Habari za Punde

Kamati za BLW kuanza kazi wiki ijayo

Na Himid Choko, BLW
KATIBU  wa Baraza la Wawakilishi  la Zanzibar ndugu Yahya Khamis Hamadi amewahimiza  Watendaji wa Mawizara na taasisi wanazoziongoza  kutoa mashirikiano ya kutosha kwa Kamati za Kudumu za Baraza hilo  zinazotarajiwa kuendelea tena na kazi zake za kawaida wiki ijayo.
Amesema  Shughuli zote za umma  zinafanywa kwa niaba na maslahi  ya wananchi, na wananchi kupitia Wawakilishi wao kwenye Baraza la Wawakilishi wanahaki ya kujua namna halisi yab serikali yao inavyotenda haki hizo.
Amesema   kwa mantiki hiyo watendaji hao  wana jukumu la kutoa mashirikiano na  taarifa sahihi  juu ya mambo  wanayoyashughulikia  katika utumishi wote wa umma ili kuwawezesha  wananchi kupitia wawakilishi wao  kujua mambo yanayofanywa kwenye   Mawizara  ya serikali kwa maslahi yao.
“ Napenda kuwasisitiza tena watendaji wote wa Mawizara na Taasisi zao, kuzipa ushirikiano Kamati hizo kwa muda wote zitakapokua katika taasisi zao  pamoja na kuzipatia taarifa sahihi  kwa dhana ile ile ya kuendeleza uwazi na uwajibikaji’ Alisisitiza  Katibu Yahya.
Amesema hiyo ndio dhana kubwa  inayojenga wajibu wa Serikali na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuhusiana na haki za Kamati.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari  ndugu Yahya amesema Kamati  hizo za Kudumu za Baraza la Wawakilishi zitaendelea na kazi zake za kawaida kuanzia Septemba  9  hadi Septemba  20, 2013.
 Amesema pamoja na Kufuatilia  Utendaji wa  Kila Wizara na taasisi zake Kamati hizo pia zitapokea taarifa ya utekelezaji wa Maagizo yaliyotolewa na Baraza kupitia  Ripoti za Kamati za Mwaka 2012/2013.
Amesema ingawa Kanuni ya 108 (15)  inaweka masharti kwa kila Wizara kuwasilisha   mbele ya Baraza , Ripoti ya utekelezaji wa maagizo ya Kamati za Kudumu za Baraza katika kila Mkutano wa mwezi wa Machi ya kila mwaka lakini pia Kamati zinawajibu wa   kufuatilia zaidi utekelezaji wa maagizo hayo kwa kujiridhisha.
  Amesema  Kamati  ya Kuchunguza  na Kudhibiti  Hesabu za Serikali na Mashirika  (PAC), Kamati ya Fedha , Biashara na Kilimo na  Kamati ya Ujenzi na Mawasiliano  zitafanyakazi zake  Unguja.
Amezitaja  Kamati nyengine zitakazofanyakazi Unguja kua ni Kamati ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii pamoja na  Kamati ya Mifugo, Utalii , Uwezeshaji  na Habari.
Ndugu Yahya amesema Kamati ya Kusimamia Afisi za  Viongozi Wakuu wa Kitaifa  itafanyakazi huko Dar es Salaam  wakati Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala itakwenda huko Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.