Habari za Punde

Wavunja amani wasionewe aibu Zanzibar

Na Salim Said Salim
 
SIKU moja wakati nipo shule, nakumbuka mwalimu wetu mmoja alituambia kuwa sio vibaya mtu kuwa jeuri na kupenda kutamka matusi ya aina yoyote ile. Hiyo ni haki yake na hakuna mtu anayeweza kukuingilia kati.
 
Karibu wanafunzi wote tulimshangaa mwalimu na kumuona mtu wa ajabu sana, na hatukujua alikuwa na lengo gani hata akatueleza hayo.
Wakati baadhi yetu tukiwa tumenyoosha mkono kwa wengine kutaka kupingana na kauli yake na wengine kutaka ufafanuzi, mwalimu alitutaka tusubiri kidogo.
“Msiwe na papara kama kifaranga kinachotaka kutoka kwenye yai,” alitueleza na kutuacha wengine tukicheka.
Mara tu baada ya kuteremsha mikono yetu chini, mwalimu alituambia kwamba kilicho muhimu ni pale unapotaka kuonyesha jeuri au kuropoka au matusi, ni lazima kwanza uhakikishe unafanya hivyo ukiwa chumbani au chooni peke yako na hakuna mtu anayekuona wala kukusikia ukifanya hivyo.

Baada ya ufafanuzi huo, sote tulielewa alichokusudia mwalimu na kubaki tunacheka.
Tukio hili kwangu mimi na wenzangu ambao baadhi yao kila tunapokutana zaidi ya nusu karne tokea mwalimu yule atueleze hivyo hukumbushana, lilikuwa somo la aina yake nililolipata enzi ya udogo wangu.
Kwa muhtasari na kutoifanya hadithi kuwa ndefu, mwalimu alikuwa anatupa wasia juu ya umuhimu wa mtu kutofanya jeuri au kutoa matusi, iwe ya mdomoni, mkononi au nguoni mbele ya watu wengine.
Kinachonisikitisha ni kuwa hivi karibuni nimeona baadhi ya watu, wengine walionizidi umri na walikuwa walimu pale mwalimu mwenzao alipotupa wasia ule, wamejitokeza kuwa na ujeuri, kibri na kejeli zinazoambatana na matusi ya nguoni mbele ya kadamnasi (jamii).
Baya zaidi na ambalo kwa kawaida huwezi kulitegemea ni kuwa wengine wanaofanya hivi ni masheikh wanaoheshimika katika jamii ya watu wa Visiwani, wakiwemo wale ambao huongoza wengine katika sala ya Ijumaa ambayo inao utukufu mkubwa kwa waumini wa dini hii.
 
 Kwa muda mrefu watu hawa wamekuwa wakinyamaziwa, labda kwa sababu ya kile kinachoitwa ‘Visiwani wenzetu’ au kuheshimu huo unaorembwa na kuelezwa kama utumishi wao uliotukuka katika serikali miaka iliyopita.
Katika jeuri yao hii waliyoifanya hadharani na sio chooni, watu hawa wametaka Wapemba waliopo Unguja “wahame waende kwao”.
 
Kwa maana hiyo hata baadhi ya viongozi wa juu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wanatakiwa wafunge virago vyao na kwenda katika vijiji vyao vya Chokocho, Mtambwe, Jambangome na Mtu Haliwa kisiwani Pemba.
Vile vile wametaka visiwa hivi vigawanyike pande mbili kwa kila upande kuwa na lake. Wengine walifika mbali zaidi kwa kuwatukana Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na Makamu wake wa Kwanza, Maalim Seif Sharif Hamad.
Sijui watu hawa wanajiamini kwa kiasi gani na nini hasa lengo lao la kufanya hivi.
Watu wengi walishangaa kuona wamenyamaziwa kimya na kubaki kuulizana kwanini watu hawa hawaguswi au walichokifanya ni kitu kizuri na kinakubalika katika jamii?
Nimewahi kusikia watu katika baraza la kahawa wakisema watu hawa wanastahiki kupewa nishani kwa uadilifu wao wa kukashifu na kutukana watu!
Lakini hatimaye kama wasemavyo Waswahili kimya kingi kina mshindo mkubwa. Hivi sasa makachero wa Jeshi la Polisi ambalo katika siku za hivi karibuni limekuwa likionyesha uvumilivu wa hali ya juu, limeamua kutumia ipasavyo mamlaka iliyopewa kisheria kama mlinzi mkuu wa usalama wa raia na mali zao.
Polisi hivi sasa wamekuwa wakiwahoji wale wote waliosemekana kuwa vinara wa makongamano yanayofanyika hivi sasa ya hao wanaoitwa wastaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Polisi, Vikosi vya SMZ, wakulima na wafanyakazi wa idara na wizara za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar waliotoaa matamshi hayo.
Hapa inafaa kulipongeza Jeshi la Polisi kwa kuchukua hatua hii muafaka kwa sababu hakuna maelezo yoyote unayoweza kuyatoa kwa matamshi ya hadharani ya aina hii isipokuwa ni kutoitakia mema Tanzania, na hasa Zanzibar ambayo imeanza kupumua baada ya mtafaruku mkubwa wa kisiasa uliozaa siasa za chuki na uhasama kwa miaka mingi.
Hapa inafaa kukumbushana kuwa matamshi kama haya ya kuchochea chuki na uhasama ndiyo yaliyosababisha watu kuuawa na wengi kuwa vilema, vizuka na yatima.
Kama alivyotamka mara nyingi Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete, hotuba za chuki na uhasama ziwe katika majukwaa ya kisiasa au maeneo ya ibada ni za hatari na hazifai hata kidogo kuvumiliwa na Watanzania.
Mtu yeyote anayetaka kuwagawa Watanzania kama mafungu ya nyanya kwa misingi ya maeneo, dini, kabila au itikadi za kisiasa anapaswa kulaaniwa na Watanzania wote.
Lakini muhimu zaidi ni kwa watu wanaopalilia siasa za chuki wasiachiwe kutamba kama vile wanavyofanya ni jambo zuri. Mkondo wa sheria lazima uruhusiwe kuchukua nafasi yake bila ya kuoneana haya kwani vinginevyo nchi hii inaweza kujikuta katika mtafaruku mkubwa kuliko tunayoiona katika nchi za jirani ambako tunapeleka askari wetu na wengine hata kupoteza maisha yao ili hawa wenzetu waishi katika usalama na amani.
Lakini wakati tunasaidia kwa kutoa roho zetu na mali kujenga kwa wenzetu, hapa kwetu wapo watu ambao kwa sababu zao mbalimbali za kibinafsi, kama kunyimwa vyeo serikalini, wameamua kubomoa nyumba yetu.
Masikini watu hawa, wanafikiri kukosa madaraka ni kudhulumiwa badala ya kuelewa kwamba kama hilo ni jukumu ambalo kila mmoja anayo haki ya kupewa, lakini asifanye nongwa akikosa kukabidhiwa.
Watu hawa na mwengine bila ya kujali kama ni mwanasiasa, mstaafu anayetembelea mkongojo au kiongozi wa dini, hapaswi kuonewa muhali au kuvumiliwa.
Kama yeye hakuona haya wala vibaya kuchochea watu, kwanini wengine wamfumbie macho kwa matamshi machafu anayoyatoa?
Hatukatai kwamba tumeamua kujenga nchi ya kidemokrasia ambayo watu wake watakuwa na uhuru wa kujieleza na kutoa maoni, lakini hayo maoni lazima yawe ya kujenga na kuleta maelewano katika nchi sio kubomoa na yasiwe na ishara yoyote ya uchochezi au kuhatarisha amani ya nchi.
Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alijitahidi sana kuhakikisha kwamba nchi hii inatawalika kwa amani na sio kwa matusi, jeuri, kejeli, vitisho au mtutu wa bunduki na kwa kiasi kikubwa waliovaa viatu vyake katika awamu tofauti, Bara na Visiwani, wamejitahidi kufanya hivyo ijapokuwa kwa mtazamo wa wengine pamekuwepo na dosari za hapa na pale.
Hivi sasa nchi yetu inakabiliwa na changamoto nyingi za ujambazi, mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, wengine wakifanyiwa unyama huu wakiwa majumbani kwao.
Hali hii tuliyonayo hivi sasa tayari imezusha hofu kubwa katika jamii na watu kujiuliza Tanzania inaelekea wapi?
Ni vizuri kwa Jeshi la Polisi kukaza kamba na kutoruhusu mwenendo huu unaoweza kuipeleka nchi pabaya. Asiyetaka kusakamwa na polisi kwa matamshi hatarishi anayotoa mdomoni, njia ya usalama ni kucha kutamka maneno ya ovyo yenye lengo la kuchochea chuki na uhasama

Chanzo - Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.