JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA MABADILIKO
YA KATIBA
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Alhamisi, Novemba
7, 2013
Tume ya Mabadiliko
ya Katiba inapenda kuwafahamisha wananchi kuwa Mjumbe wake Dkt. Sengondo Mvungi
aliyekuwa akipata matibabu katika Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI)
amesafirishwa leo (Alhamisi, Novemba 7, 2013) saa 5:45 asubuhi kwenda nchini
Afrika Kusini kwa uchunguzi na matibabu zaidi.
Akiwa nchini
Afrika Kusini, Dkt. Mvungi atapata matibabu katika Hospital ya Milpark iliyopo
jijini Johannesburg .
Itakumbukwa kuwa
Dkt. Mvungi alivamiwa nyumbani kwake Kibamba, wilaya ya Kinondoni jijini Dar es
Salaam na watu waliomjeruhi vibaya kichwani usiku wa kuamkia siku ya Jumapili,
Novemba 3, 2013. Tukio hilo
la uvamizi linaendelea kuchunguzwa na vyombo vya ulinzi na usalama nchini.
Tangu siku
alipojeruhiwa, Dkt. Mvungi alikuwa akipata matibabu katika Kitengo cha Mifupa
Muhimbili (MOI). Hata hivyo, Madaktari waliokuwa wakimtibu MOI, walishauri
afanyiwe uchunguzi na matibabu zaidi.
Dkt. Mvungi
ameondoka na ndege ya kukodi ya Shirika la Ndege la Flightlink na ameambatana
na Dkt. Mugisha Clement Mazoko kutoka MOI; Muuguzi Bi. Juliana Moshi; na mtoto
wa kaka yake Bw. Deogratias Mwarabu. Serikali inagharamia gharama zote za
matibabu ya Dkt. Mvungi.
Tume inawaomba
wananchi wote waendelee kumuombea kwa Mungu Dkt. Mvungi ili aweze kurejea
katika hali yake ya kawaida na hatimaye kuendelea majukumu yake.
Mwisho.
Imetolewa
na:
Ndg. Assaa
A. Rashid,
Katibu,
Tume ya
Mabadiliko ya Katiba,
Alhamisi,
Novemba 7, 2013
0757 –
500800 / 0714 662482 / 0717 084 252 /
No comments:
Post a Comment