Habari za Punde

Stars yaipigia kambi Uganda

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imeingia kambini jana katika hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam kujiandaa na mechi dhidi ya Uganda, The Cranes iliyopangwa kuchezwa Julai 13, mwaka huu uwanja wa Taifa.Mechi hiyo ni ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN), zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.

Wachezaji walioteuliwa na kocha Kim Poulsen katika kikosi hicho ni David Luhende. Ally Mustafa, Athumani Iddi, Frank Domayo, Kevin Yondan, Nadir Haroub na Simon Msuva wote kutoka Yanga SC.Wengine ni Aggrey Morris, Aishi Manula, Khamis Mcha, Mudathiri Yahya, John Bocco, Mwadini Ali na Salum Abubakar (Azam).Wanasoka walioitwa kutoka Simba ni Amri Kiemba, Haroun Chanongo, Juma Kaseja, Mwinyi Kazimoto, Mrisho Ngassa na Shomary Kapombe, pamoja na Juma Luizio na Vincent Barnabas (Mtibwa Sugar).

Baada ya mchezo wa kwanza dhidi ya Uganda Cranes, Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itarudiana na Waganda hao wiki mbili baadaye mjini Kampala, Uganda.

Kim anatarajiwa kutumia mechi hizo za kufuzu CHAN kuwapoza machungu Watanzania, baada ya kupoteza nafasi ya kwenda katika fainali za Kombe la Dunia Brazil mwakani, kufuatia kufungwa mabao 4-2 na Ivory Coast katika mchezo wa kundi C mwezi uliopita Dar es Salaam.

Kwa upande mwengine, Makamu Mwenyekiti wa Yanga Clement Sanga, amewaondoa hofu wapenzi wa soka nchini kuhusu wachezaji wa timu yake walioitwa kwenye kikosi cha Stars.

Kulikuwa kuna habari kwamba, Yanga ambayo itaondoka kesho Dar es Salaam kwenda kanda ya Ziwa kwa ziara ya wiki moja, haitaruhusu wachezaji wake kujiunga na kambi ya Stars, lakini juzi Sanga alisema imewapa ruhusa na jana walitajariwa kuripoti katika kambi ya timu hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.