Habari za Punde

Rais wa Zanzibar Dkt Shein, Asisitiza Kuzingatia Vipaumbele katika Mipango ya Maendeleo

STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                                     10 Oktoba, 2013
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza umuhimu wa Wizara na Idara za Serikali kuzingatia vipaumbele katika kupanga mipango ya maendeleo ya kila mwaka.
Dk. Shein alieleza hayo jana wakati akihitimisha Taarifa ya Thathimini ya Utekelezaji Kazi ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2012- 2013 na robo mwaka ya mwaka wa fedha 2013-2014 katika mkutano uliofanyika Ikulu.
Katika maelezo yake kwa uongozi wa Wizara hiyo Dk. Shein alibainisha kuwa lengo la mikutano hiyo ni kufanya tathmini ya namna Serikali inavyotekeleza majukumu iliyojipangia kwa minajili ya kuzingatia na kuangalia utekelezaji wa bajeti na malengo yaliyowekwa.
“Dhamira yetu ni kujitathmini sisi wenyewe namna tunavyopanga na kutekeleza malengo tuliyojiwekea kwa kuangalia uwiano kati ya kiwango cha fedha kinachotolewa katika bajeti na kiwango cha utekelezaji wa malengo ya Wizara na idara zake”Dk. Shein alifafanua.
Kwa hiyo alisisitiza umakini katika kuainisha na kupanga vipaumbele katika kila idara katika wizara ili kurahisisha utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa malengo ya mipango ya Serikali huku dhamira kuu ikiwa ni kuongeza ufanisi na tija katika utendaji Serikalini.
Mheshimiwa Rais ameipongeza Wizara ya Afya kwa kukamilisha taarifa hizo mbili za Utekelezaji kazi za Wizara ambazo zimeonyesha kwa mara ya kwanza mbali ya idara na taasisi zake lakini pia shughuli za Wizara hiyo katika kila wilaya za Unguja na Pemba.
Halikadhalika aliipongeza wizara kwa kuandaa kambi za matibabu ya macho ambazo zimeonyesha matokeo mazuri na kuwasaidia wananchi wengi nchini.
“suala la kambi za matibabu ya macho linahitaji kuwekewa mipango mizuri zaidi ili zizidi kuwasaidia wananchi wengi na kwa matokeo mazuri mliyoyapata tunahitaji kuliendeleza” alieleza Dk. Shein na kuongeza kuwa kambi hizo ziwe sehemu ya maandalizi ya Serikali kuacha kupelekea wagonjwa wa macho nje ya nchi.

Akizungumzia kuhusu huduma za upimaji wa macho kwa watoto Dk. Shein aliitaka wizara kuweka mipango madhubuti ya namna ya kuwasaidia watoto ambao wanagundulika na matatizo ya macho lakini wazazi wao hawana uwezo wa kugharimia matibabu.
Alisifu mafanikio ya kitengo cha benki ya damu kwa kutimiza malengo ya mwaka uliopita kwa zaidi ya asilimia mia moja lakini akahimiza kitego hicho kujiwekea lengo la kujitegemea katika shughuli zake.
“Lengo letu liwe ni kujitegemea katika kuendesha benki ya damu na kwa kuanzia mwaka ujao wa fedha kiwango cha fedha katika bajeti ya kitengo hicho kiongezwe hatua kwa hatua hadi kufikia kujitegemea kwa asilimia mia moja” Dk. Shein aliekeleza.
Katika maelezo yake hayo Mheshimiwa Rais alizungumzia pia umuhimu wa uwekaji wa takwimu sahihi katika sekta ya afya huku akihimiza ushirikiano wa karibu kati ya sekta ya umma na binafsi katika suala hilo.
“Ili kupata takwimu sahihi kitaifa hasa wakati wa magonjwa ya miripuko ni muhimu kuwepo na ushirikiano wa karibu kati ya sekta ya umma na binafsi” alisisitiza Dk. Shein.
Wakati huo huo Waziri wa Afya Mheshimiwa Juma Duni Haji alikieleza kikao hicho kuwa huduma za afya nchini zinazidi kuimairika kutokana na Serikali wakati wote kuwa sikivu kwa masuala ya afya.
Akizungumza kabla kumkaribisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuwasilisha taarifa ya utekelezaji Mheshimiwa Duni alisema maoni ya wananchi ni kuwa huduma katika sekta ya afya nchi zinazidi kuimarika pamoja na changamoto zilizopo.
Alieleza kuwa Wizara yake hivi sasa inakabiliana na tatizo la ongezeko la maombi kutoka kwa watumishi wa wizara hiyo kutaka kujiendeleza kimasomo ikiwemo kozi mapya ya udaktari yaliyoanzishwa katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar –SUZA.
Alieleza kuwa kitendo cha watumishi wengi kutaka kujiunga na masomo ya juu ni hatua nzuri lakini inasababisha uhaba wa watumishi. Alieleza kuwa maslahi mazuri kwa watumishi wa afya hivi sasa yanavutia watumishi wengi wa wizara yake kutaka kujiendeleza kimasomo. 
Akiwasilisha taarifa ya Wizara hiyo Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dk. Saleh Jidawi alileleza kuwa katika mwaka wa fedha uliopita jumla ya wagonjwa wa macho 10,558 walichunguzwa na kupatiwa matibabu katika vituo vya afya 32 na vijiji 26 Unguja na Pemba.
Sambamba na hatua hiyo Wizara kwa kushirikiana na mashirika ya Lions Club ya Mzizima na Bilal Muslim Mission zote za Dar es Salaam iliandaa kambi kubwa ya ya uchunguzi na matibabu ya macho ikiwemo kuwafanyia operesheni kwa wale waliohitaji matibabu ya aina hiyo.
Vile vile aliongeza kuwa uchunguzi wa macho ulifanyika katika skuli 26 Unguja na Pemba ambapo watoto 867 walipimwa macho miongoni mwao 278 walipatiwa miwani kwa kushirikiana na kitengo cha Elimu Mjumuisho cha Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.
Kwa upande wa Mpango wa Damu Salama Dk. Jidawi alieleza kuwa Mpango huo uliweza kufikia lengo mwaka uliopita kwa asilimia 110 kutoka lengo la kukusanya damu lita 8,000 hadi lita 8,808.
Alisema hatua hiyo mbali ya kuwa ni mafanikio makubwa kwa kuvuka lengo bali iliiweza Serikali kukidhi mahitaji ya damu kwa hospitali zote zinazotoa huduma ya hiyo nchini.
Akizungumza katika kikao hicho Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulahamid Yahya Mzee alisema kuwa watendaji wa Serikali bado wanayo fursa ya kujifunza zaidi uandaaji wa mipango ya kazi yenye malengo yanayopimika kwa urahisi kwa kuzingatia vigezo vya uwekaji malengo walivyoelekezwa.
Akizungumzia mafanikio ya matibabu ya macho yakiwemo ya upasuaji hapa Zanzibar Dk. Abdulhamid ameitaka wizara kuwaelimisha wananchi juu ya uwezo wake wa kutibu magonjwa hayo ikiwemo kufanya operesheni ili wagonjwa waachane na dhana ya kwenda kutibiwa nje kwa gharama kubwa.
“Tangazeni sana mafanikio ya operesheni za macho mnazofanya hapa ikiwemo kwa kuwatumia wagonjwa ambao wamepata matibabu hayo ili wengine  wajenge imani kuwa mnao uwezo huo”alieleza Dk. Abdulahamid.    

                                         

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.