Na Mwandishi Wetu Afrika Kusini
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumanne, Desemba
10, 2013, ameungana na viongozi wa mataifa mbali mbali duniani na maelfu ya
wananchi wa Afrika Kusini Kuadhimisha Kumbukumbu ya Kifo cha aliyekuwa kiongozi
mashuhuri wa Afrika Kusini na duniani, Mheshimiwa Nelson R Mandela.
Maelfu kwa maelfu ya
wananchi wamehimili mvua kubwa iliyokuwa inanyesha kwa nguvu kwenye Uwanja wa
Michezo wa FNB mjini Johannesburg
kumwaga Mzee Mandela ambaye alikuwa ishara kuu ya upinzani wa siasa za ubaguzi
wa rangi za makaburu wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mandela ambaye
alifariki duniani Ijumaa iliyopita, Desemba 5, 2013, alikuwa Kamanda wa Jeshi
la Ukombozi la Chama cha African National Congress la Umkhoto we Sizwe
akafungwa jela kwa uhaini kwa miaka 27 na utawala wa Makaburu.
Baada ya kutoka jela
mwaka Februari 1990, Mzee Mandela alichaguliwa kuwa Rais wa Kwanza
wa Afrika Kusini ya mwaka 1994. Lakini Mheshimiwa Mandela alitumikia kipindi
kimoja tu cha miaka mitano na kukataa kutumikia kipindi cha pili.
Kiasi cha viongozi 91
kutoka sehemu duniani wamehudhuria Kumbukumbu hiyo iliyokuwa na kila aina ya
mchanganyiko wa hisia – wengine wakiwa na majonzi na wengine wakicheza na
kuimba kwa muda wote wa shughuli hiyo iliyochukua kiasi cha jumla ya saa tano.
Mbali na Rais Kikwete
ambaye amefuatana na Mama Salma Kikwete, marais wengine mashuhuri duniani
waliohudhuria Kumbukumbu hiyo ni Mheshimiwa Barack Obama wa Marekani, Mheshimiwa
Francois Hollande wa Ufaransa, Waziri Mkuu wa Uingereza, Mheshimiwa David
Cameroun na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Ban Ki Moon.
Kumbukumbu hiyo pia
ilihudhuriwa na viongozi wa zamani wa Marekani wakiwemo marais watatu wa zamani
wa Marekani – Mheshimiwa Jimmy Carter, Mheshimiwa Bill Clinton na Mheshimiwa
George W Bush na mawaziri wakuu wawili wa zamani wa Uingereza, Mheshimiwa Tony
Blair na Mheshimiwa Gordon Brown.
Rais Kikwete kesho,
Jumatano, Desemba 11, 2013, ataungana na viongozi wenzake katia katika kutoa
heshima za mwisho na kuuaga rasmi mwili wa Marehemu Mandela ambao utawekwa
kwenye Majengo ya Urais wa Afrika Kusini ya Union
Buildings mjini Pretoria .
No comments:
Post a Comment