Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi-Zanzibar
Shirikisho la Polisi wa Kimataifa Duniani INTERPOL, limeahidi kutoa msaada wa miundombinu ya kiuchumi na vitendea kazi kwa wataalam wa vyombo vya Ulinzi na Usalama Barani Afrika kukabiliana na Uharamia katika Pwani za Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu.
Ahadi hiyo imetolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Usalama Majini wa Makao Makuu ya INTERPOL Lyon nchini Ufaransa, St. Hilaire Pierre, wakati wa mkutano wa Makachero Waandamizi na Wataalamu wa Sheria wakiwemo Waendesha Mashtaka kutoka nchi za Kenya, Shelisheli, Somalia na wenyeji Tanzania unaofanyika mjini Zanzibar.
‘Kwa kutambua kuwa nchi za Kiafrika zinakabiliwa na uhaba wa kifedha na wataalamu wa kutosha katika mifumo mbalimbali ya kiutendaji, INTERPOL itatoa kila aina ya misaada ili kuhakikisha kuwa suala la Uharamia linakomeshwa.’ Alisema St. Pierre.
Amesema nia ya mpango huo ni kuhakikisha kuwa meli zote za mizigo zinazofanya safari kutoka bara ama taifa moja na lingine inasafiri salama bila ya kuwepo hofu ya kuvamiwa na kuporwa mali ama kutekwa kwa mabaharia.
Aidha imependekezwa kuwa, ili chombo hicho kiweze kufanya kazi vizuri, kila nchi mwanachama itoe wataalam kutoka katika taasisi za Polisi, Wanasheria wakiwemoi waendesha mashtaka maahakamani pamoja na wasimamizi wa vyombo vya usafiri majini na kuingia katika timu hiyo.
Aidha Maafisa hao pia wamekubaliana kuwa lugha ya kiingereza na kiswahili zitumike katika wa operesheni na upelelezi dhidi ya wahalifu wa matukio ya uharamia katika ukanda huu wa pwani za Bahari ya Hindi na Mwambao mwa Maziwa Makuu .
Akiiwakilisha nchi ya Kenya katika Mkutano huo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi kutoka nchini Kenya SSP. Moses Barngetuny, amesema kuwa Lugha ya kiswahili inazungumzwa na kusikika katika mataifa mengi ya ndani na nje ya Bara la Afrika.
Naye mwakilishi wa Tanzania katika Mkutano huo ambaye pia ni Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Kikosi cha Wanamaji na Bandari nchini Tanzania Kamishna Msaidizi, ACP Basil Pandisha, alisema kuwa moja ya juhudi zilizochukuliwa na Jeshi la Polisi nchini Tanzania ni pamoja na kuanzisha Idara ya Upelelezi katika Kikosi cha Polisi Wanamaji na bandari idara ambayo inashughulikia kesi za Uharamia na kwamba kwa INTERPOL kukubali kusaidia mpango wa Operesheni ni wamanufaa kwa nchi masikini.
Akizungumzia uharamia katika pwani za Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu, Kamishna Pandisha amesema kuwa chanzo vitendo vya uharamia ni umaskini wa kipato unaoikabili nchi ya Somalia na kwamba baada ya kujaribu mpango wa uvamizi wa meli na kufanikiwa, sasa umegeuzwa kama mradi wa kiuchumi.
Ameyataka Mataifa makubwa kiuchumi kuangalia namna ya kutibu tatizo la uharamia kwa kuangalia chanzo cha tatizo badala ya kutumia nguvu kubwa za kimapambano ya silaha.
No comments:
Post a Comment