STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 08 Oktoba , 2013
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa ni wakati muafaka sasa kuandaa mazingira bora zaidi yatakayowezesha kuimarisha ushirikiano wa kihistoria kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Shirikisho la Urusi.
Dk. Shein ameueleza uhusiano kati ya pande mbili hizo kuwa ni wa kipekee kutokana na kitendo cha Urusi wakati huo ikilijulikana kuwa Shrikisho la nchi za Kisoshalisti za Kisovieti kuwa nchi ya kwanza kuyatambua Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika tarehe 12 Januari, 1964.
“uhusiano na ushirikiano wetu mara baada ya Mapinduzi ulikuwa wa karibu sana na ulidhihirika pale Russia ilipokuwa nchi ya kwanza kuyaunga mkono na kuyatambua Mapinduzi ya Zanzibar”alieleza Dk. Shein.
Akizungumza na Balozi wa Shirikisho la Russia bwana Alexander Rannikh ofisini kwake Ikulu leo Rais ameeleza kuwa Russia mbali ya kuyatambua Mapinduzi lakini iliisadia Zanzibar kujiimarisha kwa kuipatia wataalamu katika nyanja mbalimbali pamoja na kutoa fursa za masomo kwa vijana wa Zanzibar.
“Mara baada ya Mapinduzi Russia sio tu ilileta wataalamu wa fani mbalimbali kuja kusaidia maendeleo ya Zanzibar lakini pia ilitoa nafasi nyingi za masomo kwa vijana nikiwemo mimi mwenyewe”alieleza Dk. Shein.
Kwa hiyo alisema ni wakati muafaka sasa kupanua maeneo mapya ya ushrikiano kati ya Zanzibar na Shirikisho la Russia ikiwemo uwekezaji na biashara, viwanda na utalii.
“Urusi ni moja ya nchi zinazotoa watalii wengi ulimwenguni hivyo ni eneo ambalo ikiwa tutashirikiana linaweza kutupa mafanikio makubwa”alieleza Dk. Shein na kuongeza kuwa ni vyema mamlaka zenye kushughulikia sekta hizo kukutana na kuzungumza namna ya kushirikiana.
Kwa upande wake Balozi Alexander Rannikh alimueleza Mheshimiwa Rais kuwa nchi yake ingependa kuona ushirikiano wake na Zanzibar unaimarika na kueleza suala la ushirikiano katika biashara ya utalii ni jambo jema na linawezekana kutekelezwa.
“Tuna makampuni mengi makubwa ya kitalii nchini kwetu hivyo kinachatakiwa ni kuyahamasisha kwa kuyapatia taarifa muhimu kuhusu sekta ya utalii hapa Zanzibar”alisema Balozi Alexander ambaye alidokeza kuwa baadhi ya makampuni hayo yameonyesha nia ya kuja Zanzibar.
Alibainisha kuwa kwa wananchi wengi wa Urusi wanaobahatika kutembelea Zanzibar na wale ambao wanaishi nchini wanafurahishwa kuona wazanzibari wengi wanaozungumza lugha ya kirusi.
Katika mazungumzo hayo Balozi huyo alieleza pia dhamira ya Serikali ya nchi yake kuifungua tena Ofisi ya Ubalozi mdogo wa nchi yake hapa Zanzibar kwa kueleza kuwa hatua hiyo itakuwa muhimu sio tu katika kuimarisha ushirikiano na Serikali na Zanzibar bali pia uhusiano na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822
No comments:
Post a Comment