Habari za Punde

Serikali yatoa ruhusa jengo la uwanja wa ndege kuendelea

Na Ali Issa-Maelezo Zanzibar     31/7/2013
 
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa ruhusa ya kuendelea kwa ujenzi wa Jengo jipya la Abiria katika Uwanja wa ndege wa  Zanzibar lililosita kwa muda baada ya kuonekana kasoro za kiufundi zilizojitokeza hapo awali katika jengo hilo.
 
Hayo yameelezwa leo huko Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar na  Waziri wa Miundo mbinu na Mawasiliano Rashid Seif  Suleiman wakati  alipokuwa akiwasilisha Bajeti yake ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo.
 
Amesema katika kutekeleza hilo ujenzi huo umeanza mara baada kukamilika kwa taratibu za Michoro mipya kwa baadhi ya sehemu za jengo baada ya kupata Mshauri elekezi kutoka Nchini Ufaransa.
 
“Mnamo mwezi wa Machi mwaka huu tulimpata mshauri elekezi na kuanza kazi mwezi April na kutoa ripoti yake mwezi juni mwaka huu ambavyo ilionesha namna ya kasoro zilivyojitokeza na kuweza kutatuliwa haraka ipasavyo .”alisema Waziri Rashid Seif.
 
Aidha alifahamisha kuwa baada ya matokeo ya Ripoti hiyo mpya ya michoro Serikali ilifuatilia suala hilo kwa kuwasiliana na Benk ya Exim ya China na kuwasilisha ombi la kuongezewa muda wa mkopo ambapo ungefikia ukingoni tarehe 31 Julai mwaka huu.
 
Amesema hali hiyo ilifanikiwa pamoja na kuiomba Serikali ya Mapinduzi  pesa za ziada ya mkopo ili kugharamia ongezeko  linalotokana na kubadilika kwa baadhi ya michoro ya jengo hilo na mazingira iliyo lizunguka .
 
Waziri Rashid ameongeza kuwa ujenzi wa Uwanja huo unaendelea chini ya Mkandarasi yule yule wa kampuni ya Beijing Construction Engineering Group ya China chini ya usimamizi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mshauri Muelekezi kutoka kampuni ya ADPI ya Ufaransa.
 
Kwa upande wake Kamati ya Miundonbinu na Mawasiliano imependekeza kufanyiwa Marekebisho Makubwa Barabara zilizochakaa katika maeneo ya Unguja na Pemba.
 
Aidha Wamependekeza Bandari ya Mkoani Pemba kupewa kipaumbele cha pekee kwa kufanyiwa marekebisho ya haraka kutokana eneo lake kudidimia.
 
Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano imeliomba Baraza kuidhinisha jumla ya shl. Bilioni 20.092 ili kuiwezesha Wizara hiyo kutekeleza majukumu yake iliyojipangia kwa mwaka wa Fedha 2013/2014
 
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.