Habari za Punde

Mtanzania kuongoza Jeshi la Kulinda Amani DARFUR

Lt. Jenerali  Paul Ignace Mella,Mkuu Mpya wa Jeshi la Mseto kati ya   Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika maarufu kama UNAMID linalolinda Amani huko   DARFUR  Nchini Sudan. Lt. Jenerali. Mella kutoka  Jeshi la Wananchi wa Tanzania ( JWTZ) anachukua nafasi iliyoachwa na  Lt. Jenerali Patrick Nyamvumba kutoka  Rwanda ambaye amemaliza muda wake Machi 31,2013


Na Mwandishi Maalum

Kwa mara nyingine  Bendera ya  Tanzania imeendelea kupepea katika Tasnia ya Ulinzi wa Amani  ya Kimataifa.

 Mapema wiki hii,  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Bi. Nkosizana Dlamin Zuma wametangaza uteuzi wa Luteni General Paul Ignace Mella  Kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania ( JWTZ) kuwa Mkuu  Mpya wa Jeshi la   Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa huko Darfur ( UNAMID)

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  Ban Ki Moon, na nakala yake kutumwa  katika  Uwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  imeeleza kwamba,  Lt. Gen. Mella anachukua  nafasi iliyoachwa na Mkuu wa  zamani wa Jeshi  hilo (UNAMID), Lt. Gen Patrick Nyamvumba kutoka Rwanda ambaye amemaliza muda wake wa  utumishi  March 31,2013.

Wasifu wa Luteni General Paul Ignace Mella unaelezwa  kuwa ni  Mwanajeshi wa muda mrefu na  mwenye uzoefu na utumishi uliotukuka katika JWTZ akiwa amewahi kushika nyadhifa  mbali mbali  muhimu za uongozi.

Baadhi ya nyadhifa hizo ni pamoja na  Naibu Kamanda Kikosi cha Tanzania chini ya Umoja wa Mataifa huko Liberia (  1993-95), Kamanda wa Kikosi cha  JWTZ, Afisa Mnadhimu-Makao Makuu  ya Jeshi, Mwambata Jeshi-Ubalozi wa Tanzania Uganda na hadi sasa alikuwa ni  Mkuu wa Usalama na Utambuzi- JWTZ.

 Uteuzi wa Lt. Generali Mella unafuatia mchakato mrefu ulioshindanisha wateuliwa kutoka nchi mbalimbali duniani, na hatimaye  yeyé akaibuka mshindi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.