Habari za Punde

Majeruhi wa Ajali ya Gari Kaskazini Unguja.




Ajali mbaya yaua, yajeruhi


Khamisuu Abdalla na Kauthar Abdalla

WATU 21 wamejeruhiwa wengine hali zao zikiwa mbaya na mmoja kufariki dunia katika ajali mbaya iliyotokea jana asubuhi katika kijiji cha Mgambo, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Ajali hiyo ililihusisha gari la abiria linalofanya safari zake kati ya mjini na kijiji cha Mkokotoni na gari ndogo la kutembelea aina ya Noha.

Mashuhuda wa tukio hilo wamesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi, ambapo gari la abiria lilikuwa likifukuzana na gari jengine linalofanya safari zake kati ya mjini na Nungwi.

Baada ya kufika katika kijiji hicho dereva wa gari la Mkokotoni alishindwa kulidhibiti gari lake na kusababisha kugonga Noha na kupinduka.

Abiria aliefariki ni mtoto alietambuliwa kwa jina la Said Gharib (14) mkazi wa Gamba ambae alikuwa akisafiri pamoja na baba na mama yake kwenda mjini kwa ajili ya kutafutiwa nguo za sikukuu, huku hali ya mama yake ikiwa mbaya.

Miongoni mwa majeruhi hao 12 wametibiwa katika hospitali kuu ya Mnazimmoja na kuruhusiwa kurejea nyumbani huku tisa wamelazwa katika hospitali hiyo wakiendelea na matibabu.

Polisi waliosafiri na majeruhi hao walisema, miongoni mwa waliojeruhiwa ni abiria wawili na dereva wao waliokuwa wakisafiri kwa Noha na dereva wa gari ya abiria anashikiliwa na polisi kwa mahojiano.

Hiyo ni ajali ya tatu mbaya kutokea katika kipindi cha mfungo wa mwezi wa Ramadhan, ambapo ajali ya kwanza ilitokea katika eneo la Mwanakwerekwe wakati gari la jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lililobeba wanajeshi na raia waliokuwa wakienda kwenye mazishi ya wanajeshi waliouawa Darfur kupinduka na kujeruhi watu 24.

Ajali ya pili ilitokea Ijumaa, Julai 26 katika barabara ya Maisara baada ya gari ya abiria inayofanya safari kati ya mjini na uwanja wa ndege kupinduka na kujeruhi watu 11 na kufanya idadi ya majeruhi wa ajali zote kufikia 56.

1 comment:

  1. Inasikitisha kuona serekali zetu zinaendeshwa kienyeji kama hizi ajali zimekuwa ndio kila siku halafu tunasema zishandikwa basi zimeandikwa kwetu sisi wafririka tu ?au ni uzembe na dharau tulizo nazo ?

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.