Habari za Punde

Jaji ajiondoa kesi ya mauaji ya Padri Mushi


Na Khamis Amani
JAJI Mkusa Isaac Sepetu wa mahakama kuu Zanzibar anaesikiliza kesi ya mauaji ya Padri Evaristus amejitoa kusikiliza kesi hiyo.

Jaji Mkusa amejitoa kufuatia maombi yaliyowasilishwa na mshitakiwa wa kesi hiyo Omar Mussa Makame kwa kutokua na imani nae.

Mshitakiwa huyo kupitia Wakili wake, Abdallah Juma aliwasilisha ombi hilo katika kikao kilichopita ya kwamba hana imani na Jaji Mkusa kwa kuhofia kutomtendea haki katika kesi hiyo, kwa madai tayari ameshawahi kusikiliza maombi kadhaa ya kesi hiyo yaliyowasilishwa mbele yake na kuyatolea maamuzi.

Maamuzi hayo ambayo Jaji Mkusa aliyatoa kwa mujibu wa taratibu za kisheria za mwendo wa jinai, upande wa utetezi haukuridhika nayo na kuhofia kutotendewa haki katika kesi hiyo ya msingi na kuwasilisha ombi mahakamani la kumkataa Jaji huyo.

Akitoa maelezo ya kujitoa,Jaji Mkusa alisema ijapokuwa upande wa utetezi umewasilisha maombi hayo juu yake, lakini maombi hayo hayakuzingatia sababu za msingi za kumkataa kwa mujibu wa kumbu kumbu za kesi mbali mbali alizozielezea mahakamani hapo zilizowahi kutolewa maamuzi na mahakama ya rufaa Tanzania pamoja na mahakama ya Kenya.

Alisema, ombi hilo la upande wa utetezi la kukataa na kuchagua Jaji wa kusikiliza linakuja kwa maslahi na matakwa binafsi kwa kuona Jaji huyo hawezi kuburuzwa na anasimamia haki kwa pande zote mbili ili kuona zinatendeka na sio kwa maslahi ya mtu mmoja.

Hata hivyo, kutokana na maelezo mbali mbali aliyoyatoa katika maamuzi hayo, Jaji Mkusa alisema ili asionekane king'ang'anizi wa kusikiliza kesi hiyo ameamua kujitoa na kulirudisha jalada la kesi hiyo kwa Jaji Mkuu ili aweze kumpangia Jaji wa kuisikiliza.

Pamoja na kujitoa huko, Jaji Mkusa alifahamisha kwamba amechukua uamuzi huo si kwa kuuridhisha upande mmoja bali ni kuona haki ikitendeka kwa pande zote.

Baada ya uamuzi huo Jaji Mkusa aliiahirisha kesi hiyo hadi Agosti mosi mwaka huu kwa kutajwa na mshitakiwa amerudishwa rumande kutokana na shitaka linalomkabili ni miongoni mwa makosa yasiyokuwa na dhamana chini.

Upande wa mashitaka katika kikao hicho uliongozwa na Mwanasheria wa serikali Abdallah Issa Mgongo kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

Katika kesi hiyo Omar Mussa Makame, alishitakiwa kwa mauaji ya Padri Evaristus Mushi kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya kanuni ya adhabu sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.

Tukio hilo lilidaiwa kutokea Februari 17 mwaka huu huko Beit el Ras wilaya ya Magharibi Unguja majira ya asubuhi wakati Padri huyo alipokuwa akiwasili katika ibada ya Jumapili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.