Habari za Punde

Hutuba ya Mkuu wa Chuo Nd. Saleh Yussuf Mnemo.

                Mkuu wa Chuo cha Uandishi wa Habari Zanzibar
                              Nd. Saleh Yussuf Mnemo.

HOTUBA YA MKUU WA CHUO KATIKA SHEREHE YA KUMUAGA MKURUGENZI       MWENZA WA DARASA LA CONFUCIUS ZANZIBAR


Watendaji Wakuu wa Chuo cha Uandishi wa Habari Zanzibar;
Mwalimu Msimamizi Mkuu wa Somo la Kichina na Mkurugenzi Mwenza wa Darasa la Confucius;
Walimu;
Wageni waalikwa na wafanyakazi wote.
Assalaam aleikum

Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wote mliohudhuria katika sherehe hii ndogo ya kumuaga mwalimu wetu Bibi Xu Shuang. Shukrani makhsusi ninazitoa kwake kwa kukubali kuwa nasi katika sherehe hii. Kila mmoja kati yetu ameonesha upendo kwa kuwepo kwake.

Hata hivyo, maagano haya hayaashirii furaha ya kutengana, wala sababu kuwa kila mmoja amemchoka mwenzake, bali ni ishara ya mawafikiano na njia bora zaidi ya kufungua makubaliano na kuendeleza udugu baina ya waaganaji binafsi na taasisi wanazoziwakilisha, ambazo ni Redio ya Kimataifa ya China (CRI) na Chuo cha Uandishi wa Habari Zanzibar (ZJMMC).

Miaka miwili ya kazi katika Chuo hiki kwetu ilikuwa ni ya faraja. Bi Xu Shuang ambaye amekuwa nchini kuanzia mwezi Machi, 2011 amesaidia sana maendeleo ya Chuo. Napenda kutaja baadhi ya mambo tunayoyakumbuka ambayo kuendelea kwake kutatuwezesha kumkumbuka Bibi Khadija licha ya kuondoka kwake hapa Chuoni.

Kwanza, kuwasili kwake kuliwezesha kuanza rasmi kwa Somo la Kichina hapa Chuoni, ikiwa ni taasisi ya kwanza kufundisha somo hilo hapa Zanzibar. Tunafahamu kuwepo kwa Madarasa ya Confucius hapo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na katika Chuo Kikuu cha Taifa Dodoma hivi karibuni, lakini Chuo chetu ni dira na mfano kwa kutoa wahitimu wengi zaidi wa somo hilo hapa nchini.

Kuwepo kwa darasa la Confucius kwa ujumla+ wake kumekuwa na mafanikio makubwa si tu kwa kuendeleza darasa la Lugha ya Kichina na utamaduni, lakini pia taaluma nyengine zinazotolewa hapa Chuoni. CRI imekuwa ikitupatia vifaa vinatusaidia sana kwa kufundishia vijana wetu. Aidha, baadhi ya vifaa vinasaidia katika shughuli za utawala na hivyo kuongeza ufanisi wa kazi.

Pili, kuwepo kwake rasmi kumewezesha kushiriki ziara mbalimbali nje ya nchi zinazohusu maendeleo ya madarasa ya Confucius duniani ikiwemo ule wa Afrika ya Kusini na China Septemba na Disemba, 2013.

Tatu, kupatiwa fursa ya kujifunza nje ya nchi walimu watatu wa Chuo. Jitihada na msukumo wake katika suala hilo umefanikisha walimu watatu kupatiwa kozi za Shahada ya pili nchini China katika Miji ya Beijing na Shanghai, chini ya ufadhili wa Baraza la Ufadhili wa Masomo la China (China Scholarship Council).

Nne, kukipatia umaarufu Chuo. Bibi Khadija licha ya kuwa mwalimu anaefahamika sana hapa Zanzibar akiwa mahiri kwa kuzungumza Kiswahili, ameweza pia kukiwakilisha Chuo na kukitetea katika mikutano kadhaa na hivyo kukiwezesha kufikia katika hatua iliyopo hivi sasa. Mafanikio yanaonekana. Karibuni hivi, mwanafunzi mmoja wa Chuo chetu alichukuliwa na CRI nchini China kwa kazi maalumu na hivyo imeleta manufaa si kwa mlengwa, CRI au Chuo tu binafsi, bali kwa nchi nzima.

Ushirikiano wetu kwa ujumla umeleta mafanikio makubwa katika Nyanja zote.

Chuo kimefurahishwa na kuwepo kwake na kinatumai kuwa mrithi wake, Bwana Li Hong anaetarajiwa kuwasili karibuni ataweza kuiga mfano kwake kwa mema yote ambayo yanakubalika na Taifa na hata Chuo.

Aidha, Chuo kinaahidi kutoa ushirikiano kwa wageni wote wa CRI pamoja na walimu kikiamini kuwa hali hiyo ndio itakayodumisha maendeleo ya darasa.

Tunakuomba utufikishie salamu zetu kwa CRI na hasa Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili Bibi Han Mei kwa namna anavyoishirikisha Zanzibar katika mambo mbalimbali yanayohusu maendeleo ya redio hiyo. Chuo kinatamani sana iwapo siku moja Redio ya CRI itakubali wanafunzi wa Chuo hiki waitumie kuzalisha na kurikodi vipindi vitakavyorushwa hewani kama tutakavyoweza kukubaliana.

Tunaomba atufikishie ombi maalum kwa CRI na Serikali ya China kwa jumla kwamba Chuo kinathamini sana misaada inayotupatia kupitia Darasa la lugha ya Kichina, lakini kwa kuwa Chuo chetu kina ufinyu mkubwa wa fedha na bajeti kwa ujumla tunaomba CRI wafikirie kutanua maeneo mengine ya kutusaidia katika maeneo mengine kama vile ujenzi na vifaa vya studio kwa ajili ya maendeleo ya Chuo na kukuza ushirikiano zaidi baina ya China na Zanzibar.

Shukrani za ujumla ziwe kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa kuanzia na balozi zake zilizopo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukubali kuanzisha madarasa ya Confucius Tanzania hatua ya awali ikiwa hapa Zanzibar. Imani ya Chuo ni kuwa ushirikiano wa China, Zanzibar na Tanzania utaendelea kudumu huku ukinufaisha pande zote.

Mwisho, tunakuomba pia utukumbuke kwa kututetea katika masuala mbalimbali ambayo yanayonufaisha madarasa mengine ya Confucius ambapo Chuo chetu bado hakijanufaika nayo.

Nakutakia mafanikio ya kazi CRI, nikitumai kuwa tutakutana tena.
Karibu sana.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.