Habari za Punde

Ukata wakwamisha ujenzi barabara za Gando, Konde

Na Haji Nassor, Pemba
WANANCHI wa Gando na Konde Mkoa wa Kaskazini Pemba, wametandwa na hofu ya kutofaidika na barabara za lami, baada ya kuwepo taarifa kwamba kampuni ya MECCO inayojenga barabara hizo imehama.

Wananchi hao walisema kwa muda mrefu sasa hawaoni harakati za ujenzi wa barabara zao, ambao umefikia pahala pazuri.

Walisema wana hofu kubwa kwamba huenda kampuni hiyo imeshaondoka na vifaa vyao, licha kwamba barabara hizo hadi sasa hazijakamilika kwa kiwango cha lami.

Walisema wakati wakiwa na hofu hiyo, bado wapo baadhi ya wananchi hawajalipwa fedha zao za fidia, kutokana na kukatwa kwa miti yao wakati wa matayarisho ya ujenzi barabara hizo.

Mmoja kati ya wananchi hao, Ali Mohamed Ali alisema kwa sasa barabara hiyo iko katika hatari ya kuharibika kutokana na kusita ujenzi wake.

Nae Mjaka Ali Othman alisema tokea kuanza kwa ujenzi wa barabara hiyo mwaka 2009 walibaini kuwa kampuni hiyo haina uwezo wa kufanya kazi hiyo kutokana na kusuasua hata kwenye malipo ya wafanyakazi wake.

Mwakilishi kutoka Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Pemba anaeangalia ujenzi wa barabara hizo, Juma Othman alikiri kwamba kwa sasa ujenzi wa barabara hizo umesita.

Lakini alikanusha kwamba kampuni hiyo imeshahama na vifaa vyake badala yake ujenzi umesimama kutokana na uhaba wa fedha.

Alisema kampuni ya MECCO iliyoanza ujenzi wake Septemba 1, mwaka 2009 ilitakiwa kukamilisha ujenzi wa barabara hizo kwa kiwango cha lami Januari 1, 2012.

Alisema kutokana na kujitokeza mambo kadhaa, baadae kampuni hiyo iliomba kuongezewa miezi nane zaidi na kuahidi kumaliza ujenzi huo Agosti 27, 2012.

Alisema baada ya muda huo kumaliza, kampuni hiyo iliomba kuongezewa tena muda na kutakiwa kukamilisha ujenzi wa barabara hizo ifikapo Oktoba mwaka huu.

Hata hivyo, alisema kutokana na kusimama kwa ujenzi huo anaamini mwezi Oktoba mwaka huu 2013, unaweza kufika na kupita bila ya barabara hizo kukamilika.

“Hivi nazungumza na wewe ujenzi umesimama, hivyo hakuna sababu ya mwezi Oktoba mwaka huu kumaliza ingawa imefikia asilimia 80 ya ujenzi,” alisema.

Kwa upande wake Afisa Mdhamini wa Wizara hiyo, Hamad Ahmed Baucha alikiri kusimama kwa ujenzi huo akisema sababu kubwa ni ukosefu wa fedha.

Alisema ujenzi wa barabara za Gando -Wete na Wete-Konde unafadhiliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Mfuko wa Maendeleo wa Saudi Arabia.

‘’Ni kweli ujenzi wa barabara hizo umesimama, lakini ilitokana na washirika wetu wa maendeleo, kuchelewa kidogo kuingiza fedha na sasa taratibu zinakamilishwa ili kuendelea na ujenzi,’’ alisema.

Kuhusu fidia, alisema hakuna hata nyumba moja iliyovunjwa wakati wa ujenzi ambayo mmiliki wake hajalipwa fidia.

Alisema fidia ambayo haijalipwa ni kwa zile nyumba zilizoharibika wakati wa ujenzi na miti iliyokatwa kupisha utanuzi wa barabara.

Aidha amewataka wananchi wa maeneo mbali mbali kuendelea kuwa wastahamilivu na kamwe Serikali haijawasahau.



1 comment:

  1. Hawwa wana nchi wa konde niwakati muafaka wa kuiazibu,Cuf wao ndio wenye wizara hiyo ya miundo mbinu,malim aseme na waziri wake,au ndio ulifi kenda mbele,

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.