Na Mwantanga Ame
MBUNGE wa Jimbo la Kitope, Balozi Seif Ali Iddi, amewataka wazazi wa kijiji cha Mgonjoni, kuwaandaa watoto wao kuwa wataalamu wa baadae kwa kuhakikisha wanawasomesha zaidi badala kuwaacha bila elimu.
Balozi Seif, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa kijiji hicho kilichopo shehia ya Kilombero.
Balozi Seif, ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka wananchi hao kutokata tamaa ya kuwasomesha watoto wao licha ya msafa marefu yaliyopo kufuata huduma hiyo katika kijiji cha jirani.
Alikiri kwamba hali ya kijiji hicho bado ipo nyuma kimaendeleo, lakini wazazi bado wana wajibu kuhakikisha watoto wao wanapata elimu.
Alisema iwapo wazazi watazingatia umuhimu wa elimu kwa watoto wao watasaidia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kijiji hicho siku za usoni.
Alisema hakuna urithi bora kwa watoto isipokuwa elimu ambayo ndiyo itakayobadilisha maisha yao kiuchumi na maendeleo ya kijiji hicho.
“Kinamama muelewe kwamba mtakuwa na kazi ya ziada katika kuwahimiza watoto wenu kwenda kutafuta elimu,” alisema.
Katika kuunga mkono juhudi za wananchi wa kijiji hicho, Balozi Seif alichangia shilingi 1,000,000 kwa ajili ya ununuzi wa matofali, saruji na fedha za fundi kwa ajili ya ujenzi wa msikiti.
Balozi Seif pia aliwapatia wananchi hao vyakula aina mbali mbali kwa ajili ya futari na nguo za kike na kiume kwa ajili ya sikukuu.
Balozi Seif, aliwahakikishia wananchi hao kwamba uongozi wa jimbo hilo utaendelea kutafuta mbinu mbali za kutatua matatizo yanayowakabili likiwemo suala la madrasa na skuli.
Naye mke wa mbunge huyo, mama Asha Suleiman Iddi aliwaomba akinamama wa kijiji hicho kujikusanya pamoja na kuunda kikundi cha ushirika na yeye atakuwa tayari kuwapatia mtaji.
Mapema asubuhi, mama Asha alikabidhi vifaa mbali mbali kwa ajili ya uendelezaji wa ujenzi wa madrasat Mujitahidina iliyopo katika kijiji cha Kitope Tobora.
Vifaa hivyo ni pamoja na matofali, nondo, mchanga, fedha za fundi pamoja na kukipatia chuo hicho misahafu na juzuu kwa ajili ya wanafunzi.
Akizungumza na walimu, wanafunzi na wazazi wa kijiji hicho, mama Asha aliwasihi washirika na wahisani wa ujenzi wa misikiti nchini hivi sasa kuelekeza nguvu zao katika ujenzi wa madrasa za Quran.
Aliwakumbusha waumini kurejea katika maadili ya zamani ya upendo miongoni mwao ili ile sumu ya chuki, uhasama na matendo mengine maovu wanayofanyiana waumini hao yapungue.
No comments:
Post a Comment