Habari za Punde

Dk Shein aongoza Mazishi ya wanajeshi leo


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein,(katikati) akijumuika na Vingozi na Waislamu wengine katika Hitma ya wanajeshi waliouwawa kwa kupigwa risasi Jimbo la Daafur nchini Sudan hivi karibuni,Merehemu Sgt Shaibu Shehe Othman, na Cpl Mohammed Juma Ally iliyosomwa katika msikiti Masjid Nuru Muhammad,Mombasa Mjini Unguja leo

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein,(wa tatu kulia) akijumuika na Vingozi na Waislamu wengine katika kuwaswalia Merehemu Sgt Shaibu Shehe Othman,na Cpl Mohammed Juma Ally ,mbele katika msikiti Masjid Nuru Muhammad,Mombasa Mjini Unguja leo,wanajeshi waliouwawa kwa kupigwa risasi Jimbo la Daafur nchini Sudan hivi karibuni

Wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania wakibeba Jeneza la mwili wa Marehemu Sgt Shaibu Shehe Othman,baada ya kuwasilim katika makaburi ya Mwanakwerekwe mjini Zanzibar jana,akiwa ni miongoni mwa wanajeshi 7 waliouwawa kwa kupigwa risasi Jimbo la Daafur nchini Sudan hivi karibuni

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein,(wa pili kushoto) na viongozi wengine walihudhuria katika mazishi ya Marehemu Sgt Shaibu Shehe Othman, katika makaburi ya Mwanakwerekwe mjini Zanzibar jana,akiwa ni miongoni mwa wanajeshi 7 waliouwawa kwa kupigwa risasi Jimbo la Daafur nchini Sudan hivi karibuni

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein,akitia udungo katika Kaburi la Marehemu Sgt Shaibu Shehe Othman,aliyezikwa leo Mwanakwerekwe Mjini Unguja, akiwa ni miongoni mwa wanajeshi wa jeshi la Ulinzi la Tanzania 7 waliouwawa hivi karibuni Nchini Sudan Jimbo la Daafur

Baadhi ya Wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Tanzania na Ndugu na Jamaa wa marehemu Sgt Shaibu Shehe Othman, na Cpl Mohammed Juma Ally ,waliofurika katika viwanja vya makaburi ya Mwanakwerekwe,ambapo ndipo walipozikwa leo,mchana

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein,(katikati) na Vingozi na Waislamu,wakiangalia Wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Tanzania,walipokuwa wakitoa hesha ya mwisho kwa marehemu Sgt Shaibu Shehe Othman,wakati wa mazishi yake katika makaburi ya Mwanakwerekwe leo. [Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]

Na Rajab Mkasaba, Ikulu
 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo umeungana na viongozi mbali mbali wakiwemo wa vikosi vya ulizi na usalama wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na wafiwa na wananchi katika mazishi ya wanajeshi wa Zanzibar waliouwawa huko Darfur Jumaamosi ya Julai 13 mwaka huu.
 
Majira ya saa nne za asubuhi Dk. Shein akiwa pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad walishiriki katika duwa ya Hitma iliyosomwa kwa ajili ya maiti zote mbili pamoja na kuwasalia maiti hao huko katika masjid Noor Mohammad (S.A.W), Mombasa kwa Mchina, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
 
Wananchi, wafiwa pamoja na viongozi mbali mbali wa vyama na serikali walihudhuria katika Hitma hiyo ambapo mapema Dk. Shein alitia saini vitabu vya maombolezi kwa ajili ya marehemu hao huko katika eneo hilo la masjid Noor Mohammad (S.A.W).
 
Baada ya kumaliza dua na sala hiyo ya maiti Dk. Shein, aliongozana na viongozi wengine na wananchi walielekea katika Makaburi ya Mwanakwerekwe kwa ajili ya mazishi ya marehemu hao.
 
Katika makaburi ya Mwanakwerekwe mamia ya wananchi walikuwa tayari wameshajipanga kwa ajili ya kuwaaga narehemu hao ambao wote wamezikwa katika eneo hilo maarufu la makaruni liliopo Wilaya ya Magharibi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
 
 
 
Mbali ya wananchi hao waliokuwa wameshafika na kujipanga katika eneo hilo la makaburi nao wanajeshi wa kikosi cha Ulinzi cha JWTZ walikuwa wameshajipanga vyema kwa ajili ya kuwaagaa wenzao kwa mila, desturi na taratibu zote za Kijeshi kama ilivyo desturi.
 
Katika eneo hilo la Makaburi la Mwanakwerekwe, Dk. Shein aliungana na viongozi mbali mbali wa vyama na Serikali akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Shamsi Vuai Nahodha, wakuu wa vikosi vya ulinzi na usalama vya SMT na SMZ na wananchi pamoja na wafiwa.
 
Taratibu za mazishi zilianza katika eneo hilo ambalo makaburi mawili yaliokuwa yamechimbwa karibu karibu, mwili wa marehemu Sajenti Shaib Shehe Othman ulianza kuzikwa  kwa kuanza na taratibu zote za kijeshi na baadae kufuata taratibu za kuzika za kidini.
 
Mara baada ya kuzikwa kwa mwili wa Marehemu  Sajenti Shaib Shehe Othman, mwili wa marehemu Koplo Mohammed Juma Ali ulizikwa pembezoni mwa kaburi hilo na kufuata taratibu zote za kijenshi na baadae taratibu za kidini.
 
Baada ya hatua hiyo ya mazishi salamu za Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Mrisho Kikwete zilitolewa ambapo salamu hizo zilitoa pole kwa wafiwa na wanafamilia wa marehemu na kuwaombea kwa MwenyeziMungu aziweke roho za marehemu mahala pema peponi.
 
Aidha, salamu hizo zilieleza kuwa msiba huo ni wa Taifa zima na si kwa upande wa Tanzania pekee bali ni Afrika na dunia nzima kwa ujumla.
 
Nao wanafamilia na wazazi wa marehemu hao, walitoa shukurani zao za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa juhudi kubwa ilizozichukua katika kuhakikisha marehemu hao wanafika katika maeneo yao ya kuzikwa kwa kufanikisha taratibu zote za usafiri kwa ufanisi mkubwa.
 
Sambamba na hayo, wazazi na wanafamilia hao waliendelea kutoa shukurani zao za dhati kwa Serikali zote mbili kwa kuweza kupata taarifa kwa kila hatua iliyokuwa ikichukuliwa katika mchakato wote wa usafiri wa watoto wao hao tokea huko Sudan hadi kuwasili Tanzania na hatimae leo kuzikwa hapa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.