Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Imeelezwa kuwa Zanzibar inaweza kukumbwa na Janga la ubaba wa Maji ifikapo mwaka 2015 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo watu kuharibu Vyanzo vya Maji.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohammed Aboud ameeleza hayo alipokuwa akizindua Kongamano la Kitaifa la kukabiliana na Maafa lililofanyika Jambiani Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema kuna Tafiti zimefanywa na kuonesha hatari inayoikabili Zanzibar katika upatikanaji wa Maji na kwamba juhudi binafsi zinahitajika ili kukabiliana na hali hiyo.
Aboud amesema Wasomi na Wataalam kwa ujumla wanapaswa kufahamu hali hiyo na kuisaidia Serikali katika kukabiliana na Upungufu huo badala ya kukaa kimya na kulaumu.
“Wasomi wamekaa kimya sana hawatoi ushauri wa kitaalamu kwa Serikali juu ya nini kifanyike ili kuijengea uwezo Serikali na Jamii kwa ujumla kukabiliana na Majanga ” Alifafanua Aboud
Ametolea Mfano wa Zao la Nazi linavyoendelea kupotea katika Visiwa vya Zanzibar na kusema kuwa Wataalamu wameshindwa kuja na namna bora ya kupata Minazi bora inayozalisha zaidi na kuchukua eneo dogo kuliko Minazi iliyopo.
Aidha Waziri Aboud amesisitiza Idara ya Maafa kwa kushirikiana na wadau wengine kuendelea kutoa Elimu ya kukabilaiana na Majanga kwa jamii ili kupata jamii salama.
“Ndugu wadau Elimu ni Muhimu kwa wananchi kuanzia ngazi ya chini hadi juu,kwa kukosekana Elimu ya Majanga baadhi ya wakati hata Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanakuwa wagumu kupitisha Vifungu vya Bajeti za Idara,yote ni kiashirio cha uelewa mdogo juu ya Majanga” Aliongezea Aboud.
Awali akimkaribisha Waziri Aboud, Mkurugenzi wa Idara ya Maafa alisema licha ya kukabiliwa na Changamoto mbalimbali Idara yake imejipanga vyema kuhakikisha inafanya majukumu yake ya msingi ikiwemo kukabiliana na Maafa.
Amesema kwa Sasa Idara ya Maafa ina mpango wa kuainisha maeneo hatarishi katika Ramani ili kusaidia ufahamu na namna ya kuweza kukabiliana na maafa pale yanapotokea.
Kongamano hilo la kitaifa la kukabiliana na maafa limendaliwa na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar ambapo kwa siku mbili Washiriki kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi watajadili na namna bora ya kukabiliana na Majanga Zanzibar
No comments:
Post a Comment