Habari za Punde

Mganda, Msudan watua Simba

Na Mwandishi Wetu
KLABU ya Simba SC, imezidi kujiimarisha baada ya jana wachezaji wawili wa kimataifa kutoka Uganda na Sudan Kusini, kuwasili nchini kwa ajili ya majaribio.Kutoka Uganda, ni beki Assumani Buyinza aliyemaliza mkataba wake katika klabu moja nchini Vietnam wanakocheza pia Mtanzania Danny Mrwanda na mshambuliaji Mganda, Moses Oloya ambaye Simba walimtaka sana, lakini akawaambia wasubiri amalize mkataba Oktoba.

Mchezaji mwengine anayetoka Sudan Kusini ni Kon James wa Al Nasir Juba ambayo ilitolewa na Azam FC katika raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema, wachezaji hao wamekuja kufanya majaribio na iwapo watamvutia kocha Abdallah Athumani ‘King Kibadeni’, watasajiliwa.

Buyinza ni beki wa kati mwenye uzoefu ambaye, Simba inatumai anaweza kukidhi vigezo vya kocha Kibadeni, wakati Kon ni mshambuliaji mzuri ambaye Simba walijionea wenyewe alipokuja na Al Nasir Juba kucheza na Azam.

Tayari Simba ina wachezaji watatu wa Uganda katika kikosi chake, ambao ni kipa Abbel Dhaira, kiungo Mussa Mudde ambao wanaingia msimu wa pili Msimbazi, pamoja na beki Samuel Ssenkoom ambaye ndio kwanza amesajiliwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.