Habari za Punde

Maalim Seif : Chagueni viongozi wenye dhamira ya iutetea maslahi ya wananchi

  Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad, akimtambulisha  mgombea udiwani kata ya Elerai Mkoani Arusha kupitia chama hicho, John Gilbert Bayo ambaye alitimuliwa nafasi hiyo akitokea Chadema.
 Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na wananchi wa kata ya Elerai mkoani Arusha katika mkutano wa kampeni za udiwani na  kumnadi mgombea wake John Gilbert Bayo.
 Baadhi ya wananchi wa kata ya Elerai mkoani Arusha wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad, wakati akimnadi mgombea udiwani kupitia chama hicho, John Gilbert Bayo.
 Mjumbe wa Baraza Kuu la uongozi CUF kutoka mkoani Arusha, Flora Emmanuel,  akizungumza na wananchi wa kata ya Elerai mkoani Arusha katika mkutano wa kampeni za udiwani ambapo Maalim Seif alikuwa mgeni rasmi.
 Aliyekuwa diwani wa CHADEMA kata ya Elerai Mkoani Arusha John Gilbert Bayo, akinadi sera zake kuomba achaguliwe tena nafasi hiyo kupitia CUF, baada ya kutimuliwa na CHADEMA
Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF Abdul Kambaya  akizungumza na wananchi wa kata ya Elerai Arusha, wakati akimnadi mgombea udiwani kupitia chama hicho, John Gilbert Bayo. (picha na Salmin Said, OMKR)

Na Hassan Hamad, Arusha
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad, amewashauri wananchi wa Arusha kuchagua viongozi waliodhamiria kutetea maslahi ya wananchi badala ya wale wanaoweka mbele maslahi binafsi.
 
Amesema chama hicho kimejijengea sifa kubwa kitaifa na kimataifa kutokana na sera zake za kuendeleza amani na kujali maslahi ya wananchi, hivyo kuwaomba kukiunga mkono ili kiweze kutimiza malengo yake ya kuwakomboa watanzania.
 
Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameeleza hayo katika mkutano wa kampeni wa kumnadi mgombea udiwani kata ya Elerai Mkoani Arusha, John Gilbert Bayo.
 
Amesema Bayo ambaye alikuwa diwani wa kata hiyo kupitia CHADEMA, ni kiongozi imara, mwenye hekma na busara katika kuwatumikia wananchi, na kuwataka kumchagua ili aweze kutekeleza matakwa yao.


Amefahamisha kuwa wananchi wa kata ya Elerai wanakabiliwa na changamoto moto mbali mbali zikiwemo upungufu wa madarasa ya kusomea, kituo cha afya na miundombinu ya maji na barabara, na kuwaomba kumchagua kiongozi huyo mwenye uzoefu ili asaidie kutatua matatizo hayo.
 
Akizungumzia kuhusu mafanikio ya Serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar, Maalim Seif amesema imerejesha hali ya amani na utulivu, sambamba na kuwakomboa wakulima wa zao la karafuu ambao waliongezewa bei ya zao hilo kutoka shilingi 3000 hadi 15,000 kwa kilo moja.
 
Ameongeza kuwa sera za serikali ya Zanzibar ni kuhakikisha kuwa wakulima wa karafuu wanapata asilimia 80 ya bei ya zao hilo katika soko la dunia, hali inayowahamasisha wakulima kuongeza juhudi na uzalishaji wa zao hilo.
 
Kwa upande wake mgombea udiwani wa kata ya Elerai John Bayo, amesema ameamua kugombea nafasi hiyo kupitia CUF baada ya kutimuliwa CHADEMA, ili aweze kutimiza ahadi zake alizozitoa kwa wananchi wa kata hiyo mwaka 2010.
 
Ameelezea matumaini yake kuwa wananchi wa kata hiyo bado wana imani naye, lakini chama chake cha awali kiliamua kumdhalilisha kwa kumvua uanachama baada ya kuhoji masuala muhimu yenye maslahi na wananchi.
 
Amefahamisha kuwa baada ya kuhoji mambo hayo, chama kiliamua kuwafukuza madiwani kadhaa bila ya kuwashirikisha wananchi waliowachagua, jambo ambalo amesema ni kinyume na utaratibu, baada ya viongozi hao kuangalia zaidi maslahi binafsi.
 
Amesema tangu kufukuzwa uanachama na udiwani, miradi mingi ya maendeleo  katika kata hiyo ikiwemo miradi ya maji na zahanati imekwama, na kuahidi kuiendeleza iwapo wananchi watamchagua tena kushika nafasi hiyo.
 
Katika hali isiyokuwa ya kawaida baadhi ya viongozi wa vyama vya TLP na CHADEMA  mkoani Arusha, wameamua kumpigia kampeni mgombea huyo wa CUF ili aendelee kuwatumikia wakaazi wa Elerai.
 
Mwahija Choga ambaye ni katibu wa TLP mkoani Arusha, amesema Bayo na wenzake walitimuliwa CHADEMA kinyume na utaratibu, na kuwasisitiza wakaazi wa Elerai kuacha kuwapigia kura viongozi kwa kufuata ushabiki wa vyama, bali wazingatie viongozi watendaji.
 
“Mimi naona viongozi wa CHADEMA wanachezea akili za watanzania, wanawake na vijana wa nchi hii. Tafadhalini wakaazi wa Elerai musikubali kudanganywa, acheni kupiga kura kwa ushabiki wa chama, musibabaishwe na helikopta inayokuja kuwarushia vumbi, chagueni kiongozi mtendaji ambaye kwa kata hii ni John Bayo”, alitanabahisha Choga.
 
Nae Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF Taifa, Abdul Kambaya, amesema vijana ndio waathirika wakubwa wa hali ya maisha, na kuwataka kufanya maamuzi sahihi katika kuchagua viongozi watakaojali maslahi ya wananchi.
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.