Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akizungumza na Balozi wa Italia nchini Tanzania Pierluigi Velardi,aliyefika kumuaga Rais Ikulu Mjini Zanzibar, baada ya kumaliza muda wake wa kazi Nchini
[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]
Na Said Ameir, Ikulu
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema uwekezaji mkubwa uliofanywa na makampuni kutoka Italia katika sekta ya Utalii nchini ni moja ya matunda ya uhusiano mzuri uliopo kati ya Zanzibar na Italia.
Akizungumza na Balozi wa Italia Pierluigi Velardi ambaye alifika Ikulu kumuanga baada ya kumaliza muda wa kuitumikia nchi yake nchini Dk. Shein amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inathamini sana mchango wa wawekezaji toka nchi hiyo katika uchumi wa Zanzibar.
“mchango wa wawekezaji kutoka Italia katika uchumi wa Zanzibar hasa kwenye sekta ya Utalii ni mkubwa na umewafanya wananchi wa nchi mbili hizi kuwa karibu”Dk. Shein alieleza.
Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa sekta ya utalii nchini imekua na imo katika kiwango kizuri ingawa zipo changamoto za hapa na pale ambazo Serikali, kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali, imejidhatiti kuzitafutia ufumbuzi.
Alisema uhusiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Italia ni wa miaka mingi na umekuwa ukiimarika siku hadi siku na kueleza matumaini yake kuwa wawekezaji zaidi kutoka nchi hiyo watakuja kuwekeza nchini.
Dk. Shein aliishukuru Serikali ya Italia kwa misaada yake ikiwemo katika sekta ya afya na kubainisha kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ingependa kuona ushirikiano zaidi katika kuendeleza na kuimarisha Maabara ya Afya ya Jamii iliyopo Wawi Chake Chake Pemba.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alimtakia Balozi Pierluigi safari njema ya kurejea nyumbani pamoja na kumtakia kila la heri katika majukumu yake mapya.
Kwa upande wake Balozi Pierluigi Velardi alimhakikishia Rais kuwa atakuwa Balozi Mzuri wa Zanzibar wakati wote akiwa nchini Italia na kumhakikishia kuwa watalia wengi wanaipenda Zanzibar.
“wananchi wa Itatia wanaipenda sana Zanzibar na imeonyesha hivyo hata wakati wa kipindi kigumu cha uchumi wataliana wengi wajibana na kutembelea Zanzibar”alieleza balozi Pierluigi.
Alisema ataitangaza Zanzibar na Tanzania kwa wawekezaji wa Italia na kuwaeleza fursa na mazingira ya uwekezaji na kuonyesha mtumaini makubwa hali ikiwa nzuri wawekezaji wengi toka nchini humo watendelea kuja Zanzibar na Tanzania kwa jumla.
Balozi huyo aliishukuru Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumpa ushirikiano wakati wote alipokuwa akitekeleza majukumu yake ya kuiwakilisha nchi yake humu nchini.
Wahusika wa Protocol wamkumbushe Mheshimiwa Rais anaposalimiana na wageni awe anawaface kuwe na face to face contact.
ReplyDelete