Habari za Punde

Hakuna umeme wa bure - Serikali

JIBU LA SWALI LA MBUNGE Baraza la wawakilishi
 
NAIBU Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, ameliambia Bunge kuwa hakuna mtu nchini anayetumia umeme wa bure na badala yake kila mtu anatakiwa kulipia ikiwemo serikali yenyewe.
 
Simbachawene alisema mpango wa kutumia umeme wa bure haupo na haiwezekani kufanya hivyo kutokana na ukweli kuwa gharama za kuzalisha umeme ni kubwa na ambazo zinahitaji kuchangiwa.
 
Alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, Jaku Hashimu Ayoub (CCM), aliyetaka kujua kama umeme unaopelekwa Zanzibar kutoka Tanzania Bara ni wa kununua au ni wa bure.
 
Katika swali la msingi, mbunge huyo alitaka kujua namna ambavyo Zanzibar inanufaika na gesi ambayo inavunwa Tanzania Bara kwa kuwa suala la mafuta ni la Mungano.
 
Mbunge huyo pia alihoji ni lini kilio cha wananchi wa Zanzibar cha kutaka suala la mafuta na gesi liondolewe katika mambo ya Muungano kitasilizwa.
 
Naibu Waziri alisema mapato yote yatokanayo na gesi asilia pamoja na vyanzo vingine huingizwa katika mfuko mkuu wa mapato wa serikali ambayo ni Hazina ambako Zanzibar inapata mgawo wake kupitia mfuko huo.
 
“Aidha sehemu kubwa ya gesi asilia ambayo huzalishwa kutoka Songosongo hutumika kufua umeme unaoingizwa katika gridi ya taifa na Zanzibar hunufaika na umeme unaosafirishwa kupitia Submarine Cable iendayo huko,” alisema Simbachawene.
 
Kuhusu suala la kuondoa mafuta katika orodha ya mambo ya Muungano, alisema jambo hilo lipo kwa kamati maalumu chini ya wanasheria wa pande mbili ambao wanajaribu kulipitia kitaalamu kwanza.
 
Chanzo - Tanzania Daima

1 comment:

  1. huko bara sijui vipi lakini Zanzibar wafanyakazi tu wa shirika la umeme hawalipi kitu (ni sheria kabisa) na wala sifikirii kama mawaziri znz wanalipia umeme, haya ni mambo ya kijinga mijitu inalipwa mishahara minono, marupurupu na uhakika umeme wanalipiwa na masikini za Mungu

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.