Na Miza Othman-Maelezo Zanzibar 5/6/2013
Tatizo la uchafuzi wa Mazingira katika Visiwa vya Zanzibar limeathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya Kilimo na Uvuvi na kwamba juhudi za pamoja zinahitajika kuinusuru Zanzibar ili kukabiliana na hali hiyo.
Hayo yameelezwa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa kwanza wa Rais Fatma Abdulhabib Fereji wakati alipokuwa akizungumza na Wananchi na Wanafunzi kutoka maeneo mbali mbali ya Zanzibar huko Victoria Garden Mjini Unguja katika maadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani.
Amesema hali hiyo imetokana na Wananchi kuchafua mazingira kwa kukata Mikoko,kuchimba mchanga pembezoni mwa fukwe hali ambayo imeifanya bahari kupanda juu kwenya mashamba ya wakulima na kuhatarisha kilimo.
Ameongeza kuwa Wakulima wa Mwani wamekuwa wakikosa mavuno mazuri kutokana na kupanda kwa joto la bahari nakupelekea mwani wao kufa ambapo kwa upande wa Wavuvi hulazimika kwenda maeneo ya mbali kuvua kwavile mazalia ya samaki nayo hufa kutokana na joto la bahari kuwa kubwa.
“Tuna shuhudia kuanguka kwamiti ya kudumu na majengo mbali mbali kutokana na mmong’onyoko wa fukwe, kupotea maeneo ya kilimo kutokana na kuingiliwa na maji ya bahari, na hata kuathirika maji ya kunywa katika visima nayo yanaathiriwa na maji ya chumvi”, alisema Waziri Fereji.
Alisema hali hiyo hivi sasa haiwezi kuachwa iendelee kama ilivyo, bali Serikali na wananchi waipinge kwa nguvu zote ili kuepuka maafa hayo.
Alisema juhudi kubwa inayofanywa na Serikali ni kuihamasisha na kuielemisha jamii juu ya umuhimu wa kuifadhi mazingira na kuwataka wananchi washiriki katika matukio mbalimbali ikiwemo Midahalo na mashindano ya kuhifadhi mazingira.
“Hali ya mazingira yetu ilivyo hivi sasa hatuwezi kuiacha ikaendelea kama ilivyo,hivyo juhudi za pamoja za hali na mali zina hitajika kuazia ngazi ya Dunia Taifa,Wilaya ,Shehia hadi mwananchi mmoja mmoja kuinusuru Dunia pamoja na nchi zetu kutokana na hali mbaya ya mazingira tulio nayo”, aliongeza kuseama Waziri.
Nae Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira Zanzibar Hamza Rijal amesema sababu iliyopelekea uharibifu wa mazingira ni kuwepo kwa matumizi mabaya ya viwanda Vidogo vidogo, ambapo amesema kuwa kuwepo kwa Sheria ya Mazingira inayokidhi haja ya wakati uliopo inaweza kupunguza tatizo.
Madhimisho hayo yaliambatana utoaji wa zawadi wa pesa taslimu kwa wanafunzi walifanya vyema katika kuandaa utenzi , mchezo wa kuigiza na ngoma za asili ambapo Ujumbe wa mwaka huu ni Fikiria .kula .Weka .
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment