Habari za Punde

Shirika la Utalii Zanzibar lavunjwa.


Khamis Amani na Mwanajuma Mmanga
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imelivunja rasmi Shirika la Utalii la Zanzibar, kutokana na kushindwa kuhimili ushindani mkubwa uliopo katika sekta ya biashara ya utalii nchini.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk aliyaeleza hayo jana ndani ya ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara hiyo kwa mwaka 2013/2014.

Waziri Mbarouk alisema kwa kipindi kirefu sasa hali ya biashara imekuwa sio nzuri katika Shirika hilo ikizingatiwa changamoto kubwa inayolikabili katika kushindana na sekta binafsi.

Alifahamisha kabla ya kuvunjwa, serikali kwa kutumia wataalamu na washauri mbali mbali, ilikuwa ikitafuta ushauri wa kitaalamu juu ya hatma ya Shirika hilo ili kujua kama linaweza kuleta tija kwa Taifa.

Alisema kufuatia ushauri huo, serikali imeamua rasmi kulivunja Shirika hilo na hatua za kutekeleza maamuzi hayo tayari zimeshaanza.

"Mheshimiwa Spika, zoezi la kukamilisha taratibu za kulivunja Shirika tunatarajia kukamilika katika kipindi kifupi kijacho," Waziri Mbarouk aliwaambia Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Kwa upande wa Shirika la Magazeti ya Serikali (SMS) linalochapisha magazeti ya Zanzibar Leo, Zanzibar Leo Jumapili na Zaspoti, Waziri Mbarouk alisema Shirika hilo limepiga hatua kubwa ya kuwafikishia wasomaji huduma muhimu ya habari katika maeneo mbali mbali ya ndani ya Zanzibar na mikoa mbali mbali ya Tanzania Bara.

Alisema katika kuongeza idadi ya magazeti yanayochapishwa Shirika limeimarisha magazeti yake katika utoaji wa taarifa na upangaji wa habari zake pamoja na kuwajengea uwezo wafanyakazi wake ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kuongeza uzalishaji.

Aidha alisema hatua ya kuliweka gazeti hilo katika tovuti 'website' ya Shirika zinaendelea, huku Shirika hilo likitiliana saini MoU baina ya shirika hilo na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), ili kushirikiana katika mambo mbali mbali ya habari, taaluma na teknolojia.

Katika hotuba hiyo, Waziri Mbarouk ameliomba Baraza la Wawakilishi kujadili kwa kina matumizi ya shilingi 9,985,000,000 kwa kazi za kawaida na shilingi 510,000,000 kwa kazi za maendeleo.

Kikao cha Baraza la Wawakilishi kinatarajiwa kuendelea tena leo, ambapo Wajumbe wa Baraza hilo watapata nafasi ya kuijadili na kuichangia bajeti ya Wizara hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.