Na Said Ameir
The Hague, Uholanzi
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed
Shein amesema Serikali haina nia ya kuwanyima wazanzibari wanaoishi
ughaibuni kitambulisho cha mzanzibari mkaazi isipokuwa suala hilo ni la
kisheria hivyo kupewa kwake ni lazima mhusika atimize matakwa ya kisheria.
Kauli hiyo ameitoa hivi karibuni nchini Uholanzi alipokuwa akizungumza na
watanzania wanaoishi nchini humo wakati wa ziara yake ya siku tano kwa
mwaliko wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo bwana Mark Rutte.
“Kitambulisho cha mzanzibari ni suala la kisheria hivyo mlengwa ni lazima
atimize matakwa ya kisheria mojawapo ni la mwanachi kukaa katika eneo lake
si chini ya miezi 36” alibainisha Dk. Shein na kuongeza kuwa mzanzibari
mwenye sifa za kupata kitambulisho hicho ikitokea akanyimwa anayo haki ya
kukata rufaa kwa mamlaka husika.
Alieleza kuwa nia ya kuanzisha idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya
Nje na kitengo kama hicho katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kunaonesha
sio tu kuwatambua watanzania hao wanaoishi nje ya nchi lakini
kunathibitisha dhamira ya kweli ya serikali ya kuwashirikisha watanzania
popote waliko katika kuleta maendeleo ya nchi.
Dk. Shein aliwapongeza watanzania hao kwa kufuatilia kwa karibu taarifa
kutoka nyumbani na kuonesha kuguswa na baadhi ya matukio yanayotokea
nchini ambayo baadhi yake yanaathiri taswira nzuri ya Tanzania mbele ya
jumuiya ya kimataifa.
“nimefurahi kuona kuwa mnafuatilia kwa karibu matukio yanayotokea nchini
kwetu.
Risala yenu imethibitisha maelezo yangu”alieleza Dk. Shein na
kuwaomba watanzania kuwa karibu na Ofisi za Ubalozi za nchi yao ili kupata
taarifa sahihi kuhusu hali ilivyo nchini.
Alisema si kila chombo cha habari au mitandao ya habari inatoa taarifa
sahihi kuhusu Tanzania hivyo suala la kuwasiliana na Ofisi za kibalozi
hawana budi kulizingatia.
Aliwaeleza watanzania hao kuwa ni jambo la kujivunia kuona Serikali
imeufungua tena ubalozi wake nchini Uholanzi baada ya kufugwa kwa miaka
mingi kutokana na sababu za kiuchumi.
“Tuliufunga ubalozi wetu hapa kutokana hali mbaya ya kiuchumi lakini
tumejipanga na tunaufungua upya. Balozi ameshateuliwa na harakati za
kuundaa ubalozi zinaendelea”alieleza Dk. Shein na kumpogeza balozi
Willison Masilingi kwa kuteuliwa kuwa balozi wa Tanzania nchini humo.
Alieleza hatua hiyo ni muhimu katika kuendeleza uhusiano wa Tanzania na
Uholanzi kwa kuwa nchi mbili hizo zimekuwa katika mahusiano mazuri kwa
miaka arobaini sasa.
Akijibu swali kuhusu namna serikali inavyochukua hatua za kusafisha
taswira ya nchi kutokana na matukio ya hivi karibuni ya kumwagiwa
tindikali vijana wawili toka Uingereza huko Zanzibar Dk. Shein alieleza
kuwa hatua zimechukuliwa na bado suala hilo limo mikononi mwa vyombo vya
dola kwa uchunguzi.
“Ni vitendo vilivyoanza muda mrefu tangu mtu wa kwanza kumwagiwa tindikali
mwaka 1996. Hatujui lengo la watu wanaofanya vitendo hivi… ni matukio
yanayotutia aibu, kuharibu sifa ya nchi yetu pamoja na kuhatarisha uchumi
wetu. Hivyo Serikali inalichunguza suala hili (la tindikali) kwa makini
sana” Dk. Shein aliwaeleza watanzania hao.
Alibainisha kuwa matukio kama hayo yanapotokea Serikali huchukua hatua za
haraka ikiwemo kuieleza jumuiya ya kimataifa kwa kutumia njia mbalimbali
za mawasiliano zikiwemo za kidiplomasia na mawasiliano ya wazi kupitia
vyombo vya habari.
Wakati huo huo watanzania wanaoishi nchini Uholanzi wameishukuru Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuufungua tena Ubalozi wake nchini
Uholanzi.
Shukrani hizo hizo zimetolewa wa Jumuiya ya watanzania wanaoishi Uholanzi
katika risala yao kwa Rais wa Zanzibar.
Akisoma risala hiyo Mwenyekiti wa Jumuiya ya watanzania hao Bwana Bulemo
Francis Kweba alisema kufunguliwa kwa ubalozi huo kutawapunguzia gharama
za kufuata huduma za kibalozi mjini Bruxelles Ubelgiji ambako kwa sasa
ndiko zinakopatikana.
Katika risala hiyo watanzania hao waliiomba serikali kuweka utaratibu
mzuri utakaosaidia wao kupata fursa mbalimbali nchini kama vile viwanja
vya kujenga nyumba za kuishi na biashara pamoja na ardhi ya kilimo.
Walishauri serikali kulishughulikia suala la uraia wa nchi mbili kwa
kueleza kuwa lina manufaa makubwa kwa taifa kwani litachochea uwekezaji
nchini kwa kuwa watanzania wengi wamelazimika kuchukua uraia wa nchi
nyingine ili kupata mahitaji ya msingi kama elimu, afya na ajira nzuri.
Katika ziara hiyo Dk. Shein amefuatana na Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na
Nishati wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Ramadhani Abdalla Shaaban,
Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Rashid Seif Suleiman, Naibu Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mahadhi Juma Maalim na Mshauri wa
Rais Ushirikiano wa Kimataifa, Uwekezaji na Uchumi, Balozi Mohamed Ramia.
Rais wa Zanzibar alimaliza ziara yake nchini Uholanzi jana na anatarajiwa
kurejea nchini kesho (Jumapili).
No comments:
Post a Comment