Aahidi kurejesha umoja ZFA, BTMZ
Na Salum Vuai, Maelezo
MGOMBEA wa nafasi ya urais wa Chama cha Soka Zanzibar Ravia Idarous Faina, jana ameanza kampeni zake katika wilaya zote kisiwani Pemba, huku akiahidi kuweka uwiano na uhusiano mwema kati ya chama hicho na taasisi nyengine.
Akizungumza kwa nyakati tafauti na wapiga kura wa wilaya za Pemba, Ravia alisema, kama kweli wanataka mabadiliko, wampigie kura nyingi zitakazomuwezesha kushika nafasi hiyo.
Ravia aliahidi kuzika tafauti kwa kuondoa mgawanyiko wa kimaeneo kati ya Unguja na Pemba, na kujenga ZFA moja itakayokuwa imara na yenye dhamira ya kweli kuleta maendeleo ya soka nchini.
Chanzo chetu cha habari kutoka Pemba, kimeliambia gazeti hili kuwa, mgombea huyo amesema anaumwa sana na kuwepo kwa kambi mbili za ZFA zinazopingana Unguja, na nyengine zilizojigawa kati ya Pemba na Unguja, na kusema hali hiyo ndiyo inayosababisha migogoro isiyokwisha ambayo inarudisha nyuma soka la Zanzibar.
Ravia ameahidi kuzifanyia mambo mazuri wilaya zote Unguja na Pemba ingawa hakuwa tayari kuyaweka hadharani.
Aidha amewaambia wapiga kura hao, kwa miaka saba aliyoishi ndai ya ZFA, nafahamu kila kitu, na pia kuwepo kwa tafauti kati ya uongozi wa juu wa chama hicho na Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ), akisema akipewa ridhaa, hali hiyo itaondoka kwa manufaa ya soka la nchi hii.
“Mbali na hayo, pia nitaimarisha mahusiano na ushirikiano kati yetu na wenzetu wa TFF, CECAFA na CAF, ili kuijengea Zanzibar heshima na hadhi katika medani ya mpira wa miguu.
Mgombea mwengine anayetoka ndani ya kamati tendaji ya ZFA Unguja Abdallah Juma Mohammed, alipoulizwa juu ya mipango yake alisema anafanya kampeni zake kimya kimya bila ya vishindo.
Uchaguzi mdogo wa Rais wa ZFA unatarajiwa kufanyika Juni 8, mwaka huu katika hoteli ya Zanzibar Ocean View, kufuatia kujuzulu kwa Amani Ibrahim Makungu mwishoni mwa mwezi Januari 2013.
No comments:
Post a Comment