HOTUBA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR,
MHE. BALOZI SEIF A. IDDI
KATIKA UFUNGAJI WA MKUTANO WA KUMI NA MBILI
WA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR
TAREHE 07 AGOSTI, 2013
UTANGULIZI:
1.
Mheshimiwa Spika, napenda
kuchukua fursa hii adhimu kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa
kutuwezesha kwa mara nyingine tena kukutana hapa katika mkutano huu wa Kumi na
Mbili wa Baraza la Wawakilishi ambao unamalizika ndani ya mwezi Mtukufu wa
Ramadhani kwa mafanikio makubwa sana. Aidha, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa
kuijaalia nchi yetu kuendelea kuwa katika hali ya amani, utulivu, usalama na
mshikamano, mambo ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
2.
Mheshimiwa
Spika, naomba pia kutoa pongezi zangu za dhati kwako
binafsi Mheshimiwa Spika pamoja na
Wasaidizi wako wote, wakiwemo Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wenyeviti
wa Baraza kwa kuendelea kuliongoza Baraza letu kwa busara, hekima na ufanisi
mkubwa kwa kufuata misingi ya kidemokrasia na Kanuni za Baraza. Pia, napenda
kuwapongeza Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati mbali mbali za Kudumu za Baraza la
Wawakilishi na Wajumbe wote wa Baraza hili Tukufu kwa kuendelea kutekeleza
majukumu yao kwa hekima na uadilifu mkubwa.
3.
Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa napenda kuchukua fursa hii kumshukuru kwa dhati
Kiongozi wetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa uongozi wake thabit na imara uliojaa
hekima, busara na upeo mkubwa unaozingatia malengo na matarajio ya maendeleo ya
nchi yetu.
4.
Mheshimiwa Spika, sina budi pia kutoa shukrani nyingi kwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Mheshimiwa Maalim
Seif Shariff Hamad kwa kumshauri na kumsaidia vyema Mheshimiwa Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika kuiongoza nchi yetu kwa misingi ya
utawala bora. Vile vile, naomba kuwapongeza sana Mawaziri, Naibu Mawaziri,
Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na
Watendaji wote wa Serikali kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao vyema kwa
lengo la kuharakisha maendeleo ya nchi yetu.
5.
Mheshimiwa Spika, aidha, napenda kuwashukuru sana
Waandishi wa vyombo vyote vya Habari. Sisi sote
hapa ni mashuhuda jinsi Waandishi wa Habari katika Baraza walivyoweza
kufuatilia kwa makini mwenendo mzima wa matukio mbali mbali ndani na nje ya
Baraza, ikiwemo utoaji wa taarifa za hoja, michango na mijadala iliyojitokeza
Barazani na kuwafikia wananchi wetu. Nachukua nafasi hii kuvipongeza na kuvishukuru
sana vyombo hivyo kwa kutekeleza vyema jukumu lao kuwapasha habari za Baraza
wananchi ipasavyo. Natoa pongezi za
pekee kwa wakalimani wa lugha ya alama kwa kazi kubwa waliyoifanya katika
kutafsiri mijadala kwa ishara ili kuwawezesha wananchi wetu wenye ulemavu wa
kutokusikia kupata taarifa juu ya mijadala yetu ndani ya Baraza.
6.
Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa naomba nizungumzie
juu ya tukio la msiba uliotupata nchini kwetu hivi karibuni. Taifa letu
lilipokea kwa mshituko na huzuni kubwa taarifa ya vifo vya wapiganaji wetu saba
wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambao wameuawa nchini Sudan baada ya
kuvamiwa na Waasi wa Darfur katika harakati za kusaidia kuweka amani nchini
humo. Vifo vya wapiganaji hao ni msiba mkubwa kwetu sote. Ni dhahiri kuwa Wapiganaji wetu hao
wameonesha ujasiri na moyo wa uzalendo mkubwa kwa wananchi wa Tanzania na kwa
Bara la Afrika. Ni ukweli usiopingika
kuwa Wapiganaji hao wamekufa kishujaa na nimefarajika sana kuona kwamba mazishi
yao yamepewa heshima zote za Kitaifa. Katika tukio hilo la kuhuzunisha
walikuwamo wanajeshi wawili kutoka Brigedi ya Nyuki ya Zanzibar ambao ni
Sajenti – Shaibu Shehe Othman na Koplo Mohammed Juma Ali. Naomba kuchukua nafasi hii kwa niaba ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kutoa salamu za rambirambi kwa familia,
ndugu, jamaa, marafiki na wananchi wote na nawaomba wawe na subira katika
kipindi hiki kigumu cha huzuni na maombolezo, Mwenyezi Mungu azilaze roho za
Marehemu pahala pema peponi, Amin.
MASUALA MUHIMU YALIYOJIRI NCHINI
7.
Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ipo katika hatua ya
kutekeleza malengo ya maendeleo, hususan kutekeleza mikakati na sera ya matumizi
na umiliki wa ardhi, juhudi kubwa zinaendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha ardhi
tuliyonayo inatumiwa ipasavyo na inatoa tija kubwa zaidi. Lengo la mikakati na
sera za ardhi ni kutatua kwa uadilifu migogoro ya ardhi inayojitokeza mara kwa
mara hapa nchini.
Miongoni
mwa hatua zinazoendelea kuchukuliwa kuhusiana na suala la migogoro ya ardhi ni
zoezi linaloendelea la usajili wa ardhi na kuhakikisha kwamba ardhi yote ya
Zanzibar inasajiliwa na taarifa zake zinawekwa katika daftari maalumu. Madhumuni ya zoezi hilo ni kuiwezesha
Serikali kupata taarifa sahihi za watu wote ambao wana haki ya matumizi ya
ardhi. Pia, hatua hiyo itaiwezesha Serikali kupanga matumizi mazuri ya ardhi
pamoja na kuweka kumbukumbu sahihi za wamiliki wa ardhi hizo nchini.
8.
Mheshimiwa
Spika, katika hatua nyengine ya kupunguza mrundikano wa
kesi za ardhi, Serikali imepanga kuanzisha Mahakama za Ardhi katika kila Mkoa
pamoja na kuongeza idadi ya Mahakimu wa Mahakama ya Ardhi Unguja na Pemba ili
kurahisisha na kuharakisha mwenendo wa kesi za migogoro ya ardhi ambazo
zimekuwa zikiongezeka siku hadi siku.
9.
Mheshimiwa
Spika, azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuwa na
miji ya kisasa yenye huduma za aina zote.
Katika suala la upangaji wa miji na matumizi ya ardhi, Serikali
inaendelea na zoezi la utayarishaji wa “Master Plan” ya Mji wa Zanzibar na Mpango
wa Mji wa Chake Chake. Lengo ni kuipanga
upya miji hiyo ambapo suala la makaazi, biashara, viwanda na maeneo ya michezo
na mapumziko yamezingatiwa kwa kina kwani maeneo haya yote ni muhimu kwa uchumi
na afya za wananchi wetu.
10.
Mheshimiwa
Spika, naomba kuchukua nafasi hii kutoa wito kwa wananchi
na Viongozi kufuata
taratibu za usajili wa ardhi ili kuhakikisha tunakuwa na matumizi mazuri ya
ardhi pamoja na kupata ufumbuzi wa kudumu wa migogoro ya ardhi inayojitokeza
mara kwa mara. Lakini pia, ningependa
kuwasihi Watendaji wa Wizara ya Ardhi kutekeleza maagizo ya Viongozi yenye nia
ya kuleta suluhu katika migogoro ya ardhi inayojitokeza kwani wakati mwingine
wanachukua muda mrefu kutekeleza maagizo hayo.
11.
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa Zanzibar imekuwa
ikitumia chanzo kimoja cha umeme. Hali
hii imepelekea kupata malalamiko kutoka kwa wananchi pale inapotokea hitilafu
za kukosekana kwa umeme au kupanda kwa gharama za huduma hiyo muhimu. Kwa msingi huo, Serikali imetoa kipaumbele
katika kutafuta chanzo cha nishati mbadala ya uhakika badala ya kutegemea
chanzo kimoja cha umeme. Hivyo, kwa
kupitia Wizara inayohusika, Serikali inaendelea na utafiti yakinifu wa kupata
nishati mbadala. Tunatarajia baada ya utafiti huo, Zanzibar itaweza kupata
chanzo chengine cha nishati mbadala na hatimae kuwekeza katika uzalishaji wa
nishati hiyo. Mpaka hivi sasa
wamejitokeza wawekezaji kadha walioonyesha nia ya kuwekeza katika miradi ya
umeme mbadala. Wapo wa kutumia solar,
wapo wa kutumia upepo, wapo wa kutumia takataka na wapo wa kutumia mawimbi ya
bahari. Hivi sasa Serikali inachunguza
ni mradi wa aina gani utakuwa wa manufaa zaidi kwa nchi, kiuchumi na
kimazingira.
12.
Mheshimiwa Spika, hivi sasa tunakabiliwa na changamoto
nyingi za uharibifu wa mazingira, na zaidi tatizo hilo limejitokeza kutokana na
kuwepo kwa athari za mabadiliko ya tabianchi, maendeleo ya sekta ya utalii,
ujenzi wa miundombinu na ukosefu wa miundombinu ya uondoaji wa taka pamoja na
uingizaji wa bidhaa chakavu za elektroniki na mifuko ya plastiki. Katika juhudi za kukabiliana na hali hiyo,
Serikali imechukua hatua za kuanzisha Sera mpya ya Mazingira ya mwaka 2013,
Mkakati wa Zanzibar wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kuweka
Kanuni za Usimamizi Endelevu wa Maliasili zisizorejesheka pamoja na kufanya
mapitio ya Sheria ya Mazingira Namba 2 ya Mwaka 1992.
13.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hatua hizo, Serikali
imekamilisha muongozo ambao utaitaka kila Taasisi kuwa na wajibu wa kutekeleza
mipango yake kwa kuzingatia masuala ya mazingira na mabadiliko ya
tabianchi. Kwa kuzingatia umuhimu wa
suala hilo, Serikali inawashauri wananchi kupanda miti kwa wingi katika maeneo
mbali mbali hasa miti ya matunda na mazao ya biashara.
Naomba kuwatanabahisha
wananchi kwamba Serikali haitamvumilia mwananchi yeyote ataekwenda kinyume na
taratibu za uhifadhi wa mazingira nchini.
Kwa sababu kama hatukuwa waangalifu katika kuyalinda mazingira yetu,
nchi yetu itaweza kupata majanga makubwa.
14.
Mheshimiwa Spika, katika muktadha wa
kuhifadhi mazingira na kumlinda mtumiaji, naomba kuliarifu Baraza lako Tukufu kwamba Serikali kupitia Taasisi
zinazohusika imeweza kuangamiza tani 700 za unga wa ngano mbovu ulioingizwa
nchini kinyume na Sheria. Naomba kuchukua nafasi hii kuishukuru kwa dhati
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais,
kwa mashirikiano makubwa iliyotupa kufanikisha uangamizaji wa unga huo. Katika
kuhakikisha kuwa tunakuwa na mfumo madhubuti wa kusimamia ubora wa bidhaa
nchini, Serikali inaifanyia marekebisho Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi ya
Mwaka 2006 kwa lengo la kudhibiti uingizaji na utumiaji wa bidhaa hizo.
15.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
inawaagiza wafanyabiashara wote kuwa makini wakati wa kuingiza nchini bidhaa
zao zisiwe zilizopitwa au zinazokaribia kupitwa na muda wake wa matumizi pamoja
na bidhaa mbovu. Serikali itawachukulia hatua kali wafanyabiashara wote
watakaokwenda kinyume na agizo hili, kwani ni wajibu wa Serikali kuwalinda
wananchi wasile vyakula vibovu vitakavyoweza kuwaletea madhara.
16.
Mheshimiwa Spika, katika kufanikisha utekelezaji mzuri
wa masuala ya viwango vya bidhaa, Serikali inaijengea uwezo Taasisi ya Viwango
ya Zanzibar (Zanzibar Beurau of Standards – ZBS) ili iweze kuweka viwango vya
bidhaa zinazoingizwa na kutengenezwa nchini.
Azma hiyo inatokana na umuhimu wa kuepusha nchi yetu kugeuzwa kuwa jaa
la kutupia bidhaa mbovu na zisizo na viwango na kulinda afya za wananchi
wetu. Wizara ya Biashara inaagizwa kuona
umuhimu wa kuzikagua bidhaa kabla ya kuingizwa nchini kwani kumekuwepo na
malalamiko kuwa Zanzibar ni njia ya kupitisha bidhaa mbovu. Taasisi ya Viwango ya Zanzibar (ZBC)
inashauriwa kufungua ofisi nje ya nchi ili kuzikagua bidhaa zinazotaka
kuingizwa nchini kabla ya kuingizwa nchini bidhaa hizo.
17.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la kuendeleza zoezi la
Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivi sasa jamii
imeshaunda Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na hatua za kukusanya maoni kupitia
Mabaraza hayo inaendelea. Napenda kuwapongeza Wajumbe wote wanaowakilisha
Mabaraza hayo kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwasilisha mawazo yao kwa amani
na utulivu. Hilo ni jambo la msingi sana
katika kuhakikisha kuwa Wazanzibari wanawasilisha maoni yao ya Kikatiba kwa
kufuata taratibu zilizowekwa kwa misingi ya demokrasia. Ni matarajio yetu kwamba ushiriki wa wananchi
kupitia Mabaraza hayo utakuwa na mafanikio na hatimae tutaweza kupata Katiba
ambayo itakuwa na maslahi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa nchi yetu na
wananchi wake. Hivyo, wananchi wanaombwa kutoa maoni yao kwa uhuru na uwazi
bila ya woga.
18.
Mheshimiwa Spika, katika hatua nyengine zinazochukuliwa
kuimarisha Demokrasia na Utawala Bora nchini, Serikali inaendelea kuratibu
vyema zoezi la uhakiki wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kupitia Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC). Lengo la
zoezi hilo, ni kuwaandikisha wale wote wanaostahiki na kuwatoa wale ambao
hawastahiki. Hili ni zoezi muhimu kwa
maslahi ya kisiasa kwa wananchi wetu.
Napenda kutoa wito kwa wananchi wote kushiriki kwa kikamilifu katika
zoezi hilo. Katika kufanikisha zoezi
hili kwa amani na utulivu, nawasihi wananchi wote kufuata sheria na taratibu za
uandikishaji zilizowekwa ikiwemo kuwa na ithibati zote zinazohitajika ili
kuweza kuandikishwa bila ya bughudha.
Wananchi wanaonywa kutowafanyia hila au vurugu wananchi wenzao ili
kuwazuia wasijiandikishe. Hilo ni kosa
la jinai na mtu atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria.
19.
Mheshimiwa Spika, ni jambo la faraja kuona kuwa sekta ya uvuvi imezidi kuimarika kutokana na
kuongezeka kwa shughuli za uvuvi wa baharini na pia wananchi wengi wameanza
kufuga samaki na mazao mengine ya baharini. Mafanikio makubwa yameweza
kupatikana hasa katika kisiwa cha Pemba.
Uchambuzi wa takwimu umeonesha kwamba katika kipindi
cha mwaka 2012/2013 sekta ya uvuvi imepata mafanikio makubwa matatu yafuatayo:-
20.
Mheshimiwa Spika, kwanza, idadi ya samaki wanaovuliwa imeongezeka
kutoka tani milioni 28.8 hadi 29.4, sawa na ongezeko la tani 651 ambayo ni
asilimia 2.3. Pili, wingi wa samaki
wanaovunwa umefikia jumla ya tani 9.8 kwa mwaka ambapo Pemba imevuna tani 7.7
na Unguja tani 2.1 kwa mwaka 2012/2013.
Tatu, mafanikio makubwa katika zao la mwani kutoka tani 13 elfu mwaka
2011 mpaka tani 15 elfu mwaka 2013 ikiwa ni ongezeko la asilimia 16.
21.
Mheshimiwa Spika, kwa jumla shughuli zote za kilimo cha mwani, uvuvi
wa baharini na samaki wa kufuga, zimeweza kusaidia kuongeza kipato cha wananchi
sambamba na malengo ya Mpango wa Pili wa
Kupunguza Umaskini (MKUZA II) pamoja na
Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2010/2015. Katika kuendelea kuyalinda mazalio ya samaki,
tunawasihi wavuvi kuacha uvuvi haramu, kwani uvuvi haramu unaweza kusabibisha
uharibifu wa mazalia ya samaki na hivyo kupunguza idadi ya samaki
baharini. Wavuvi wakumbuke kuwa wakivua
leo, waweke akiba ili waweze kuvua na kesho.
22.
Mheshimiwa Spika, hali ya sekta ya mifugo nayo imeanza kutoa matumaini yenye kutia
moyo. Miongoni mwa mafanikio hayo ni kuimarika kwa utoaji wa huduma za
uzalishaji na utibabu wa mifugo. Pia kujengwa kwa mitambo mipya ya gesi asilia
(biogas) kumi na moja (11), Unguja minane na Pemba mitatu. Kukamilika kwa
ujenzi wa mitambo hiyo kumepelekea kuwa na mitambo 24 kwa Unguja na Pemba iliyokwisha
kujengwa.
23.
Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kuwawezesha wananchi kiuchumi
Serikali imetoa jumla ya mikopo 193 yenye thamani ya Shilingi Milioni 156 kwa
kupitia Mfuko wa Kujitegemea. Aidha,
Serikali imetoa Shilingi Milioni 303 kwa Vyama vya Ushirika na vikundi vya
wajasiriamali 199 kwa kupitia Mfuko wa Zaka.
24.
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha uratibu wa utoaji wa mikopo
midogo midogo, Serikali imeanzisha mtandao wa Taasisi zinazotoa huduma za fedha
kwa wajasiriamali wadogo. Mtandao huo unajumuisha taasisi mbali mbali zikiwemo
WEDTF, YOSEFO, Benki ya CRDB, Changamoto, Melinne SACCOS na Jumuiya ya
Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Zanzibar. Lengo la mtandao huo ni
kubadilishana taarifa za wakopaji ili kuweza kutathmini idadi ya watu wanaofikiwa
kwa huduma za mikopo na pia kuimarisha mashirikiano katika huduma zao. Hatua hii inasaidia kubainisha thamani na
aina ya mikopo ambayo hutolewa na taasisi mbali mbali kwa wajasiriamali na
namna mikopo hiyo inavyowasaidia wajasiriamali hao kuendesha maisha yao na
kujikomboa kutoka kwenye umasikini.
25.
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha usafiri wa baharini, mnamo tarehe
10 Julai, 2013, Serikali imetiliana saini mkataba wa ujenzi wa meli ya abiria
na mizigo na kampuni ya Daewoo ya Korea ya Kusini. Meli hiyo ambayo itakuwa na
uwezo wa kuchukua abiria 1200 katika daraja tatu tofauti na uwezo wa kubeba
mizigo yenye uzito wa tani 200, itakamilika ujenzi wake baada ya miezi 23
kuanzia Julai mwaka huu.
26.
Mheshimiwa Spika, hatua hii imekwenda sambamba na ukarabati wa jengo
jipya la abiria katika eneo la bandarini kwa mashirikiano na mwekezaji wa
kizalendo S.S. Bakhresa wa Kampuni ya Azam Marine. Uzinduzi wa mradi huu
umefanyika rasmi tarehe 8 Julai, 2013.
Serikali inatoa shukurani za dhati kwa Uongozi wa Kampuni ya Azam Marine
kwa mchango wao mkubwa katika kusaidia maendeleo ya shughuli za usafiri kwa
kuwaondolea bughdha wasafiri.
27.
Mheshimiwa Spika, tarehe 12 Januari, 2014, nchi yetu
itaadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Maadhimisho hayo
yanatarajiwa kuwa ya aina yake na yatazinduliwa rasmi na Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein tarehe 15
Agosti, 2013. Kwa lengo la kufanikisha sherehe za maadhimisho hayo, Serikali
inatoa wito maalumu kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kwa pamoja na
sekta binafsi kushirikiana na Serikali ili kuzifanya sherehe hizo kuwa za
kihistoria pamoja na kuzipa hadhi ya juu
na ya kipekee.
Sherehe hizo zitajumuisha mafanikio ya
utekelezaji wa sekta zote za uzalishaji na utoaji wa huduma kwa kuonesha
maendeleo yao ya miaka 50 ya Mapinduzi. Madhumuni ya kufanya sherehe hizo
yanatokana na haja ya wananchi wa Zanzibar kuelewa na kutathmini wapi
tulipotoka, tulipo sasa na wapi tunapokusudia kwenda kwa mtazamo wa kuinua hali
za maisha ya wananchi walio wengi na kuharakisha maendeleo ya nchi kwa jumla.
MAMBO MUHIMU YALIOJITOKEZA BARAZANI
28.
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu wa 12 wa Baraza lako
Tukufu, Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza
walijadili na kupitisha Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha
2013/2014. Aidha, Waheshimiwa Mawaziri
wamewasilisha Miswada miwili ya sheria ambayo ina umuhimu mkubwa kwa ustawi na
maendeleo ya nchi yetu.
29.
Mheshimiwa Spika, Mswada wa kwanza uliojadiliwa ni Mswada wa Sheria ya
Kutoza Kodi na Kubadilisha baadhi ya
Sheria za Fedha na Kodi Kuhusiana na Ukusanyaji na Udhibiti wa Mapato ya
Serikali na mambo mengine yanayohusiana na hayo. Madhumuni ya mswada huo ni kudhibiti mianya
ya uvujaji wa mapato ya Serikali na kuweka utaratibu mzuri wa udhibiti
ukusanyaji wa mapato.
30.
Mheshimiwa Spika, Mswada wa Pili ni Mswada wa Sheria ya Matumizi ya Fedha za Umma (Appropriation Bill).
31.
Mheshimiwa Spika, katika kikao hiki cha kumi na mbili
Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara zote waliwasilisha hotuba za Mapato na Matumizi
za Wizara zao kwa mwaka fedha 2013/2014, na Waheshimiwa Wajumbe walipata nafasi
ya kuzijadili, kuzichangia kwa uangalifu, umakini na uadilifu mkubwa na hatimae
kuzipitisha. Waheshimiwa Wajumbe
walipata nafasi ya kuhoji kwa yale mambo ambayo walihisi hayakuwa bayana na
yalihitaji ufafanuzi na Waheshimiwa Mawaziri kwa mujibu wa Kanuni za Baraza
walitoa ufafanuzi unaostahiki na hatimae Wajumbe walizipitisha bajeti za mwaka
huu, ingawa baadhi ya Bajeti hizo zilipita kwa mbinde. Hii imeonyesha umakini mkubwa waliokuwa nao
Wajumbe wa Baraza. Naomba kusisitiza
kwamba baada ya Baraza kufanya kazi kubwa ya kuzichambua, kuzihakiki na kutoa
mapendekezo katika Bajeti za Wizara mbali mbali, Uongozi wa Wizara zote kuwa
makini katika matumizi na usimamizi kwa mujibu wa malengo na taratibu za
matumizi ya fedha. Waheshimiwa Mawaziri
na Makatibu Wakuu wanaombwa kusimamia kwa makini matumizi ya fedha za Wizara
zao zilizoidhinishwa na Baraza hili.
32.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya Wajumbe katika uchangiaji wa
bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi walihoji juu ya uagizaji wa kuku kutoka nje
ya nchi. Mjadala mrefu ulitokana na wasiwasi wa baadhi ya Wajumbe hao kuwa
uingizaji wa bidhaa hiyo utadhoofisha soko kwa wafugaji wa ndani na hatimae
kuwakosesha kipato wafugaji hao. Ukweli
dhana hiyo sio kweli kwani Serikali inazingatia sana hali za wananchi wake si
wafugaji au wafanyabiashara pekee. Kabla ya Serikali kufanya uamuzi huu,
ililitafakari kwa kina suala hili na hatimae kufanya uamuzi huo baada ya kuona
kuwa haukuwa na madhara kwa wafugaji wetu.
Hata hivyo, naomba kueleza kuwa Serikali
kwa muda mrefu hapo nyuma iliamua kuchukua hatua za kuimarisha ushindani wa
kibiashara. Lakini tatizo kubwa linalojitokeza ni kwamba mahitaji ya soko la
kuku Zanzibar ni kubwa. Kwa hivyo, kwa
kipindi hiki si vyema kuchukua hatua yoyote ya kubana uingizaji wa kuku kutoka
nje hadi pale soko la ndani litakapoweza kujitosheleza. Kwani tukichukua hatua
hiyo ghafla tunaweza kuhatarisha mahitaji halisi ya biashara katika sekta
nyengine hasa sekta ya utalii nchini.
33.
Mheshimiwa Spika, nawaomba Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu wasilichukulie suala
hili kuwa sawa na wenzetu wa Tanzania Bara. Tukijilinganisha na wao kwa hali zetu
tutakosea kwani sababu zao ni tofauti na zetu kwa sababu:-
a) Wenzetu Tanzania Bara wana wafugaji wengi
wanaozalisha kwa viwango vinavyotakiwa.
b) Waliamua kuzuia uletaji wa kuku pamoja na mambo mengine kwa sababu ya maradhi. Mambo ambayo uletaji wa kuku wetu huwa
yanazingatiwa kwa kiwango kikubwa.
c) Wananchi wetu wengi hawawezi kumudu bei
za kuku hapa nchini. Hii ni kutokana na gharama kubwa mno za
uzalishaji.
Kwa maana hiyo Serikali haikupuuza
ushauri wa baadhi ya Wajumbe wa Baraza bali itaendelea kufanya utafiti wa hali
halisi ya biashara hiyo ili tufaidike sote, wafugaji na walaji pia.
34.
Mheshimiwa Spika, kwa kuelewa wasiwasi wa wafugaji wa kuku wa
ndani, Serikali itaendelea kuangalia mwenendo mzima wa uzalishaji na uagizaji
wa kuku ili kuhakikisha kuwa wafugaji wa ndani hawaathiriwi na suala hilo, kama
Baraza lilivyoelekeza. Serikali
itawasaidia wafugaji wetu ili wazalishe zaidi ili tuweze kupunguza uagizaji
kidogo kidogo hadi pale tutakapojitosheleza kwa ukamilifu.
35.
Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilisha kazi za awali za
mradi wa E-Government ikiwemo kutandika Mkonga wa “Fibre Optic” Serikali
imeendelea na kazi za kuimarisha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Kutokana na umuhimu wa suala hilo, hata Wajumbe
wa Baraza walichangia sana juu ya haja ya kukamilisha mradi wa
E-Government. Hivyo, napenda kuchukua
nafasi hii kuwahakikishia Wajumbe pamoja na wananchi kuwa Serikali imekusudia
kwa dhati kufanikisha mradi huu haraka iwezekanavyo.
36.
Mheshimiwa Spika, madhumuni hasa ya mradi huu yanalenga
katika kuendesha na kusimamia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
katika sekta ya Utumishi wa Umma ili kuhakikisha kuwa usimamizi wa kumbukumbu
za eletroniki pamoja na teknolojia ya habari na mawasiliano unatumika katika
kuimarisha huduma za Utawala Bora. Mradi
huu utaanzisha mfumo wa pamoja utakaotumiwa na Taasisi zote za umma pamoja na
kuweka mazingira mazuri ya utekelezaji wa jumla kwa mujibu wa dhana ya
kuimarisha utoaji wa huduma za Serikali zilizounganishwa ki-eletroniki.
37.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya mtandao kwa muda huu
tulionao ni kitu cha lazima. Kwa msingi
huo, naomba nitoe tahadhari kuwa mafanikio ya mradi huu yatafikiwa sambamba na
jamii kuweza kutumia vyema teknolojia ya kompyuta. Hatua hii itapelekea haja ya Viongozi,
watumishi wa Serikali pamoja na wananchi kuchukua juhudi za makusudi kujifunza
kutumia kompyuta. Tukizingatia kwamba
teknolojia hii inakuwa kwa haraka mno na tusisite kujifunza hivi sasa kwani
tukijifunza baadae tutakuwa tumechelewa mno na hivyo tutapitwa na wakati.
38.
Mheshimiwa
Spika, napenda kulihakikishia Baraza lako Tukufu kuwa,
Serikali inaendelea na juhudi za kuimarisha sekta za utoaji huduma, ikiwemo
sekta za maji safi na salama, afya, elimu na miundombinu. Kwa upande wa
uzalishaji, Serikali itaendelea kutoa kipaumbele kwa kuimarisha sekta za
kilimo, mifugo na uvuvi, viwanda vidogo vidogo, utalii na biashara nchini.
Lengo kuu la juhudi hizi zinazochukuliwa na Serikali ni kukuza uchumi na
kupunguza umasikini katika nchi yetu.
39.
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kusisitiza mambo
yafuatayo: Kwanza, Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wajue kuwa
tumemaliza Mkutano wa Baraza hili la kumi na mbili na hivyo ni vyema wakarudi
katika Majimbo yao ili kushirikiana na wananchi wao katika harakati za kuleta
maendeleo kwa nia ya kuimarisha maelewano baina ya wananchi na Wawakilishi
wao. Pili, katika suala la ardhi
tunawaomba wananchi na Viongozi kufuata taratibu zilizowekwa katika suala la
uhifadhi wa mazingira, umiliki na matumizi mazuri ya ardhi, pamoja na Viongozi
wa ngazi zote kuacha kabisa tabia potofu zinazochangia ongezeko la migogoro ya
ardhi nchini. Tatu, kwa upande wa
Watendaji Wakuu wa Serikali tunasisitiza uwajibikaji kwa mujibu wa Sheria ya
Utumishi wa Umma na kuhakikisha utekelezaji wa malengo ya bajeti unaendeshwa
kwa misingi ya uadilifu kama ilivyosisitizwa katika mkutano huu wa kumi na
mbili kwa azma ya kufikia matarajio ya Wizara zetu. Agizo hili liende sambamba na utekelezaji wa
Sheria ya Matumizi ya Fedha za Umma na tuepukane kabisa na mtindo wa
utekelezaji wa kufanya kazi kwa kutumia uzoefu “business as usual.” Serikali itaendelea kuliunga mkono Baraza la
Wawakilishi katika juhudi zake za kuwafichua Watendaji wabadhirifu na wabinafsi
na kuwachukulia hatua wanazostahiki.
Lakini kuifanikisha kazi hii lazima sote tuwe na sauti moja, ya
kuwafichua na siyo wengine kuwa mawakili wa wafichuliwa.
40.
Mheshimiwa
Spika, kabla ya kumaliza hotuba yangu, ningependa nieleze machache kuhusu
suala zima la amani na utulivu katika nchi yetu. Nalisema hili kwa sababu kila mmoja wetu
naamini anafahamu umuhimu wa amani kwa nchi yoyote ile sio hapa nyumbani
tu. Kwa maana hiyo ndio sababu Mataifa
mbali mbali huwa makali wakati nchi zao zinapohatarishiwa utulivu na amani yao.
Hivi
karibuni amejitokeza kiongozi wa kidini kutoka nje ya visiwa hivi na kuanza
kupita misikitini kwa lengo la kutoa mihadhara ya uchochezi dhidi ya Serikali
na Viongozi wake. Mihadhara ambayo ilikuwa ya kuwapotosha wananchi.
Kitendo
hicho kwa kweli ni cha kusikitisha na hakikuwa cha kiungwana na kinakwenda
kinyume na maadili ya dini yenyewe ya Kiislam, licha ya kuhatarisha amani na
utulivu uliopo. Lazima ifahamike wazi
kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika suala la kudumisha amani haina
stahamala wala muhali. Haitosita
kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria za nchi kwa kikundi au mtu yeyote
atakayeonekana kujiingiza kwa njia moja au nyengine katika kuchezea amani yetu. Serikali itailinda amani ya nchi na wananchi
wake kwa gharama yoyote ile.
41.
Mheshimiwa Spika, Zanzibar
haina mgongano wowote wa dini wala
waumini wa dini zozote, endapo Viongozi na waumini wake watafanya ibada
zao kwa kufuata sheria na taratibu za nchi zilizowekwa. Kwa mnasaba huo, Serikali haitakubali kuona
kiongozi wa dini kufanya mahubiri yanayoelekeza sura za uchochezi zinazopelekea
kuondoa utulivu badala ya mshikamano wa raia wote.
Hivyo,
Serikali inalaani vitendo vya mahubiri ya aina hiyo hususan kitendo cha
kiongozi huyo kufanya mihadhara ndani ya misikiti kadhaa hapa nchini kwa lengo
la uchochezi. Katu hakitavumiliwa, na Serikali haitahofu kutupiwa lawama kwa
hatua itakazochukua dhidi ya watu wa aina hiyo.
Hii ni kwa sababu sote tunafahamu kuwa amani na utulivu tulionao umepatikana
kwa gharama kubwa.
Hapa
ningependa kuwaasa wananchi wasiwaunge mkono viongozi wa aina hiyo, kwani
hawaitakii mema nchi yetu na wanataka kuturejesha nyuma katika hali ya uadui,
uhasama miongoni mwa jamii yetu.
42.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha muhubiri huyo kuleta uchochezi nchini
mwetu kupitia Misikitini ni kutusababishia kutokea kwa vurugu nchini ambapo
hatimae ni sisi wenyewe ndio tutakaoumizana.
Muhubiri huyo amekaanga mbuyu na kuwaachia wenye meno watafune. Zikitokea vurugu na ukosefu wa amani nchini,
tutakaoumizana ni sisi, yeye atakuwa hayupo wala mkewe na watoto wake. Nawasihi sana wananchi wasiyafuate mahubiri
hayo.
43.
Mheshimiwa Spika, nimepata habari kuwa kuna kikundi cha watu kimeanzisha
utaratibu wa kupita katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba na kuwahoji
wananchi kuwa ni wafuasi wa Chama gani – CCM au CUF. Wamekuwa kama wanajaribu kufanya sensa ya
kujua katika maeneo hayo kuna wanachama wangapi wa CCM na wangapi wa CUF.
44.
Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuwaeleza wananchi wote kwamba
Serikali haina habari na zoezi hilo na wala haijatoa agizo la kufanyika kwa
sensa hiyo. Hivyo, ninawaomba wananchi
wasikubali kushiriki katika zoezi hilo ambalo halina baraka za Serikali. Aidha, ningependa kukionya kikundi hicho
kuliacha zoezi hili mara moja kwa sababu Serikali haiendeshi sensa ya aina
hiyo.
45.
Mheshimiwa Spika, katika suala hili ningependa kuwaomba Masheha wote,
Unguja na Pemba kulifuatilia suala hilo kwa karibu na kuhakikisha kuwa zoezi
hilo halifanyiki katika maeneo yao.
46.
Mheshimiwa Spika, katika mikutano kadhaa ya Baraza, na hasa katika
Mkutano huu wa Bajeti jambo moja limekuwa likijitokeza sana, nalo ni matumizi
ya taarifa na nyaraka za Serikali ambazo baadhi yao ni za siri.
Kuhusiana na suala hili, kwanza nitangulie kueleza
wazi kuwa Serikali inaelewa na kuthamini kuwa msingi mmoja wa Utawala Bora ni uwazi. Lakini naamini kuwa Waheshimiwa Wajumbe wote
watakubaliana nami kuwa uwazi hauna maana kuwa hakuna utaratibu tena wa kupata
taarifa na nyaraka za siri za Serikali, na wala haina maana kuwa ni ruhusa kwa
kila mwenye taarifa ya Serikali au hata taarifa za mtu binafsi azisambaze kwa
kadri apendavyo yeye, kwani kwa upande wa pili, moja ya msingi mkuu wa haki za
binaadamu ni haki ya faragha.
Tumeshuhudia mara kadhaa, Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza hili
wakilalamika na kuwa wakati kwa taarifa zao binafsi kama zile za maslahi yao
kuwekwa hadharani bila ya ridhaa zao.
Hivyo, naomba kutanabahisha kuwa, kwanza kwa mujibu wa
Sheria ya Kinga, Haki na Fursa ya Baraza la Wawakilishi Namba 4 ya mwaka 2007,
hasa kifungu cha 9 inaelezwa wazi kuwa ni haki ya Wajumbe kupata taarifa kutoka
Serikalini ili mradi tu taarifa hizo hazizuiliki kutolewa kwa mujibu wa
masharti ya kifungu cha 19 cha Sheria hiyo.
Hata hivyo, kifungu chenyewe cha 9 cha Sheria hiyo ya Kinga, Haki na
Fursa za Baraza kinaeleza wazi kuwa Wajumbe wana haki ya kupata taarifa kwa
kufuata Sheria na Taratibu zilizowekwa na Sheria yenyewe, Sheria nyengine za
nchi na taratibu za Serikali za kupata taarifa.
Miongoni mwa taratibu zilizowekwa na Sheria ya Kinga ni kwa taarifa
kutolewa na Ofisa muhusika kwa Baraza au kwa Kamati. Aidha, kama Mjumbe anataka taarifa kutoka
katika Taasisi ya Umma na kama taarifa hizo si za matumizi ya jumla ya umma,
utaratibu uliopo ni kwa kupitia Ofisi ya Baraza. Mbali ya Sheria hiyo ya Kinga kuweka taratibu
nilizoeleza, naomba niwatanabahishe watumishi na watendaji wa Taasisi za Umma
kuwa Sheria ya Siri za Serikali, Namba 5 ya mwaka 1983, chini ya kifungu cha 5
cha Sheria hiyo imeweka bayana kuwa ni kosa la jinai kwa mtu yeyote kutoa
taarifa za Serikali ambazo ama amekabidhiwa au amezipata kwa sababu ya kazi au
wadhifa wake kwa mtu asiyehusika. Adhabu
ya kosa hilo ni kifungo kisichozidi miaka kumi na mbili bila ya faini.
47.
Mheshimiwa
Spika, sio nia wala madhumuni ya Serikali kuficha au kuzuia taarifa za uovu wowote unaofanywa na mtendaji
yeyote wa Serikali bali inachosisitiza kufuatwa kwa taratibu. Serikali inaamini kuwa Sheria na taratibu
ziliopo kwa Waheshimiwa Wajumbe kupata taarifa wanazohitaji, zinatoa fursa ya
kutosha kufanya hivyo kihalali bila ya kuvunja sheria wala taratibu
ziliopo. Bila ya kufuata taratibu
yatajitokeza mambo kadhaa kama tulivyoanza kuyaona. Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na taarifa
kutolewa nusu nusu au za upande mmoja ili mradi mjumbe ajenge hoja anayopenda
yeye na hivyo kuwapotosha Waheshimiwa Wajumbe na wananchi kwa jumla. Aidha, baadhi ya taarifa zinapotolewa upande
mmoja zinahatarisha maisha na usalama wa baadhi ya watendaji kwa kuonyesha kama
kwamba wao ndio waliotoa uamuzi wakati wanafanya hivyo katika kutekeleza
majukumu ya kazi zao.
48.
Mheshimiwa Spika, katika
Mkutano huu tunaouahirisha leo, jumla ya maswali 104 ya msingi na masuala 246
ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wawakilishi na kujibiwa na Waheshimiwa
Mawaziri husika. Nawapongeza sana Waheshimiwa Wajumbe kwa kuja na masuala
mazuri yenye lengo la kujenga zaidi na kuimarisha uwajibikaji wa watendaji wa
Serikali. Aidha, nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri kwa majibu yao ya kina ambayo
hatimaye yaliwaridhisha Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu.
49.
Mheshimiwa Spika, ikiwa tunaendelea kutekeleza Ibada ya Mwezi Mtukufu wa
Ramadhani, naomba tuendelee kuimarisha amani na utulivu iliyopo nchini kwetu
ili tuweze kunufaika na neema alizotujalia Mwenyezi Mungu pamoja na kupata
fadhila za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Kwa kuwa hapatakuwa na kikao chengine
cha Baraza kwa kipindi hiki cha karibu naomba pia kuchukua nafasi hii kutoa
mkono wa Idd-el–Fitri kwenu Wajumbe wa Baraza hili Tukufu na wananchi kwa
jumla. Nakutakieni kila la kheri na baraka katika Sikukuu hii adhim ya Idd El
Fitri.
50.
Mheshimiwa Spika, kwa mara nyengine tena naomba kuchukua nafasi hii
kukushukuru wewe binafsi, Wajumbe wa Baraza lako, Waandishi wa Habari na
Wananchi wote kwa mashirikiano yao makubwa katika kuliendesha Baraza letu kwa
mafanikio. Ni matarajio yetu kwamba wananchi wataendelea kuwa karibu nasi
katika kuimarisha demokrasia na utawala bora pamoja na maendeleo ya Taifa
letu. Nawatakia safari ya salama
Waheshimiwa Wajumbe wote ya kurejea majimboni mwao.
51.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa
naomba
kutoa hoja ya kuliakhirisha Baraza lako Tukufu hadi siku ya Jumatano, tarehe 9
Oktoba, 2013 saa 3.00 barabara za asubuhi panapo majaaliwa.
52.
Mheshimiwa Spika,
naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment