Habari za Punde

SUZA yatakiwa kuandaa vijana kumudu soko la EAC

Na Juma Khamis
SKULI ya Elimu Endelezi na Utaalamu ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SCOPE) imekutana na wadau wa taasisi mbali mbali wenye maamuzi, kujadiliana na kutangaza mafunzo mbali mbali yanayotolewa na skuli hiyo.

Akifungua mkutano huo wa majadiliano uliofanyika hoteli ya Zanzibar Ocean View, Naibu Makamu Mkuu wa SUZA (utawala), Dk. Zakia Abubakar, alisema chuo kimejidhatiti kutoa elimu bora itakayokidhi mahitaji ya wananchi na kutoa elimu yenye ubora inayohitajika katika soko la ajira.

Nae Makamu Mkuu wa SUZA (taaluma), Dk. Haji Mwevura, alisema lengo la SUZA ni kuhakikisha kinakuwa chaguo la kwanza katika masuala ya taaluma na utafiti katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Aidha alisema chuo kitaendelea kutoa elimu bora inayolingana na mazingira sambamba na kuisaidia jamii kuzikabili changamoto za karne ya 21 na kwamba azma hiyo itafikiwa ikiwa wadau watashirikiana na chuo hicho.

Kwa upande wake Mkuu wa SCOPE, Gharib Mohammed Hamza, aliwambia wadau hao kwamba skuli hiyo imeanzisha mafunzo mbali mbali, hivyo akawanasihi wawaruhusu wafanyakazi wao kujiunga na mafunzo hayo.

Alisema pamoja na mambo mengine, mafunzo hayo yatasaidia kumaliza changamoto katika sehemu za ajira na kuongeza ushirikiano.

Wakichangia mjadala huo, wadau walisema muda umefika sasa kwa SCOPE kufikiria kuanzisha mafunzo ya walimu wa maandalizi kwa kuwa hakuna chuo kinachotoa mafunzo hayo nchini.

Mkurugenzi Utumishi, Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya wanawake na Watoto, Iddi Ramadhan Mapuri, alisema kwa kuwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto vinaendelea na kwa kuwa serikali inatumia fedha nyingi kusomesha watendaji wake katika maeneo hayo nje ya Zanzibar, hakunabudi kwa SCOPE kuanzisha mafunzo ya jinsia na hifadhi ya mtoto.

Aidha aliishauri skuli hiyo kuanzisha mafunzo ya hifadhi ya jamii kwa kuwa tayari serikali imeshaanzisha sera ya hifadhi ya jamii pamoja na shahada ya kwanza katika kada hiyo.

Wadau wengine walikishauri chuo hicho kuanzisha mafunzo katika kada za tiba ya mimea na wanyama kwa kuwa wananchi wengi wanategemea maeneo hayo katika shughuli zao za maisha.

Pia walishauri yawepo mafunzo katika maendeleo ya mikoa katika kipindi hichi ambacho tayari serikali imepitisha sera ya madaraka mikoani ili kupunguza upungufu wa watendaji katika eneo hilo.

Hata hivyo, baadhi ya wachangiaji walishauri vyuo vidogo viachiwe vitoe mafunzo ya muda mfupi badala ya mafunzo hayo kufundishwa SUZA pekee.

Walisema kwa kuwa SUZA kinaendelea kujitanua, hakunabudi mazingira ya chuo kuboreshwa ikiwemo majengo yanayojengwa kuwafikiria watu wenye ulemavu.

Mkurugenzi wa Idara ya Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, Mohammed Juma, pamoja na kupongeza kazi nzuri iliyofanywa na SUZA lakini alikitahadharisha chuo hicho kisifikirie kujikumbia kila kitu, badala yake kizingatie ubora wa elimu kuliko wingi wa kozi inazofundisha.

Dk. Ahmad Hamad Khatib kutoka Kamisheni ya Utalii, alisema SUZA inapaswa kufundisha vijana watakaohodhi ajira chache zilizopo zisichukuliwe na wageni na baadae kushambulia ajira zilizopo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.