HOJA YA MJUMBE WA BARAZA LA WAWAKILISHI LA
ZANZIBAR KULIOMBA BARAZA LA WAWAKILISHI LA ZANZIBAR KUTOA MAAZIMIO DHIDI YA
VITENDO VYA UDHALILISHAJI WA WATOTO ZANZIBAR (CHINI YA KANUNI YA 27(1) (n),
27(3), 49(1), 50 YA KANUNI A BARAZA LA
WAWAKILISHI, TOLEO LA 2012)
MAELEZO YA
HOJA
KWA KUWA, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa na
dhamira ya dhati ya kuwalinda watoto wa Zanzibar kwa kuchukua hatua mbali mbali ikiwemo ya
kuwa na Sheria namba 6 ya 2011na kuhakikisha kupatikana kwa haki zao ikiwa ni pamoja na kuwapatia elimu
bora, makaazi, mavazi, chakula na
kuwalinda dhidi ya aina zote za udhalilishaji.
NA KWA KUWA, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeridhia
mikataba inayohusiana na haki za watoto duniani, ambayo Zanzibar inahusika katika utekelezaji wa mikataba hiyo
ili kuona azma ya kuwalinda watoto inafikiwa.
NA KWA KUWA, Kumekuwepo na ongezeko kubwa la kesi za
udhallilishaji wa watoto, ikiwa ni pamoja na kesi za ubakaji na ulawiti hapa
nchini
NA KWA KUWA kwa mujibu wa takwimu za Mahakama Kuu ya
Zanzibar inaonesha kuwa katika mwaka wa 2010 kesi zipatazo 48 zilifunguliwa,
ambapo kesi 35 zilitolewa maamuzi, kesi
13 zinaendelea kusikilizwa, na katika kesi zilizotolewa maamuzi ni kesi 2 tu
ambazo washtakiwa wake walipatikana na hatia na kuhukumiwa adhabu ya kifungo na
7 kulipa faini na kesi 28 washtakiwa wake wameachiwa huru;
NA KWA KUWA, Kwa mwaka 2011 kesi 74 zilifunguliwa
ambapo ni pamoja na kesi 18 za kuingiliwa kinyume na maumbile na kesi 56 za
ubakaji, kesi zinazoendelea ni 38 na
kesi 36 zimetolewa maamuzi na kati ya hizo zilizotolewa maamuzi ni kesi 2 tu
ambazo washtakiwa wake walitiwa hatiani na kupewa adhabu ya kifungo na 2 kulipa
faini, na kesi 32 washtakiwa wake wameachiwa huru;
NA KWA KUWA, Kwa mwaka 2012 kesi 72 zilifunguliwa zinazojumuisha
kesi 10 za kuingilia kinyume cha maumbile, na kesi 62 za ubakaji ambapo kesi 61 zinaendelea kusikilizwa, na kesi 11
zimetolewa maamuzi ambapo kati ya hizo kesi 2 washtakiwa wake wametiwa hatiani
na kupewa adhabu na 1 kulipa faini, na kesi 8 washtakiwa wake wameachiwa huru;
NA KWAKUWA kwa mujibu wa takwimu za tafiti
zilizofanywa na taasisi mbali mbali zikiwemo asasi za kiraia zinaonyesha kuwa
kesi nyingi zaidi zimekuwa zikiriporipotiwa polisi lakini zimeshindwa
kufikishwa mahakamani kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo ya kukosekana
ushahidi;
NA KWAKUWA , mbali na takwimu za mahakama kutoonesha
hali halisi ya matukio mengi ya udhalilishaji wa watoto hapa Zanzibar, bado
inaonyesha kuwa tatizo hilo ni kubwa sana nchini.
NA KWA KUWA , kesi nyingi zinazofikishwa mahakamani
zimeshindwa kuthibitishwa kutokana na sababu mbali mbali na hivyo kupelekea
washitakiwa wengi kuachiwa huru na hatimae kupelekea kuongezeka kwa vitendo
hivyo vya udhalilishaji kwa watoto wetu.
NA KWA KUWA, Serikali inapaswa kuchukua hatua
madhubuti ili kuwalinda watoto hao dhidi ya udhalilishaji na pale inapotokea
watoto hao kufanyiwa vitendo hivyo vya udhalilishaji, kuhakikisha wahusika wa
vitendo hivyo wanachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa Sheria ili kukomesha
kabisa vitendo vya udhalilishaji kwa watoto wetu.
NA KWA KUWA, hali halisi ilivyo sasa hasa katika
uendeshaji wa mashtaka ya wanaotuhumiwa kufanya udhalilishaji wa watoto
inaonyesha kuwa bado tunashindwa kulikabili tatizo hili na hivyo wahusika wengi
wa vitendo hivyo kuendelea na vitendo hivyo bila ya kupatikana na hatia
kutokana na udhaifu wa mfumo mzima wa utoaji haki katika kesi za aina hii.
NA KWA KUWA, endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa
katika suala hili, watoto wengi wanaweza kuathirika kiafya na kisaikolojia na
hivyo kuathiri maendeleo ya watoto hao na pia kuwafanya waathirika wa matukio
haya ya udhalilishaji watoto kupoteza imani na mfumo mzima wa utoaji haki.
HIVYO BASI
Mimi, Mgeni Hassan Juma, Mjumbe wa Baraza la
Wawakilishi nafasi za wanawake, chini ya kanuni ya 27(1) (n) 27(3), 49 (1) na
kanuni ya 50 ya kanuni za kudumu za Baraza la Wawakilishi toleo la 2012,
naliomba Baraza
hili tukufu, kwa kutumia mamlaka liliyo nayo liridhie kupitishwa maazimio
yafuatayo:-
1. Kuitaka Serikali ianzishe Mkakati wa
Kitaifa wa Kupambana na Kutokomeza Udhalilishaji wa watoto utakaojumuisha
Wawakilishi wa makundi mbali mbali katika jamii wakiwemo viongozi wa dini,
polisi, makundi ya wanasheria, asasi za kiraia, Ofisi ya Mkurugenzi wa
Mashtaka, Wakuu wa Wilaya, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na Wizara
nyengine zinazohusika;
2. Kwamba katika bajeti ya Serikali ya mwaka
2014/2015 na bajeti zitakazofuata, Mkakati wa kupambana na kutokomeza
udhalilishaji wa Watoto uwe ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ili hatua
za kupambana na udhalilishaji wa watoto zinazohitaji rasilimali fedha ziweze
kutekelezeka bila ya vikwazo;
3. Kwamba miongoni mwa majukumu ya msingi ya
Mkakati wa Kupambana na Kutokomeza Udhalilishaji wa Watoto yazingatie utoaji wa
taaluma kwa jamii kwa ujumla kuhusu namna ya kuwalinda watoto dhidi ya vitendo
vya udhalilishaji na pia namna ya kushughulikia matukio ya udhalilishaji watoto
pale yanapojitokeza;
4. Kwamba kutokana na udhaifu ulioonekana
katika kushughulikia kesi za udhalilishaji watoto, Serikali ianzishe utaratibu
wa mafunzo ya pamoja ndani na nje ya nchi katika vipindi maalum kwa wahusika
wanaosimamia mfumo wa utoaji haki katika kesi za watoto wakiwemo mahakimu,
waendesha mashtaka, polisi, madaktari na makarani wa mahkama ili kuyajengea
uwezo makundi hayo katika kushughulikia kesi za udhalilishaji watoto na pia
kuleta uratibu wa pamoja (coordination) miongoni mwa taasisi hizo;
5. Kwamba Serikali iingize katika mitaala ya
elimu hasa katika ngazi ya elimu ya awali na elimu ya msingi, suala la
udhalilishaji watoto na namna ya kujikinga dhidi ya udhalilishaji huo;
6. Serikali iwekeze rasilimali zaidi ili
kuziimarisha Mahakama za Watoto kwa kuweka idadi ya kutosha ya Mahakimu wa
kudumu wa mahakama hizo, majengo, samani na mambo mengine yatakayofanya kesi
hizo zisikilizwe katika muda mfupi na kwa kuzingatia haki;
7. Serikali ifanye mapitio ya Sheria ya Mtoto
na sheria nyengine zinazosimamia uendeshaji wa kesi za udhalilishaji wa mtoto
ili kuleta tija katika uendeshaji wa kesi hizo ikiwemo kuweka muda maalum
ambapo kesi hizo za udhalilishaji
zitapaswa kuwa zimemalizika;
8. Katika kurahisisha upelelezi wa kesi za
udhalilishaji wa watoto, serikali ihakikishe ndani ya kipindi kifupi kijacho,
mashine ya uchunguzi wa vinasaba (DNA) inapatikana hapa Zanzibar;
9. Kwamba Serikali ilete kila mwaka katika
Baraza la Wawakilishi, ripoti ya hatua zinazochukuliwa katika kulikabili tatizo
la udhalilishaji wa watoto itakayoonyesha hatua zilizochukuliwa katika kuzuia
tatizo hilo na matokeo yake na pale matukio ya udhalilishaji yalipojitokeza,
hatua zilizochukuliwa na matokeo ya hatua hizo;
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
………………………….
Mgeni Hasan Juma,
Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi,
Zanzibar.
No comments:
Post a Comment