Habari za Punde

DK. SHEIN: ELIMISHENI WANANCHI JUU YA PROGRAMU ZA MAENDELEO NA CHANGAMOTO ZAKE


STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                                      11 Oktoba, 2013
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Wizara, Idara na Taasisi za Serikali zimetakiwa kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utekelezaji wa programu mbalimbali ikiwemo changamoto zinazozikabili katika utekelezaji wa programu hizo.
Wito huo umetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein wakati wa kikao cha kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpangokazi wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati ya mwaka wa fedha 2012/2013 na robo ya kwanza ya mwaka wa fedha wa mwaka 2013/2014  
Mheshimiwa Rais amebainisha kuwa wakati jitihada nyingi zinafanyika katika kuongeza kiwango cha utoaji huduma mbalimbali kwa wananchi kukosekana kwa elimu ya mara kwa mara kunawafanya baadhi ya wananchi kuendelea kulalamika.
Akitolea mfano sekta ya maji alisema “wananchi lazima waelezwe upungufu huo wa maji chanzo chake ni nini na ni hatua gani Serikali imekuwa ikichukua kukabiliana na upungufu huo” na kuongeza kuwa elimu hiyo itolewe kwa lugha nyepesi ambayo kila mwananchi ataufahamu ujumbe wake.
Alisisitiza kuwa ni vyema wananchi wakaelezwa kinagaubaga hatua zilizofikiwa katika miradi ya maji na matarajio yake ya kumalizika na huduma ya maji kupatikana kwa uhakika.
Kwa upande wa suala la upimaji ardhi kinyume na sheria Dk. Shein aliitaka Wizara iwaelimishe wananchi umuhimu wa kufuata taratibu zilizowekwa za upimaji ardhi pamoja na madhara yanayoweza kuyapa wanapofanya kinyume na hivyo.

“Tutoe elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kufuata taratibu za upimaji ardhi na hata kuwapa tahadhari ya madhara yanayoweza kuwapata watakapokiuka taratibu zilizowekwa” Dk. Shein alieleza.
Dk. Shein aliipongeza Wizara hiyo kwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi katika mwaka wa fedha uliomalizika na kuwataka watumishi wa wizara hiyo kuimarisha utendajikazi wa pamoja (Team work).
Amewakumbusha kuwa jukumu la Serikali ni kuwatumikia wananchi hivyo hawana budi kutekeleza wajibu wao kwa kutoa huduma bora na kwa wakati ili kukidhi matarajio ya wananchi.   
Wakati huo huo huo Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Ramadhani Abdalla Shaaban amesema Wizara yake hivi sasa imeelekeza nguvu zake zaidi katika kutatua tatizo la maji nchini.
“Baada ya tatizo la kupatikana umeme kumalizika wizara yangu hivi sasa imejikita katika kushughulikia suala la maji ambapo tunatarajia ifikapo Septemba mwaka 2014 tuwe tumepiga hatua kubwa” Waziri alikiambia kikao hicho.
Kwa upande wa umeme Waziri alieleza kuwa kufuatia kukamilika mradi wa uwekaji wa laini ya pili ya umeme wenye uwezo wa MW 100 Wizara hiyo imeweka mkazo katika kuimarisha miundombinu ya umeme pamoja na kuusambaza vijijini.
Halikadhalika Waziri alibainisha kuwa kwa kushirikiana na Jumuiya ya Nchi za Ulaya(EU) wizara imeendelea kufanya utafiti wa nishati mbadala nchini.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Shariff Hamad  na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.    

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.