eneo la tukio kufuatia taarifa waliyopelekewa kutoka kwa mjukuu wa bibi huyo na kumtia nguvuni na hatimae kumshushia kipigo hicho.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Mkadam Khamis Mkadam alithibitisha tukio hilo na kusema upelelezi wake bado unaendelea.

Akielezea chanzo cha tukio hilo Kamanda Mkadam alisema, kijana huyo alifika nyumbani kwa bibi huyo na kuingia ndani baada ya kufungua mlango uliotengenezwa kwa madebe ulioegeshwa mtaimbo, kwa lengo la kutaka kufanya nae mapenzi.

Alisema tukio hilo lilimshitua kutoka usingizini bibi huyo na kumuuliza mjuu wake aliyekua amelala nae nini kilichojiri, lakini kabla ya jibu ghafla kijana huyo alitokea na kumkamata bibi huyo na kumtoa nje kwa kumburura.

Mjukuu wa bibi huyo kwa upande wake alilazimika kutoa msaada lakini alishindwa baada ya kijana huyo kumzidi nguvu kwa kumpiga hadi kuanguka chini hali iliyosababisha kupoteza fahamu.

Hata hivyo baada ya kupata fahamu zake, mtoto huyo alikimbilia kwenye makaazi ya watu umbali wa mita 25 kutoka nyumbani kwao na kuomba msaada kutoka kwa majirani.

Majirani hao walipofika katika nyumba ya bibi huyo walimkuta kijana huyo kwenye mti akimwingilia kinguvu lakini alishindwa kumalizia matamanio yake kwa kukimbia baada ya kuona watu.

Hata hivyo jitihada zake za kukimbia ziliishia ukingoni, kwani watu hao walifanikiwa kumtia mikononi na kuanza kumpiga mithili ya pweza na kumsababishia majeraha makubwa.

Kuhusu kijana huyo, Kamanda Mkadam alisema kuwa wiki ijayo wanatarajia kumfikisha mahakamani kujibu shitaka hilo.

Hata hivyo, alisema kwa hali yake sio nzuri , wataiomba mahakama ihamie kwa muda hospitalini hapo kwa ajili ya kumsomea mashitaka akiwa kitandani.

Kijana huyo anakabiliwa na shitaka kama hilo la ubakaji mbele ya hakimu Makame Khamis Ali wa mahakama ya mkoa Vuga, ambalo kesho linatarajiwa kufikishwa tena mahakamani.

1 comment:

  1. aende jela huyo 20 yrs ili iwe fundisho kwa wengine... hana adabu..

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.