RIPOTI YA KAMATI TEULE YA
BARAZA LA WAWAKILISHI ILIYOUNDWA KUCHUNGUZA MIGOGORO YA ARDHI ZANZIBAR, 2013
UTANGULIZI:
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa Kanuni ya 120(1) ya Kanuni za Baraza la
Wawakilishi, toleo la mwaka 2012 ambayo inatoa uwezo kwa Baraza kuunda Kamati
Teule kwa ajili ya jambo fulani, Baraza liliunda Kamati Teule kwa ajili ya
kuchunguza baadhi ya migogoro ya ardhi hapa Zanzibar. Migogoro hiyo iliibuliwa na Wajumbe mbali
mbali wakati wa Mkutano wa Bajeti wa mwaka wa Fedha 2012/2013 na baadhi ya
migogoro hiyo ilitokana na taarifa ya Kamati za Kudumu za Baraza la
Wawakilishi.
Baada ya wewe Mheshimiwa Spika kutafakari kwa umakini
na kwa busara kubwa siku ya tarehe 10 Ogasti, 2012 uliwateua wajumbe wafuatao
kuunda Kamati Teule hiyo:-
1. Mheshimiwa Abdalla Mohammed Ali
2. Mheshimiwa Abdalla Juma Abdalla
3. Mheshimiwa Ali Mzee Ali
4. Mheshimiwa Fatma Mbarouk Said
5. Mheshimiwa Nassor Salim Ali
Aidha Kamati ilisaidiwa shughuli zake na Makatibu
wawili ambao ni Ndg. Mussa Kombo Bakari na Ndg. Khamis Hamad Haji. Barua za
uteuzi kwa Wajumbe wa Kamati zilitolewa tarehe 22/08/2012 na Kamati ilikutana
kwa mara ya kwanza tarehe 15 Octoba, 2012 kwa ajili ya kumteua Mwenyekiti wa
Kamati ambapo katika kikao hicho, wajumbe walimchagua Mheshimiwa Ali Mzee Ali
kuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo.
Pamoja na malalamiko mbali mbali yanayohusiana na
migogoro ya ardhi kuwasilishwa mbele ya Kamati wakati Kamati ilipokuwa
ikitekeleza majukumu yake, Kamati ilifanya kazi zake kwa mujibu wa Hadidu Rejea
ilizopatiwa na Baraza, ambazo zilikuwa kama ifuatavyo:-
1. Maeneo ambayo yanalalamikiwa kuwa umiliki
wake umefutwa kutoka kwa watu waliopewa umiliki wa maeneo hayo bila ya kufuata
taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria;
2. Maeneo ambayo yalikuwa yanatumiwa na
wananchi kwa shughuli zao za kuendesha maisha, lakini yamechukuliwa bila ya
kuzingatia maslahi ya wananchi waliokuwa wanayatumia;
3. Wawekezaji wanaochimba mchanga kwenye
maeneo ya fukwe;
4. Mgogoro wa Ardhi baina ya serikali na
wananchi (wakulima), Bambi;
5. Mgogoro wa Ardhi baina ya mfanyabiashara na
wakulima, Tumbe;
6. Mgogoro wa maeneo ya ardhi ya wananchi
yaliyonyang’anywa na kufanywa vitega uchumi, Makangale;
7. Mgogoro wa Ardhi kati ya wananchi na
viongozi wa serikali, Mchangamle,
Kizimkazi;
8. Mgogoro wa Ardhi kati ya wananchi,
Vitongoji Makaani;
9. Mgogoro wa Ardhi baina ya wanakijiji na
Muekezaji, Pwani Mchangani;
10.
Mgogoro
wa Ardhi baina ya wananchi na viongozi wakuu wa juu wa serikali, Tondooni
Mkunguni, Pemba;
11.
Mgogoro
wa ardhi baina ya Idara ya Upimaji na Ramani na Wizara ya Kilimo, Tumbe,
mgogoro ambao umepelekea wananchi kulivamia eneo hilo;
12.
Mgogoro
wa ardhi baina ya wananchi na muwekezaji, shehia ya Mzwardini, Bwejuu.
Mheshimiwa Spika,
Ni vyema ikafahamika kuwa pamoja na hadidu rejea
ilizopatiwa Kamati Teule kuwa kumi na mbili, hadidu rejea namba moja na namba
mbili zilitajwa kwa ujumla jumla bila ya kuweka wazi migogoro yenyewe na hivyo
Kamati ilifanya kazi ya kupitia hansard ili kupata migogoro mahsusi ambayo
Kamati iliifanyia kazi. Hivyo maeneo ambayo Kamati hii iliyafanyia kazi yaliongezeka
kutoka kumi na mbili hadi kufikia maeneo ishirini na moja. Baada ya kupitia
hansard kuhusiana na hadidu rejea namba moja, Kamati ilipata kadhia nane ambazo
ilizifanyia kazi. Kadhia hizo ni hizi zifuatazo:-
1. Kadhia ya Mgogoro wa ardhi Maruhubi unaomhusisha
Bw. Ali Muradi
2. Kadhia ya mgogoro wa ardhi unaohusisha
kampuni ya Leisure Corp (Al Nakheel)
3. Kadhia ya mgogoro wa ardhi unaohusisha
kampuni ya Sovereign Sands Resort
4. Kadhia ya mgogoro wa ardhi unaohusisha
kampuni ya SAGO Palm
5. Kadhia ya mgogoro wa nyumba ya Mazizini
6. Kadhia ya mgogoro katika kisiwa cha Kwale
7. Kadhia ya mgogoro wa ardhi unaohusisha
kampuni ya Sunset Paradise Resort
8. Kadhia ya mgogoro wa ardhi unaomhusisha Bw.
Bruno Conti
Aidha katika hadidu rejea mamba mbili, Kamati baada ya
kupitia hansard ilipata maeneo matatu ya kuyafanyia kazi chini ya hadidu rejea
hiyo. Maeneo hayo ni haya yafuatayo:-
1. Mgogoro wa mashamba ya Selem
2. Mgogoro wa mashamba ya Kijichi
3. Mgogoro wa mashamba ya Dole
Kamati hiyo ilianza rasmi kazi ya kuchunguza migogoro
ya ardhi iliyotajwa tarehe 29 Octoba, 2012.
Kamati iliwahoji wahusika mbali mbali wakiwemo Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi walioibua hoja hizo ndani ya Baraza, watendaji wa taasisi mbali
mbali, wananchi wanaohusika na migogoro hiyo na watu wengine mbali mbali. Aidha
Kamati ilitembelea maeneo mbali mbali yenye migogoro na kupata maelezo kutoka
pande zilizohusika na migogoro hiyo.
Mheshimiwa Spika,
Kamati katika kuchunguza migogoro hiyo ya ardhi
ilifanya kazi zake kwa muda wa siku ishirini ambapo kwa upande wa Unguja Kamati
ilifanya kazi kwa siku kumi na tano na kwa upande wa Pemba ilifanya kazi kwa
siku tano za kazi. Hatimaye Kamati ilikutana kwa muda wa siku saba kwa ajili ya
uchambuzi wa hoja na vielelezo vilivyowasilishwa mbele ya Kamati pamoja na
kupitia ripoti ya Kamati na kufanya maamuzi kwa kila jambo lililoshughulikiwa
na Kamati.
Kamati katika kutekeleza majukumu yake ilizingatia
misingi ya sheria ya Kinga, Nguvu na Uwezo ya Baraza la Wawakilishi ya mwaka
2007 na Kanuni za Baraza la Wawakilishi, Toleo la Mwaka 2012. Kwa mfano, Kamati
ilizingatia Kanuni ya 108(17) Inayotaka Kamati kutoshughulikia jambo lolote
linalosubiri uamuzi wa mahakama. Baada ya kupata taarifa za kuwepo kwa kesi
mahakamani katika baadhi ya migogoro, Kamati ilifuatilia kwa kuandika barua kwa
taasisi zinazohusika ili kupata ufafanuzi juu ya kuwepo kwa mashauri katika
mahakama kuhusiana na jambo ambalo lina uhusiano na hadidu rejea za Kamati
Teule na baada ya kuthibitishiwa kuwepo kwa kesi katika kadhia hizo, Kamati
ilisita kushughulikia masuala hayo.
Aidha, Kamati ilizingatia Kanuni ya 123 ya Kanuni za
Baraza la Wawakilishi inayoelekeza kuwa Kamati Teule kuwasilisha taarifa yake
pamoja na vielelezo. Kamati hii kwa kuelewa matakwa hayo ya kanuni, ilijitahidi
kukusanya vielelezo kwa kuwasiliana mara kwa mara na taasisi mbali mbali za
serikali pamoja na kuweka msisitizo kwa taasisi hizo kuipatia Kamati vielelezo
vilivyohitajika. Kamati ilifanikiwa kupata baadhi ya vielelezo hivyo ambavyo
vinaambatanishwa na ripoti hii na ambavyo vinafafanuliwa katika hadidu rejea
husika. Hata hivyo, Kamati ilishindwa kupata baadhi ya vielelezo ilivyohitaji
pamoja na hatua zilizochukuliwa za kuzungumza na watendaji na kuwaandikia barua
kuhitaji vielelezo hivyo.
Historia
Fupi ya Ardhi Zanzibar
Mheshimiwa Spika,
Ardhi imekuwa ni tatizo kubwa kwa nchi nyingi
zilizotawaliwa duniani. Kwa hapa Zanzibar ardhi ilimilikiwa na watawala chini
ya Sultan na wageni walipoingia ndani ya nchi walitafuta ardhi yenye rutuba. Kwa hivyo, ardhi yenye
rutuba kwa kiasi kikubwa wakati wa ukoloni ilimilikiwa na watu wachache na
wananchi waliokuwa wengi hawakuwa na ardhi hasa ile yenye rutuba. Kwa mfano,
mashamba makubwa 745 yaliyokuwepo Unguja na Pemba wakati wa Sultan yalimilikiwa
na makabaila na mabepari 73 tu. Orodha ya mashamba makubwa na mabepari na
makabaila waliokuwa wakiyamiliki inaambatanishwa na ripoti hii kama
Kiambatanisho namba KTA 1A.
Ahadi ya chama cha Afro
Shiraz kuhusu ardhi
Kutokana na hali hiyo ya kutokuwepo kwa usawa katika
umiliki wa ardhi hapa nchini, harakati za kuwakomboa wananchi wa Zanzibar kwa
kuwafanya nao wamiliki rasilimali za nchi na hivyo kuondokana na unyonge
waliokuwa nao zilianza hata kabla ya Mapinduzi ya 1964.
Tarehe 8 Machi, 1959, hapo Machui, kiongozi mkuu wa
chama cha Afro Shiraz Marehemu Sheikh Abeid Aman Karume alitangaza kuwa Afro
Shiraz ikipata serikali, ardhi yote itakuwa mali ya wananchi wa Zanzibar.
Kutokana na ahadi hiyo kulikuwa na madhila na unyonge waliofanyiwa wakulima
waliokuwa chama cha Afro Shiraz na kuondolewa katika mashamba waliokuwa
wakilima na hatimaye chama cha Afro Shiraz kikanunua shamba la Kilombero na
kuwakabidhi wanachama wake ili waweze kuendesha maisha yao.
Mheshimiwa
Spika,
Mapinduzi matukufu yalifanyika tarehe 12 Januari mwaka
1964 na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar tarehe 8 Machi, 1964 alitangaza na
kutekeleza ahadi ya ASP iliyotolewa Machui mwaka 1959 kwa kutoa taarifa muhimu
ambayo ni Azimio la Jamhuri ya Zanzibar. Azimio hilo lilikusudia kuiweka ardhi
yote mikononi mwa serikali kwa ajili ya kuigawa kwa wananchi kwa usawa. Nakala
ya Azimio hilo inaambatanishwa na Ripoti hii kama Kiambatanisho KTA 1B. Azimio
hilo lilifuatiwa na sheria mbali mbali ikiwemo Sheria ya ‘’The Confiscation of
Immovable Property Decree, 1964’’ na Sheria ya Ugawaji wa Ardhi ‘’(The Land
(Distribution) Decree, 1966’’ ili kutekeleza azma ya kuiondoa ardhi mikononi
mwa makabaila na mabepari wachache na kuwapatia wananchi walio wengi ardhi
hiyo. Kazi ya kugawa ardhi ilianza rasmi kwa Unguja tarehe 8/11/1965 kwa shamra
shamra na sherehe kubwa sana katika ardhi ya Dole, wilaya ya Magharibi katika
Shamba la Mfalme Hemed bin Thuwein ambapo hadi mwaka 1973, eka 24,000 ziligaiwa
kwa wananchi. Kwa upande wa Pemba kazi hiyo ya kugawa ardhi kwa wananchi
ilianza Mbiji, Wilaya ya Mkoani, na hadi kufikia mwaka 1972, eka 72,000
zilishagaiwa kwa wananchi.
Aidha katika kudhihirisha azma yake ya kuwanyanyua
wananchi hao kiuchumi, Serikali iliwasaidia kwa kiasi kikubwa wananchi
waliojishughulisha na kilimo, kwanza kwa kutowatoza kodi yoyote kwa maeneo waliyopewa
tofauti na ilivyokuwa kabla ya Mapinduzi ambapo wananchi hao walipaswa kulipa
kodi kwa maeneo waliyokuwa wakilima. Aidha baada ya kuwapatia wananchi eka
tatu, Serikali ilianza kuwatoza wananchi shilingi 28 kwa eka moja kwa
kuchimbuliwa na kuburugiwa tofauti na ilivyokuwa kabla ya Mapinduzi ambapo
wananchi hao walilipa Shilingi 75 kwa kuchimbuliwa tu bila ya kuburugiwa.
Baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964, zilitungwa
sheria zilizoweka misingi ya mapinduzi. Sheria hizo zinajumuisha The
Legislative Powers Law, 1964 ambayo ilitoa mamlaka kwa Baraza la Mapinduzi
kutunga sheria, The Constitutional Government and the Rule of Law Decree, 1964,
The Equality, 1964, High Court Decree, 1964 na Sheria Nam. 6 ya mwaka 1964
inayojulikana kama ‘’Reconciliation and Unity of Zanzibar Peoples Decree’’
ambayo nakala ya kiswahili inaambatanishwa na ripoti kwa ajili ya rejea kwa
Waheshimiwa Wajumbe kama Kiambatanisho Nam KTA 1C. Sheria hizi ziliweka misingi
ya utawala wa sheria katika nchi na kuweka misingi ya usawa na utu miongoni mwa
wananchi na kuondokana na misingi ya kubaguliwa kutokana na rangi, ukabila,
jinsia au kwa namna yoyote. Sheria hizi pia ziliimarisha miongoni mwa wananchi
usawa, umoja na kujenga muafaka baina yao. Aidha sheria hizo ziliweka misingi
hiyo ya usawa kwa kutangaza rasmi kuwa kila raia wa Zanzibar ana haki iliyo
sawa katika kupata haki, fursa na ulinzi kwa uraia wake. Mheshimiwa Spika, ili
kufahamu umuhimu na uzito wa sheria Nam. 6 ya mwaka 1964, tunaomba kunukuu
baadhi ya vifungu vya sheria hiyo kama ifuatavyo:-
Kifungu cha
2. ‘’ Madhumuni makuu ya Mapinduzi ya Watu wa
Zanzibar ni kutokomeza upendeleo wa kiuchumi, kijamii au upendeleo wa kisheria
na mapungufu yote yaliyopita yaliyokuwa yanawagawa wananchi na makundi mbali
mbali ya raia kwa njia ya ukabila, jinsia, dini au uasili wa mtu, na madhumuni
hasa ya Mapinduzi ni kukuza usawa, maridhiano na umoja kwa Watu wa Zanzibar.
Kifungu cha
3. ‘’kwa msingi huo, kila raia wa
Zanzibar anatangazwa kuwa ana haki sawa, fursa na hifadhi ya uraia wake kama
vile ambavyo anatekeleza majukumu na wajibu wake wa uraia. Hakuna haki, fursa
au hifadhi inayoweza kufutwa kisheria kwa raia yeyote kwa kutumia vyombo vya
dola au kwa kutumia hatua za mtu binafsi kwa sababu ya msingi au kisingizio cha
ukabila, dini, jinsia au uasili wa raia huyo’’.
Kifungu cha
4. ‘’hakuna kifungu chochote ndani ya
sheria hii kitakachoizuia serikali kutunga sheria itakayotoa nafuu maalum au
upendeleo wa kiuchumi, kiutamaduni au kijamii kwa raia waliokosa haki za msingi
kwa madhumuni ya kuwaletea usawa kama raia wengine’’.
Mheshimiwa
Spika,
Msingi wa Mapinduzi ya mwaka 1964 ni kuwakomboa
wananchi na kuimarisha hali za wananchi wote wa Zanzibar na kuondoa tofauti
kubwa ya kipato iliyokuwepo wakati wa ukoloni. Kwa msingi huo, ndio maana mageuzi
ya ardhi (Land Reform) yaliyofanywa Zanzibar yalikusudia kugawanya ardhi kwa
wananchi masikini wa Zanzibar na kuitoa ardhi hiyo mikononi mwa Mabepari
wachache. Azma hii inathibitishwa na maneno ya Marehemu Sheikh Abeid Aman
Karume aliyoyatoa mara baada ya mapinduzi ya mwaka 1964 na Mheshimiwa Spika
naomba ninukuu baadhi ya maneno hayo kama ifuatavyo:-
‘’ Sisi tumejitawala ili
uchumi wa nchi hii uwe mikononi mwetu. Ikiwa yupo kiongozi anayewapa wageni
fursa ya uchumi wa nchi, basi hafai.
Tunataka pato la nchi hii liwarejee wenyewe wananchi’’.
‘’ Mwenyezimungu
katujaalia mambo mawili makubwa sana katika nchi yetu. La kwanza sisi ni
kidogo, na la pili tunayo ardhí nzuri yenye rutuba ambayo watu wengi duniani
hawana’’.
‘’Kama tulivyoupindua
usultani sasa tunaupindua ubepari. Mtu mmoja kuwa na eka elfu tatu peke yake,
na watu wengine wakawa hawana kitu, hapa kwetu mpango huo basi’’.
Maneno haya mazito na yaliyojaa uzalendo yanafaa
kuenziwa kwa vitendo wakati tukikaribia kuadhimisha miaka hamsini ya mapinduzi
yetu kwa kuzingatia kuwa suala la serikali kuichukua ardhí na kuigawa kwa
wananchi ilikusudia kurejesha utu kamili. Marehemu Sheikh Abeid Aman Karume
alisema na tunamnukuu ‘’Katika mwaka 1964, tulichukua hatua ya kurejesha utu
kamili, kwa kufanya ardhí ni mali ya wananchi wote’’.
Mheshimiwa
Spika,
Katika usimamizi wa suala la ardhi, sheria nyingi
zimetungwa toka wakati wa utawala wa Sultan ili kuratibu usimamizi huo. Katika
kipindi cha miaka sitini na tatu kabla ya mapinduzi ya mwaka 1964 kuanzia mwaka
1900 hadi mwaka 1963, sheria nane zinazohusiana na masuala ya ardhi zilitungwa.
Orodha ya sheria hizo inaambatanishwa na ripoti hii kama kiambatanisho Nam. KTA
1D.
Katika kipindi cha miaka arobaini na tisa baada ya
Mapinduzi ya mwaka 1964 hadi sasa, sheria 17 zinazohusiana na masuala ya ardhi
zimetungwa. Orodha ya sheria hizo inaambatanishwa na ripoti hii kama
kiambatanisho Nam. KTA 1E. Kutungwa kwa sheria hizi kunadhihirisha uzito wa
suala hili la ardhi hapa Zanzibar ambapo pamoja na kuwepo kwa sheria zote hizo
zinazosimamia ardhi, bado migogoro ya ardhi imejitokeza na inaendelea
kujitokeza katika sehemu mbali mbali hapa Zanzibar. Historia inaonyesha kuwa
migogoro hii imeanza muda mrefu toka enzi ya ukoloni na Kamati hii ilipata
fursa ya kupitia ripoti ya Bw. R.H.W Pakenham ya mwaka 1946 inayoonyesha namna
alivyofanya uchunguzi katika mgogoro wa ardhi miongoni mwa wahadimu huko
Chwaka, mgogoro ambao ulihusisha vijiji vya Shahafi na Mkanjani. Bw Pakenham aliteuliwa kuchunguza mgogoro
huo, tarehe 5 Febuari,1944 kupitia Gazeti Rasmi la Serikali na kutakiwa kutoa
ripoti si zaidi ya tarehe 30 Juni, 1944.
Mheshimiwa Spika,
Mgogoro mwengine wa ardhi uliojitokeza Zanzibar na
kufanywa uchunguzi maalum ni ule wa Vitongoji katika Mudiria ya Chake Chake,
Pemba ambapo tarehe 29/08/1955 Sir John Gray aliteuliwa kuchunguza mgogoro huo
na kutakiwa kuangalia watu wenye haki katika maeneo hayo. Mgogoro huo
uliwahusisha Sheikh Abdulla bin Mbarak el- Mauli na familia yake, Khamis bin
Faki Shiraz na wenzake kumi na tatu, Hassan bin Ali na Nassor bin Khalfan el-
Yorubi. Kamati inapenda kuambatanisha sehemu ya utangulizi na mapendekezo ya
ripoti hiyo ya Sir. John Gray ili wajumbe waweze kufanya rejea.
Ripoti nyengine zilizowahi kuelezea masuala ya ardhi
ni pamoja na Land Tenure System and Land Reform in Zanzibar; 1830- 1870; ya
Prof. Ibrahim Fokas Shao, utafiti uliofanywa na W.R. McGeagh and W. Addis,
Review of the Systems of Land Tenure in Zanzibar and Pemba, Zanzibar 1934 na
ripoti ya Land Tenure in Zanzibar ya mwaka 1961 ya John Middleton na nyingi
nyenginezo.
Mheshimiwa Spika,
Baada ya utangulizi huo pamoja na historia fupi ya
masuala ya ardhi hapa Zanzibar, sasa naomba kuwasilisha taarifa ya namna hadidu
rejea zilivyoshughulikiwa pamoja na uamuzi na mapendekezo ya Kamati kama
inavyoainishwa katika bango kitita hapa chini.
Hadidu Rejea ya kwanza.
Maeneo ambayo yanalalamikiwa kuwa umiliki wake
umefutwa kutoka kwa watu waliopewa umiliki wa maeneo hayo bila ya taratibu
zilizowekwa kwa mujibu wa sheria
Namna ilivyoshughulikiwa na
Kamati
Katika Hadidu Rejea hii, Kamati ilizingatia hoja mbali
mbali ambazo zilizungumzwa na wajumbe wa Baraza ambazo zilihusu maeneo
yanayolalamikiwa kuwa umiliki wake umefutwa na kupewa wengine bila ya kufuata
utaratibu wa kisheria. Hoja kuhusu maeneo hayo zinafafanuliwa hapa chini:-
1. Kadhia
ya Bw. Ali Muradi;
Namna ilivyoshughulikiwa.
Kamati katika kushughulikia suala hili ilimualika
Mjumbe wa Baraza aliyeibua hoja hii ndani ya Baraza, Mheshimiwa Ali Salum Haji.
Mjumbe huyo aliieleza Kamati kuwa aliibua hoja hii
baada ya kupata malalamiko ya Bw. Ali Muradi kuwa amenyang’anywa eneo
alilopatiwa kwa mujibu wa sheria akiwa na hati na kupewa mtu mwengine.
Mjumbe huyo aliendelea kuieleza Kamati kuwa pamoja na
Waziri anayehusika na ardhi kulieleza Baraza kuwa suala hilo limeshamalizika
baada ya kumpatia Bw. Ali Muradi eneo jengine, mgogoro huo bado upo kutokana na
kutokuwepo kwa makubaliano baina ya pande zinazohusika. Aidha Kamati
ilitembelea eneo linalodaiwa kuchukuliwa kutoka kwa Bw. Ali Muradi na kupewa
kampuni ya Zanzibar Dairy Products kwa makusudio ya kumpatia eneo jengine Bw.
Ali Muradi kama ilivyoelezwa na Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati
wakati wa bajeti ya Wizara yake mwaka 2012/2013 kwa mujibu wa hansard ya tarehe 13 Julai, 2012, ukurasa wa 73.
Katika ziara hiyo Kamati ilifuatana na watendaji wa
Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati wakiongozwa na Mkurugenzi wa Ardhi na
Usajili.
Watendaji hao wa Wizara waliionyesha Kamati eneo
ambalo Bw. Ali Muradi alikuwa akilimiliki na kueleza kwamba eneo hilo
lilionekana kufaa sana kuongeza (extension) eneo la kiwanda cha Zanzibar Diary
Products na hivyo Bw. Ali Muradi kupatiwa eneo jengine ili kupisha utanuzi wa
eneo la kiwanda hicho cha maziwa.
Kutokana na Bw. Ali Muradi kutokuwepo katika ziara
hiyo iliyofanywa, Kamati ilifanya juhudi na kukutana na Bw. Ali Muradi ambaye
mara nyingi amekuwa nje ya Zanzibar kutokana na shughuli zake. Kikao hicho
baina ya Kamati na Bw. Ali Muradi kilifanyika katika Afisi ya Baraza la
Wawakilishi, tarehe 16/07/2013.
Bw. Ali Muradi aliieleza Kamati kuwa alikiomba kiwanja
hicho kilichokuwa kikimilikiwa na Wizara ya Kilimo kwa barua na baada ya
mashauriano baina ya Wizara ya Kilimo na Wizara iliyokuwa inashughulikia Ardhi,
alikabidhiwa rasmi kiwanja hicho kwa hati, tarehe 10/12/2003. Hati hiyo ni
sehemu ya ripoti hii kama Kiambatanisho
nam. KTA 1. Bw. Ali Muradi
aliendelea kuieleza Kamati kuwa eneo hilo alilopewa kwa wakati huo alipopewa
lilikuwa halijengeki kutokana na kupita umeme wa voltage kubwa na kuhitaji
kufukiwa, mambo yaliyomlazimu kutumia fedha nyingi na muda mwingi ili
kurekebisha mazingira ya eneo hilo.
Aidha Bw. Ali Muradi aliileza Kamati kuwa alipata
kibali cha ujenzi wa ukuta kilichotolewa 3/10/2011 kutoka Baraza la Manispaa
Zanzibar. Kibali hicho kinaambatanishwa na ripoti kama Kiambatanisho nam. KTA2.
Kamati pia ilielezwa na Bw. Ali Muradi kuwa baada ya
marekebisho kadhaa aliyoyafanya katika kiwanja hicho ili kiweze kutumika kwa
matumizi aliyoyakusudia ambayo ni kuweka kontena (Container Terminal), eneo
hilo lilibadilika ikiwemo ukubwa wa eneo hilo.
Bw. Ali Muradi alidai kuwa wakati akiendelea na
ujenzi, aliamriwa kusitisha ujenzi huo na Idara ya Ardhi na Usajili kwa kudaiwa
kuwa umiliki wa eneo hilo ulishafutwa kwa barua iliyoelekezwa kwa Bw. Ali
Muradi ambaye hata hivyo alikanusha kuwa aliipata barua hiyo. Bw. Ali Muradi
aliwasilisha mbele ya Kamati, nakala ya barua ya kusitisha ujenzi huo ya tarehe
19/03/2012 ambayo ilieleza kuwa umiliki wa eneo hilo umesitishwa tokea tarehe 29/02/2012. Barua hiyo inafanya sehemu
ya ripoti hii kama Kiambatanisho nam.
KTA3.
Bw. Ali Muradi aliijibu barua hiyo kupitia kwa wakili
wake na kueleza kuwa hakuwahi kuipata barua hiyo na pia hakuwahi kupewa notisi
ya ufutaji wa haki ya kulitumia eneo hilo kama sheria inavyoelekeza. Barua hiyo
iliwasilishwa mbele ya Kamati na hivyo inakuwa sehemu ya ripoti hii kama Kiambatanisho nam. KTA4.
Tarehe 21/03/2012
Wizara ya Ardhi ilimuandikia tena Bw. Ali Muradi ikimueleza kuwa aliwahi
kupatiwa notisi ya kumfutia hati ya matumizi ya eneo hilo kwa kushindwa
kuliendeleza kwa kipindi kirefu na kuambatanisha barua hiyo na nakala ya
ukurasa wa kitabu cha kupokelea barua (dispatch book) kuthibitisha kuwa Bw. Ali
Muradi alipokea barua hiyo ambaye hata hivyo anakanusha na kudai kuwa saini
iliyowekwa si yake. Barua hiyo iliwasilishwa mbele ya Kamati na hivyo inafanya
sehemu ya ripoti kama Kiambatanisho nam.
KTA5
Aidha Bw. Ali Muradi aliijibu barua hiyo siku hiyo ya
tarehe 21/03/2012 kupitia kwa wakili wake na kudai kuwa hakuwahi kufikishiwa
barua ya kusitisha umiliki wa eneo hilo wala ya notisi ya kukusudia kusitisha
umiliki huo na kudai katika barua hiyo kuwa notisi ya kumtaka ajieleze ni kwa
nini asifutiwe umiliki wa eneo hilo ilitumwa kwa tarehe ya mbele baada ya hati
ya eneo hilo kuwa imeshafutwa jambo ambalo lilionyesha kasoro. Barua hiyo pia
iliwasilishwa mbele ya Kamati na hivyo inafanywa kuwa sehemu ya ripoti hii kama
Kiambatanisho nam. KTA 6.
Awali Bw. Ali Muradi alieleza kuwa aliwahi kuitwa
mbele ya Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo na Makatibu wakuu wa wizara hizo na
kuelezwa kuwa serikali ilifanya makosa kumpa eneo ambalo tayari lilikuwa
likimilikiwa na mtu mwengine na kuomba asaidie ili kupatikana kwa ufumbuzi.
Bw. Ali Muradi aliieleza Kamati kuwa alitoa masharti
kuwa ili aweze kusaidia, athibitishiwe kuwa eneo hilo kweli alishapewa mtu
mwengine kabla yake pamoja kumpatia eneo mbadala linalofanana na eneo alilonalo
masharti ambayo anadai hayajatekelezwa.
Kwa upande wake, Wizara ya Ardhi iliieleza Kamati kuwa
eneo hilo lenye mgogoro liliombwa na mwekezaji mzalendo aliyekuwa na azma ya
kuweka kiwanda cha uzalishaji wa maziwa cha Zanzibar Dairy Products.
Wizara ilieleza kuwa hati ya eneo hilo aliyopewa Bw.
Ali Muradi ilifutwa ili eneo hilo akabidhiwe mwekezaji wa Zanzibar Dairy
Products na Bw. Ali Muradi kupewa eneo jengine mbadala.
Wizara iliwasilisha barua inayoonyesha kufutwa kwa
hati hiyo iliyosainiwa terehe 29/02/2012
na Mhe. Ali Juma Shamhuna akiwa Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati,
ambayo ilieleza sababu za kufutwa ni
kuwa Bw. Ali Muradi kushindwa kuliendeleza eneo alilopewa toka mwaka 2003,
barua hiyo inaambatanishwa na ripoti hii kama Kiambatanisho nam. KTA 7
Hata hivyo, Wizara iliwasilisha kielelezo chengine cha
kufutwa kwa hati ya Bw. Ali Muradi mbele ya kamati ambayo ni barua iliyosainiwa
na Mhe. Ramadhan Abdalla Shabaan tarehe 6/08/2012 ikieleza sababu za kufutwa
kwa hati ya kiwanja hicho kuwa ni kuwapo
kwa hati nyengine namba 195/95 ya tarehe 29/6/1995 kwa eneo hilo, iliyotolewa
kabla ya eneo hilo kupewa Bw. Ali Murad. Barua hiyo ya pili ya kufuta hati ya
Bw. Ali Muradi inaambatanishwa na ripoti hii kama kiambatanisho namba KTA 8.
Baada ya kupata barua hiyo ya pili ya kufuta hati ya
Bw.Ali Muradi, kamati iliiandikia barua Wizara ya Ardhi ya tarehe 12/11/2013,
ya kuitaka Wizara iipatie kamati hati hiyo namba 195/95 ambayo hata hivyo
Wizara ilishindwa kuwasilisha nakala ya hati hiyo.
Barua hiyo ya Kamati kuhusu maombi ya kupatiwa hati
hiyo kwa Wizara inaambatanishwa na ripoti hii kama kiambatanisho namba KTA 9.
MAONI YA KAMATI
Katika eneo hilo hilo moja alilopatiwa Bw. Ali Muradi,
inaonekana mawaziri wawili wa Wizara inayoshughulika na ardhi kwa wakati
tofauti walitoa barua ya kufuta hati ya muda ya matumizi ya ardhi.
Katika barua ya awali ya ufutaji wa kiwanja hicho ya
tarehe 29/02/2012 iliyosainiwa na Mheshimiwa Ali Juma Shamuhuna, ambaye alikuwa
Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kwa wakati huo, maelezo ya sababu ya
kufutwa kwa kiwanja hicho ni kutokana na Bw.Ali Muradi kushindwa kuliendeleza
eneo hilo.
Hata hivyo, hati hiyo hiyo ya muda ya Bw. Ali Muradi
ilifutwa tena tarehe 06/08/2012 kwa barua iliyosainiwa na Mheshimiwa Waziri wa
Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kwa maelezo kuwa eneo hilo tayari lilishawahi
kutolewa hati kwa mtu mwengine na kwamba wakati Bw. Ali Muradi anapatiwa eneo
hilo, hati hiyo ya mwanzo yenye namba 195/95 ilikuwa haijafutwa.
Kamati iliomba kupatiwa hati hiyo iliyotolewa mwanzo
kwa maandishi na hadi wakati wa kuwasilisha ripoti hii, wizara ya Ardhi,
Makaazi, Maji na Nishati imeshindwa kuwasilisha nakala ya hati hiyo.
Hata hivyo maelezo hayo yanapingana na kauli aliyoitoa
Mkurugenzi wa Idara ya Ardhi wakati wa ziara katika eneo la tukio na pia
maelezo ya Wizara ya maandishi kwamba sababu ya kumuondoa Bw. Ali Muradi ni
kufuatia muwekezaji wa Zanzibar Dairy Products kuhitaji kuongeza eneo kwa
shughuli za kiwanda. Aidha kwa mujibu wa hansard ya Baraza ya tarehe 13 Julai,
2012, Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati alilieleza Baraza kuwa mgogoro
wa eneo hilo umemalizika kwa kampuni ya Zanzibar Dairy Product na Bw. Ali
Muradi kila mmoja kupatiwa eneo. Utaratibu huu si wa kawaida kwa anayefutiwa
hati kupatiwa eneo jengine.
Aidha wizara ya Ardhi katika taarifa yake kwa kamati
ilieleza kuwa eneo hilo lilifutwa kutokana na eneo hilo kuwahi kupewa mtu
mwingine na hivyo kuamua kufuta hati ya Bw. Ali Muradi kwa msingi huo.
Kamati iliitaka Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na
Nishati kuwasilisha mbele ya Kamati hati ya matumizi ya ardhi iliyotolewa awali
kwa ajili ya kiwanja hicho kwa kuiandikia barua mara kadhaa lakini hata hivyo
Wizara ilishindwa kuwasilisha nakala ya hati hiyo hadi wakati wa kuwasilisha
ripoti hii.
Kamati pia iliarifiwa kuwepo kwa Kamati ya mawaziri
wawili ambao ni waziri anayeshughulikia Fedha na yule anayeshughulikia ardhi
ambayo inajaribu kusuluhisha tatizo la eneo hilo la Maruhubi. Kamati hii
inaamini utaratibu huu pia si wa kawaida na hauzingatii matakwa ya sheria ya ardhi.
Kwa kuwa katika suala hili sababu za kufuta hati ya
muda ya matumizi ya ardhi zinatofautiana na kwamba Bw. Ali Muradi alifutiwa
hati hiyo kabla ya kupatiwa notisi, ambapo alipatiwa notisi hiyo baada ya
kufutiwa hati hiyo badala ya kupewa notisi hiyo kabla ya kufutiwa hati hiyo,
kamati inaamini kuwa taratibu za kufuta hati hiyo hazikufutwa kwa ukamilifu na
hivyo kamati inapendekeza kuwa ufutaji wa hati ya matumizi ya kiwanja hicho
ubatilishwe.
1. Kadhia
ya Leisure Corp (Al-Nakheel)
Namna ilivyoshughulikiwa.
Katika kuishughulikia kadhia hii, Kamati ilimualika
Mjumbe aliyeiwasilisha katika kikao cha Baraza Mhe. Hamza Hassan Juma ili
kupata maelezo zaidi na vielelezo kuhusiana na hoja hiyo. Mjumbe aliieleza
Kamati kuwa Kampuni ya Al Nakheel ilikodishwa eneo huko Matemwe kwa ajili ya
uwekezaji wa hoteli na kampuni hiyo ilifutiwa eneo hilo kwa kushindwa
kuliendeleza kwa mujibu wa sheria ya Matumizi ya Ardhi ya mwaka 1992.
Hata hivyo Mjumbe aliieleza Kamati kuwa wizara katika
ufutaji wa hati ya ukodishaji wa eneo hilo, haikuzingatia masharti ya kifungu
cha 48 cha Sheria ya Matumizi ya Ardhi ambacho kinaelekeza kutolewa kwa notisi
ya miezi mitatu kwa aliyekodishwa ardhi kabla ya kumfutia hati hiyo. Ili
kujiridhisha katika madai hayo kamati iliomba Wizara ya Ardhi, kuipatia nakala
ya barua ya notisi kwa kampuni hiyo.
Mjumbe aliwasilisha nakala ya barua za malalamiko ya ufutwaji huo, kutoka kwa mwekezaji
huyo kwenda kwa Waziri wa Ardhi na Mamlaka ya Uendelezaji Vitega Uchumi
Zanzibar (ZIPA). Nakala za barua hizo zinaambatanishwa na ripoti hii kama Kiambatanisho nam KTA 10.
Wizara ya Ardhi iliieleza Kamati kupitia ripoti yake
kwa kamati katika ukurasa wa 10, kuwa mwekezaji huyo alifutiwa hati ya
ukodishaji ardhi tarehe 14 Machi, 2011 baada ya kushindwa kuliendeleza eneo
hilo toka mwaka 2007 alipopatiwa, nakala ya ripoti hiyo inaambatanishwa pamoja
na ripoti hii na kuwa kiambatanisho
namba KTA 11.
Wizara iliendelea kueleza kuwa baada ya kufutiwa mkataba wa ukodishwaji kwa kampuni
ya Leisure Corp. LLC eneo hilo lilikodishwa kwa kampuni ya Penny Royal
(Gilbraltar), AEACUS Ltd na Horizon Resort Ltd, pamoja na kutoa hati ya
matumizi ya ardhi kwa ndugu Saleh Mohamed Said na ndugu Elizabeth Mayala.
Wizara iliwasilisha nakala ya barua ya ufutaji wa hati ya kukodishwa ardhi kwa
kampuni hiyo na pia kwa makampuni ya Supercab Hotel Development, Penny Royal
Limited, Aeacus limited, Horizon Resorts Limited, Ndg. Saleh Mohammed Said na
Ndg. Elizabeth Lazaro Mayala.
Wizara ilieleza kuwa makampuni hayo matatu yalifutiwa
mikataba ya ukodishwaji kutokanana miradi yao kutopitia na kuidhinishwa na
ZIPA. Aidha hati za matumizi ya ardhi kwa ndugu Elizabeth Mayala na ndugu Saleh
Mohamed Said, zilielezwa kufutwa kutokanana kutolewa katika maeneo ya
uwekezaji.
Barua za kufuta mikataba ya ukodishaji ardhi ya
Kampuni za Supercab Hotel Development, Leisure Corp. LLC (Al Nakheel) na
kampuni tatu zilizopewa badala yake
pamoja na hati za matumizi za ndugu Elizabeth Mayala na ndugu Saleh
Mohamed Said zinaambatanishwa na ripoti hii kama kiambatanisho namba KTA 12.
Hata hivyo katika barua hizo za ufutaji wa mikataba
hiyo, Kamati imebaini kasoro iliyokuwepo ambapo Kampuni ya Leisure Corp
ilifutiwa mkataba siku moja na Kampuni hizo tatu zilizodaiwa kupewa eneo hilo
baada ya Kampuni ya Leisure Corp kufutiwa. Hii inaonyesha kuwa kampuni hizo
tatu zilipewa eneo hilo wakati Kampuni ya Leisure Corp ikiwa haijafutiwa
mkataba wa ukodishwaji.
MAONI YA KAMATI
Katika kadhia hii, pamoja na kamati kuhitaji kupatiwa
nakala ya notisi kabla ya kufuta mkataba wa ukodishwaji wa ardhi kwa kampuni ya
Leisure Corp. (Al Nakheel) kwa mujibu wa kifungu cha 48 cha Sheria ya Matumizi
ya Ardhi ya mwaka 1992, Wizara ilishindwa kuipatia Kamati kielelezo hicho.
Hivyo, Kamati inapendekeza kuwa masharti ya Sheria ya Matumizi
ya Ardhi ya mwaka 1992 chini ya kifungu cha 48 yazingatiwe. Kifungu hicho
kinapiga marufuku kufuta mkataba wa ukodishaji isipokuwa kwa masharti
yaliyotajwa katika kifungu hicho ambayo yanajumuisha utoaji wa notisi ya miezi
mitatu ili kumpa nafasi aliyepewa mkataba huo kurekebisha kasoro iliyojitokeza.
Aidha baada ya Kampuni hiyo ya Leisure Corp kufutiwa
mkataba wa ukodishwaji wa ardhi, eneo hilo liligawanywa katika maeneo matano
ambapo makampuni mengine matatu yalipatiwa mikataba ya ukodishwaji kwa eneo
hilo na watu wawili walipatiwa hati za matumizi ya ardhi.
Hata hivyo, Wizara ilikiri kuwa makampuni hayo
yalifutiwa kutokana na miradi yao kutopitia na kuridhiwa na Mamlaka ya
Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) kwa mujibu wa kifungu cha 46(3) cha
Sheria ya Matumizi ya Ardhi ya mwaka 1992.
Kifungu hicho kinampa mamlaka Waziri anayeshughulikia
ardhi kukodisha ardhi baada ya mradi kuridhiwa na ZIPA. Aidha Wizara ilifuta
hati hizo za matumizi ya ardhi katika eneo hilo kutokana na eneo hilo kutengwa
kwa ajili ya uwekezaji na hivyo kustahili kutolewa kwa kupitia mikataba ya
ukodishwaji na si hati ya matumizi ya ardhi. Hivyo Kamati inapendekeza kufuatwa
kwa masharti ya sheria katika utoaji wa mikataba ya ukodishwaji wa ardhi.
1. Kadhia
ya Sovereign Sands Resort
Namna ilivyoshughulikiwa na
Kamati.
Kadhia hii pia ilielezwa katika kikao cha Baraza na
Mjumbe wa Baraza Mhe. Hamza Hassan Juma. Kamati ilipata fursa ya kuzungumza na
Mjumbe ambaye aliieleza Kamati kuwa Kampuni ya Sovereign ambayo kiwango chake
cha malipo kwa mwaka ni dola za Kimarekani 13,365 ilifutiwa hati ya ukodishaji
wa eneo hilo na badala yake kupatiwa Kampuni ya The Address ambayo ilitakiwa
kulipa Dola za Kimarekani 3,000.
Mjumbe aliwasilisha nakala ya bili ya malipo ya
Kampuni ya Sovereign kwa mwaka 2011 ambayo ni US $ 13,365 pamoja na nakala ya
hati ya kukodishwa kwa kampuni ya The Address katika eneo hilo hilo baada ya
kufutiwa hati ya ukodishaji kampuni ya Sovereign Sand ambapo kampuni hiyo ya
the Address inapaswa kulipa US $ 3,000. Nakala
ya bili ya malipo ya kampuni hiyo inaambatanishwa kama Kiambatanisho Nam KTA
14.
Wizara ya Ardhi iliieleza Kamati kuwa kampuni ya
Sovereign Sands ilifutiwa hati ya kukodisha eneo hilo kwa kutoliendeleza kwa
kipindi cha zaidi ya miaka minne toka ilipokodishwa mwaka 2006.
Wizara iliwasilisha nakala za hati ya kukodishwa eneo
kwa Kampuni ya Sovereign Sands iliyotolewa tarehe 07 Novemba, 2006, barua ya
notisi ya miezi mitatu ya kufuta eneo hilo iliyotolewa tarehe 31/10/2011 na
nakala ya kufuta hati ya ukodishaji wa eneo hilo kwa kampuni ya Sovereign Sands
iliyotolewa tarehe 01/02/2012. Nakala hizo zinaambatanishwa na ripoti hii kama Kiambatanisho nam KTA 15.
Kamati pia ilipokea nakala ya mkataba wa ukodishwaji
wa ardhi kwa kampuni ya The Address iliyotolewa tarehe 28/02/2012. Hati hiyo
inaambatanishwa na ripoti hii kama kiambatanisho
namba KTA 16.
Hata hivyo, kamati iliandikia Ofisi ya Wakala wa
Usajili wa Biashara na Mali Zanzibar ili kuthibitisha usajili wa Kampuni hiyo
ya The Address, Ofisi hiyo iliipatia kamati nakala ya hati ya usajili wa
kampuni hiyo ambayo inaonyesha kuwa ilisajiliwa tarehe 11 April, 2012. Nakala
ya hati ya usajili inaambatanishwa pamoja na ripoti hii kama kiambatanisho namba KTA 17.
MAONI YA KAMATI
Katika kadhia
hii kamati ilipatiwa nakala ya notisi ya miezi mitatu kwa mujibu wa sheria kwa
kampuni ya Sovereign Sands Resort kabla ya kampuni hiyo kufutiwa mkataba wa
ukodishwaji wa ardhi.
Notisi hiyo
inaonyesha kuwa ilitolewa tarehe 31/10/2011 ambapo kampuni hiyo ilifutiwa rasmi
mkataba huo tarehe 1/2/2012. Hivyo, kwa mujibu wa vielelezo hivyo, Kamati
imebaini kuwa utaratibu huu wa kisheria wa kutoa notisi kabla ya kufuta mkataba
wa ukodishwaji wa ardhi ulizingatiwa.
Kamati imebaini
kuwa kwa mujibu wa mkataba, kampuni hii ya Sovereign Sands Resort ilikodishwa
eneo hilo tarehe 7/11/2006 na hivyo kutakiwa kwa mujibu wa sheria ya matumizi
ya ardhi kuliendeleza eneo hilo ndani ya miezi 30 iliyomalizika mwezi Mei,
2009.
Hata hivyo,
Kamati ilipata nakala ya risiti ya malipo ya kodi ambayo Kampuni hiyo imelipa
kwa Mamlaka ya Mapato Zanzibar, kodi ambayo ililipwa mwezi Novemba, 2010 na
ilikuwa inamalizika mwezi Juni, 2011, kipindi ambacho mwekezaji alishapindukia
muda uliotajwa kwa mujibu wa sheria wa kuendeleza eneo hilo.
Kamati
inapendekeza kuwa kuwepo na uratibu mzuri baina ya taasisi za Serikali ili
inapotekezea ukiukwaji wa masharti ya Sheria
kwa upande wa mwekezaji, taasisi inayohusika na ukusanyaji wa mapato
isikusanye kodi hiyo kutoka kwa kampuni ambayo imekiuka utaratibu uliowekwa na
sheria na hatua za kutoa notisi zichukuliwe haraka na hatimaye kufanya maamuzi
ya kufuta endapo kasoro iliyojitokeza haikurekebishwa.
Kutokana na
uthibitisho kutoka Ofisi ya Wakala wa Usajili na Mali kamati imebaini kuwa
ukodishwaji wa ardhi kwa Kampuni ya The Address haukuwa sahihi kutokana na
kampuni hiyo kukodishwa ardhi siku 42 kabla ya kuwepo kwake kisheria kwa maana
kupata usajili.
Kamati imebaini kuwepo kwa kasoro katika ukodishwaji
wa eneo hilo na inapendekeza kuwa ukodishwaji wa eneo hilo uzingatie masharti
ya sheria kama yalivyoelezwa katika Sheria ya Matumizi ya Ardhi na Sheria ya
ZIPA.
1. Kadhia
ya SAGO
Namna ilivyoshughulikiwa na
Kamati.
Katika kadhia hii, kamati ilibaini kuwepo kwa maelezo
yaliyotolewa na Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kama
yalivyoanishwa katika hansard ya tarehe 13 Julai, 2012, ukurasa wa 75 kuwa
suala linalohusu kadhia hii, Kampuni ya SAGO PALM, imefungua kesi katika
mahakama ya Ardhi dhidi ya Kampuni ya
Coconut Resorts and Villa.
Hivyo kamati iliandikia Mahakama ya Ardhi ili
kuthibitisha kuwepo kwa kesi hiyo katika mahakama hiyo. Mahakama hiyo ilijibu
barua ya kamati na kuijulisha kuwa kesi hiyo ilifunguliwa katika mahakama hiyo
na baadae kufunguliwa shauri hilo katika Mahakama Kuu ya Zanzibar baada ya
kuunganishwa katika kesi hiyo Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, na Waziri wa Ardhi,
Makaazi, Maji na Nishati. Barua hiyo kutoka mahakama ya Ardhi inaambatanishwa
na ripoti hii kama kiambatanisho namba
KTA 18.
Kamati ililazimika kusita katika kuishughulikia kadhia
hii kutokana na masharti ya kanuni ya 108 (17) ya kanuni za kudumu za Baraza la
Wawakilishi, toleo la mwaka 2012, kuamuru kamati kutoshughulikia jambo lolote
linalosubiri uamuzi wa mahakama.
MAONI YA KAMATI
Kamati ilisita kuchunguza kadhia hii baada ya kugundua
kuwepo kwa shauri mahakamani
1. Kadhia
ya Nyumba za Mazizini
Namna ilivyoshughulikiwa na
Kamati.
Kadhia hii ipo katika nyumba iliyopo katika kiwanja
walichopewa Ubalozi wa Oman hapo Mazizini. Kamati ilimwalika Mjumbe wa Baraza
aliyetoa hoja ndani ya kikao cha Baraza Mhe. Mohammedraza Hassanali ambaye
aliieleza Kamati kuwa ubalozi wa Oman ulipatiwa eneo lililopo katika nyumba
hizo za Mazizini lakini ubalozi huo umeshindwa kulitumia eneo hilo kutokana na
kuwepo kwa wapangaji jambo ambalo halileti picha nzuri kwa serikali.
Kadhia hii ilianza mwaka 2009 baada ya Serikali
kukodisha eneo hilo kwa ubalozi wa Oman. Nakala ya barua ya makubaliano ya
ukodishaji eneo hilo inaambatanishwa na ripoti hii kuwa kiambatanisho namba KTA 19.
Kamati
ilitembelea eneo hilo na wapangaji hao wa familia mbili za Bi. Fatma Salum Nassor
na Bw. Makame A. Muhajir walieleza kamati kuwa wapo tayari kuhama nyumba hiyo
iwapo watapatiwa makaazi mbadala.Wizara ilieleza kuwa imeanza na inaendelea
kuchukua hatua ili kuwahamisha wapangaji hao.
Wakati
Kamati ikiendelea kuifanyiakazi kadhia hii, Wizara kupitia Idara ya Nyumba
iliieleza Kamati kuwa iliwapa notisi ya kuhama wapangaji wa familia mbili
katika nyumba hiyo kwa barua ya tarehe 6/3/2012 kwa Bi. Fatma Salum Nassor
ambaye alijibu kwa barua ya tarehe 22/3/2012 akiomba kupatiwa makaazi mbadala
na familia yake.
Wizara iliandika barua nyengine ya msisitizo
wa kuwataka wapangaji hao wahame ya tarehe 27/3/2012. Barua hizo zinaambatanishwa pamoja na ripoti hii kama kiambatanisho namba 20.
Hata
hivyo, Wizara ilifanya jitihada ya kuwapatia wapangaji wote wawili makaazi
mbadala katika Block nambari 10, Michenzani ambapo:-
i.
Mpangaji wa kwanza Bi. Fatma Salum Nassor alipewa nyumba nambari 10/23,
Michenzani, nakala ya barua ya tarehe 21/12/2012.
ii.
Mpangaji wa pili, Bw. Muhajir, amepewa nyumba nambari 10/22, Michenzani kwa
barua ya tarehe 08/01/2013. Barua hizo zinaambatanishwa na ripoti hii kama kiambatanisho namba KTA 21.
Aidha
kamati iliarifiwa kwa barua ya tarehe 26/2/2013, kutoka Idara ya nyumba kuwa
tayari ubalozi wa Oman umeshakabidhiwa nyumba hiyo baada ya kuwatoa wapangaji
waliokuwamo.
Idara
hiyo iliwasilisha nakala ya barua hiyo kwa kamati na inaambatanishwa na ripoti
hii kama kiambatanisho namba KTA 22.
MAONI YA KAMATI
Muda mrefu umepita tangu Serikali ifanye uamuzi wa
kuupatia ubalozi wa Oman kiwanja kwa ajili ya kujenga ubalozi wake. Suala hili
limeanzia mnamo tarehe 6 Mei 2009 wakati mkataba wa ukodishwaji wa eneo hilo
ulipofungwa baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Ubalozi wa Oman hapa
Zanzibar.
Kwa kipindi chote hicho, tokea mwaka 2009 hadi kufikia
mwaka 2013 wizara imeshindwa kusimamia uamuzi huo wa kulikabidhi eneo hilo kwa
ubalozi wa Oman kwa kushindwa kuwahamisha wapangaji waliomo katika nyumba
No.12, iliyopo katika kiwanja hicho.
Kamati ilihoji sababu za kutotekelezwa kwa kwa maamuzi
hayo ambapo sababu kubwa iliyoelezwa ni kwa wapangaji wa nyumba hiyo kutokuwa
na makazi mbadala.
Kutokana na maelezo hayo, Kamati ilihoji kwa nini Wizara
haikuchukua jitihada za kuwapatia maeneo mengine ya kuwakodisha wapangaji hao
kama vile nyumba za maendeleo za Michenzani ili kuweza kutekeleza maamuzi
yaliyopitishwa ya kuukodisha eneo hilo Ubalozi wa Oman.
Kutokana na msukumo huo wa Kamati, Wizara iliweza
kuwahamisha wapangaji hao na kuwapatia makazi wapangaji hao katika nyumba hizo
za Michenzani na kulikabidhi rasmi eneo hilo kwa Ubalozi wa Oman.
1. Kadhia
ya Kisiwa cha Kwale
Namna ilivyoshughulikiwa na
Kamati.
Katika kuishughulikia hoja hii, Kamati iliwaalika
watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambao waliieleza Kamati kuwa Kisiwa cha
Kwale ni miongoni mwa maeneo yaliyopo chini ya hifadhi ya Ghuba ya Menai. Eneo
la kisiwa hiki lilikodishwa baada ya mashauriano mbalimbali kufanyika baina ya
taasisi za Serikali na kampuni ya The Rihla kwa hati ya ukodishwaji inayonyesha
kuwa kampuni hiyo imekodishwa eneo hilo kwa muda wa miaka 33.
Hati ya
ukodishwaji eneo hilo inaambatanishwa na ripoti hii kama kiambatanisho namba KTA 23.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliipatia kamati vielelezo vinavyoonyesha
mawasilianao ya Kitaasisi na vielelezo hivyo vinaambatanishwa na ripoti hii
kama kiambatanisho KTA 24. Vielelezo
vya mradi huo vinaambatanishwa pamoja na ripoti hii kama kiambatanisho namba KTA 25.
Wizara
ya Mifugo na Uvuvi inatarajia kuingia katika Makubaliano na Kampuni ya the
Rihla (Memorandum of Understanding) baada ya kukamilika kwa utafiti wa
kimazingira (Environment Impact Assessment) ambao hivi sasa upo katika ngazi ya
Idara ya Mazingira.
MAONI YA KAMATI
Kamati inapendekeza kuwa taasisi
zinazohusika katika suala hili ziharakishe katika kuchukua hatua ili kulimaliza
suala hili kwa manufaa ya nchi.
1. Kadhia
ya Sunset Paradise Resort
Namna ilivyoshughulikiwa na
Kamati.
Kamati ilimualika Mjumbe aliyetoa hoja hii katika
mkutano wa Bajeti wa Baraza wa mwaka 2012/2013 Mheshimiwa Hamza Hassan Juma
ambaye aliieleza Kamati kuwa Kampuni ya Sun Set Paradise ilikodishwa ardhi eneo
la Kama kwa hati ya ukodishwaji ambayo inaambatanishwa na ripoti hii kama kiambatanisho namba KTA 26. Kwa mujibu
wa mkataba huu Kampuni hiyo inalipa kodi ya dola za Kimarekani 39,000 na
Mheshimiwa aliwasilisha nakala ya bili ya kodi ya ardhi inayoonyesha kiasi
hicho ambayo inaambatanishwa na ripoti hii kama Kiambatanisho nam. KTA 27.
Aidha Mjumbe
huyo aliwasilisha nakala ya kibali cha ujenzi kwa Kampuni hiyo kilichotolewa
tarehe 21/12/2010 ambayo inaambatanishwa na Ripoti hii kama Kiambatanisho nam. KTA 28.
Mjumbe
aliieleza Kamati kuwa tarehe 7 Machi, 2011, Kampuni hiyo ilifutiwa hati ya ukodishaji
ardhi bila ya kupewa notisi kwa Kampuni hiyo kama Sheria ya Matumizi ya Ardhi
ya Mwaka 1992 inavyoelekeza.
Mjumbe
pia aliieleza Kamati kuwa baada ya kufutwa kwa hati ya ukodishaji kwa Kampuni
ya Sunset, eneo hilo lilikodishwa kwa Kampuni ya Sea Rock Resort Ltd kwa kodi
ya Dola za Kimarekani 2,500.
Wizara iliieleza Kamati kuwa Kampuni ya Sunset
ilifutiwa hati ya ukodishaji ardhi kutokana na kushindwa kuliendeleza eneo hilo
ndani ya kipindi cha zaidi ya miaka mitatu. Aidha Wizara iliwasilisha nakala ya
barua ya ufutaji huo na mikataba ya ukodishwaji mbele ya kamati na nakala hizo
zinaambatanishwa na ripoti hii kama Kiambatanisho nam KTA 29.
MAONI YA KAMATI
Kamati ilihitaji kupatiwa notisi kabla
ya kufutwa kwa mkataba wa ukodishwaji wa ardhi kwa kampuni ya Sun Set Paradise
lakini Wizara inayoshughulikia ardhi ilishindwa kuipatia Kamati nakala ya
notisi hiyo hadi wakati wa kuwasilisha ripoti hii. Utaratibu huu wa kutoa
notisi ni kwa mujibu wa matakwa ya kifungu cha 48(3) ambacho kinataka kabla ya
waziri kufuta hati ya ukodishwaji wa ardhi, mwenye hati hiyo apatiwe notisi ya
miezi mitatu ya kurekebisha jambo ambalo litapelekea kufutiwa kwake mkataba wa
ukodishwaji wa ardhi.
Kamati inashauri kuwa kwa vile utaratibu
wa kufuta hati ya matumizi ya ardhi ni wa kisheria, basi ufutaji huo wa mkataba
wa ukodishaji wa eneo hilo ufuate masharti ya Sheria.
Aidha Kamati imebaini kuwa hakuna
‘’fomula’’ maalum ya malipo ya kodi ya ardhi kwa wawekezaji kinyume na
inavyodaiwa na Wizara inayoshughulika na ardhi.
Katika taarifa yake kwa Kamati, Wizara
hiyo inadai kuwa mwekezaji Mzalendo kikawaida hupaswa kulipa Dola za Kimarekani
500 kwa hekta moja kwa mwaka. Kwa mfano, katika kadhia hii, na nyengine katika
ripoti hii, inaonyesha kinyume chake. Kampuni ya Sea Rock Ltd iliyopewa eneo
walilofutiwa Sun Set Paradise, wanalipa dola za Kimarekani 3000 kwa hekta 8.20,
wakati kwa kiwango kilichotajwa na Wizara, wengetakiwa kulipa kiasi cha dola
4100.
Zipo pia kampuni ambazo zimekodishwa kwa
viwango tofauti licha ya kupewa maeneo yenye ukubwa unaofanana, mfano hekta
2.57 zimekodishwa kwa dola za kimarekani 3000 na nyengine hekta hizo hizo kwa
dola 5000.
Kamati inapendekeza kuwepo kwa mpango maalumu wa
kuweka viwango vya kodi ya ardhi kwa kushirikiana na Waziri mwenye dhamana na mambo
ya Fedha, vitakavyowekwa kwa uwazi ili vifahamike kwa urahisi na mwekezaji au
mwanachi yeyote.
1. Kadhia
ya Bruno Conti
Namna ilivyoshughulikiwa na
Kamati
Kamati ilipata maelezo kutoka Wizara ya Ardhi,
Makaazi, Maji na Nishati kuwa Mnamo tarehe 04/08/2000 Bw. Bruno Conti
alikodishwa eneo la ardhi lililopo Uroa kwa muda wa miaka 33 kwa hati yenye
nambari ya usajili DP 431/2000 ambayo inatolewa kama sehemu ya ripoti hii, Kiambatanisho nam. KTA 30.
Eneo hilo lenye ukubwa wa Hekta 0.39 lilikodishwa kwa
madhumuni ya Ujenzi wa ofisi na makaazi kwa kodi ya ardhi ya Dola za Kimarekani
mia saba na themanini (USD 780).
Mbali na maelezo hayo, Kamati ilipata maelezo ya
upande wa pili wa kadhia hii kupitia Mheshimiwa Hamza Hassan Juma. Mheshimiwa
Hamza aliikabidhi Kamati vielelezo mbali mbali vya Bw. Bruno Conte ikiwamo
barua ya malalamiko kupitia Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar kwenda kwa
Makamo wa Pili wa Rais.
Katika barua hiyo ya tarehe 16/08/2011 ambayo kamati
inaitumia kuwa sehemu ya ripoti yake na kuwa Kiambatanisho nam. KTA 31, Bw. Bruno anaeleza kadhia nzima ya
kufutiwa eneo lake.
Bw.Bruno ameeleza kuwa taratibu zote za kufuta Mkataba
zimefanywa siri, kinyume na sheria wala yeye hakujulishwa. Kwa maelezo ya barua
hiyo, wakati Wizara ikidai kuwa mkataba wa ukodishwaji ulifutwa tarehe
13/06/2011, kamati imepata barua ya tarehe 6/06/2011 iliyofuta mkataba wa
ukodishwaji wa eneo hilo ambayo imetolewa na aliyekuwa Waziri wa Ardhi,
Makaazi, Maji na Nishati, Mheshimiwa Ali Juma Shamuhuna, (kiambatanisho nam. KTA 32).
Kwa mujibu wa maelezo ya Wizara ya Ardhi, Makaazi,
Maji na Nishati, eneo hilo alilofutiwa Bw. Bruno, amepewa Bw. Said Ali Juma
Shamuhuna. (tafadhali rejea
kiambatanisho namba 11 katika ukurasa wa 16)
Bw. Bruno katika barua yake kwa Makamo wa Pili wa Rais,
kupitia kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar anaeleza kwamba, mnamo tarehe
13/06/2011 watu wasiojulikana walivamia eneo hilo na kuanza kuvunja ukuta wa
fensi, ghala pamoja na vitu kadhaa ambavyo mpaka leo havijulikani vilipo.
Aidha ilielezwa kuwa, wakati hayo yote yanafanyika
siyo Bwana Bruno wala Mwakilishi wake Bw. Mzee Mwinyi (kwa hati ya uwakala
inayoambatanishwa KTA 33) walipewa
taarifa (notisi) ya hatuwa yoyote inayoendelea. Siyo sheha wala Ofisi ya
Halmashauri iliyokuwa na taarifa ya uvunjwaji na ujenzi mpya uliokuwa
unaendelea.
Kutokana vielelezo vya Bw. Bruno Conte, wakati Wizara
ikidai kumfutia Mkataba wa ardhi wa eneo lake kwa madai ya kutoliendeleza na
kulitelekeza eneo hilo, Bw. Conte ameonyesha kuwa ameliendeleza eneo hilo isipokuwa
alivunjiwa majengo aliyoyaendeleza. Aidha kamati ilipatiwa kielelezo
kinachoonesha kuwa Bw. Bruno alikuwa akilipa kodi ya ardhi Serikalini na
kielelezo hicho kinaambatanishwa kama kiambatanisho namba KTA 34.
MAONI YA KAMATI
Katika kadhia hii, Kamati ilitaka
kupatiwa vielelezo kadhaa ikiwemo nakala ya notisi ya kufuta mkataba wa
ukodishwaji kutoka wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati lakini hata hivyo
hadi wakati wa kuwasilisha ripoti hii, Wizara ilishindwa kuipatia Kamati
kielelezo hicho.
Aidha Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na
Nishati iliieleza Kamati kuwa eneo hilo baada ya kufutiwa mkataba wa
ukodishwaji Kampuni ya Bruno Conti, alipatiwa Ndg. Said Ali Juma Shamuhuna kwa
hati ya matumizi ya Ardhi.
Kamati iliagiza kupatiwa vielelezo
vyenye kuonyesha uhalali wa matumizi ya haki ya matumizi ya ardhi kwa Ndg. Said
Ali Juma Shamuhuna pamoja na nyaraka nyengine zilizotumika katika hatua za
uombaji na hadi kupewa eneo hilo Ndg. Said Ali Juma Shamuhuna. Hata hivyo
pamoja na jitihada za Kamati kufuatilia kwa mazungumzo na viongozi wa wizara na
hata kwa kuiandikia wizara barua mara kadhaa kuhusu vielelezo hivyo, wizara
ilishindwa kuipatia Kamati vielelezo hivyo.
HADIDU REJEA NAM 2
Maeneo ambayo yalikuwa yanatumiwa na wananchi kwa
shughuli zao za kuendesha maisha, lakini yamechukuliwa bila ya kuzingatia
maslahi ya wananchi waliokuwa wanayatumia
Namna ilivyoshughulikiwa na
Kamati
Katika Hadidu Rejea hii, Kamati baada ya kupitia
taarifa ya Hansard wakati wa Mkutano wa Bajeti wa mwaka wa fedha 2012/2013,
iliainisha maeneo ya Kijichi, Selem na Dole kuwa ni miongoni mwa maeneo ambayo
yalikuwa yanatumiwa na wananchi kuendesha maisha na kuchukuliwa bila ya
kuzingatia maslahi ya waliokuwa wanayatumia.
Wizara imeieleza Kamati kuwa kutokana na kuwepo kwa
mgogoro katika maeneo hayo, suala hilo limeundiwa Kamati inayohusisha Makatibu
Wakuu watatu kutoka Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Wizara ya Ardhi, Makaazi,
Maji na Nishati na Wizara ya Kilimo na Maliasili. Kamati hiyo ya Makatibu Wakuu
imemaliza kazi yake kwa upande wa Kijichi Nguruweni na kazi ya kugawa ardhi kwa
wakulima kwa eneo hilo imefanyika kwa kiasi kikubwa.
Kamati Teule iliomba kupatiwa ripoti inayohusu
wakulima wa eneo hilo kupatiwa maeneo hayo pamoja na orodha ya wananchi
waliopewa maeneo hayo. Hata hivyo hadi wakati wa kuwasilisha ripoti hii, Wizara
ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati ilishindwa kuwasilisha vielelezo hivyo mbele
ya kamati.
Hata hivyo, kwa maeneo ya Selem na Dole Ndunduke,
Kamati ilibaini kuwa zoezi hilo bado halijakamilika.
MAONI YA KAMATI
Kamati inapendekeza kuharakishwa kwa hatua za kutatua
mgogoro uliopo katika maeneo hayo na hatimae kuwapatia wananchi wanaostahili
haki ya kutumia maeneo hayo.
HADIDU REJEA NAM. 3
Wawekezaji wanaochimba mchanga kwenye maeneo ya fukwe.
Namna ilivyoshughulikiwa na
Kamati
Katika kadhia hii, Kamati ilielezwa kuwa msingi wa
tatizo hilo ni ujenzi wa jeti unaokusudiwa kufanywa na Hoteli ya Palumbo
iliyopo huko Uroa na matumizi ya fukwe kwa wageni wa hoteli hiyo.
Suala hilo ambalo limejadiliwa kwa pamoja baina ya
taasisi mbali mbali za serikali zikiwemo Afisi ya Mkuu wa Wilaya, Idara za
Ardhi, Idara ya Mazingira na Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais na kukubaliana juu
ya haja ya kufanya Uchambuzi wa Kimazingira (EIA) utakaotoa mwelekeo wa
kukubaliwa au kukataliwa kwa ujenzi wa jeti baada ya kwanza kufanya utafiti
katika jamii inayozunguka kuona namna wanavyopokea suala hilo.
MAONI YA KAMATI
Kamati inakubaliana na uamuzi wa kuwashirikisha
wananchi katika kufikia maamuzi juu ya namna ya kulishughulikia suala hilo na
hatimaye kufanya Uchambuzi wa Athari za Kimazingira na inapendekeza kuwa mambo
hayo yaharakishwe ili kuondosha mgogoro huo.
HADIDU REJEA NAM. 4
Mgogoro wa Ardhi baina ya serikali na wananchi
(wakulima), Bambi
Namna ilivyoshughulikiwa na
Kamati
Kamati Teule ilikutana na watu mbali mbali
wanaohusika na hoja hii akiwemo Mh. Hamza Hassan Juma, Mjumbe wa Baraza la
Wawakilishi ambaye aliibua hoja hii ndani ya Baraza la Wawakilishi. Kamati
pia ilifanya ziara katika bonde la Matora Bambi ambapo iliambatana na Mkuu wa
Wilaya ya Kati, Mkurugenzi wa Ardhi na wasaidizi wao.
Kamati ilipata maelezo kutoka kwa wakulima
wanaolitumia bonde hilo ambao walieleza kuwa wamekuwa wakilitumia eneo hilo
kwa muda mrefu katika shughuli za kilimo na ufugaji na kwamba
hawakushirikishwa katika hatua za awali katika maamuzi ya kulitumia eneo hilo
kwa shughuli za uwekezaji wa ufugaji wa ng’ombe kwa ajili ya kiwanda cha
maziwa kiitwacho Zanzibar Dairy Products.
Watendaji wa Wizara ya Ardhi walieleza kuwa walipewa
kazi ya kulipima Bonde la Matora na wakulima wa eneo hilo waliwazuia
watendaji hao kufanya shughuli hiyo kwa kupinga kuchukuliwa kwa eneo hilo.
Baada ya hatua hiyo, Kamati ilielezwa kuwa timu ya mawaziri watatu wa
serikali ilifika Bambi ili kuwanasihi wakulima hao kukubali eneo hilo kupewa
mwekezaji. Mawaziri hao ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo.
Wakulima hao
hawakuridhika hasa kutokana na kulitegemea bonde hilo la Bambi kwa ajili ya
shughuli za kujitafutia maisha yao na kwamba kumpatia mwekezaji eneo hilo
kungewaathiri kimaisha. Pamoja na mawaziri hao kuwaahidi wakulima kuwa
uwekezaji huo ungewapatia ajira wakulima hao, wananchi hawakuridhika kutokana
na kutohakikishiwa kama wakulima wote wa bonde hilo wangepatiwa ajira
kutokana na uwekezaji huo.
Aidha Kamati ilijulishwa kuwa Serikali katika ngazi
ya masheha na Mkuu wa Wilaya hawakushirikishwa katika hatua za awali juu ya
kubadili matumizi ya bonde hilo kutoka kwa wananchi na kumpatia mwekezaji kwa
ajili ya mradi huo.
|
Hata hivyo Kamati ilielezwa na Wizara ya Ardhi kuwa
katika ngazi ya Wizara hiyo, wameishauri serikali kuwa mradi huo usiendelee
tena katika eneo hilo.
MAONI YA KAMATI
Ingawa eneo hilo la bonde la Matora ni
la Serikali lakini bado hakukuwa na utaratibu wa uwazi wa kulihamisha matumizi
yake kutoka kilimo kwenda kwenye uwekezaji wa mifugo kwa kuipatia Kampuni ya
Zanzibar Diary Products. Taasisi zinazohusika na uwekezaji hazikushiriki
kikamilifu katika kusimamia mradi huu wa uwekezaji badala yake sehemu kubwa ya
uwekezaji huu imeratibiwa na Serikali kuu.
Pamoja na jitihada za Mawaziri watatu
ambao ni waziri anayeshughulikia masuala ya fedha, waziri anayeshughulikia
masuala ya ardhi na waziri katika Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi katika kuwashauri wananchi kuhusu mradi huo, jitihada hizo
hazifanikiwa.
Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ilipoitwa
kueleza ushiriki wake katika suala hili, ilieleza kuwa haifahamu kwa kina suala
hilo kutokana na kutoshirikishwa kikamilifu.
Kamati inapendekeza kuwa Serikali
ichukue hatua za kulimaliza tatizo hilo kwa kushirikiana na taasisi mbali mbali
zikiwemo ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kati na ZIPA kwa ajili ya manufaa ya
wananchi.
HADIDU
REJEA NAM. 5
Mgogoro wa Ardhi baina ya mfanyabiashara
na wakulima, Tumbe.
Namna
ilivyoshughulikiwa na Kamati
Sehemu ya kwanza ya mgogoro huu inahusu wananchi wa
Kijiji cha Kijichame, Tumbe, ambao walikuwa wakilima maeneo ya mashamba ya
serikali ambayo serikali imeyapima viwanja bila ya wao kupatiwa viwanja hivyo.
Kamati ilipata maelezo ya Mjumbe wa Baraza aliyeiibua
hoja hii ndani ya Baraza, Mheshimiwa Rufai Said Rufai wa Jimbo la Tume ambaye
aliieleza Kamati kuwa Idara ya Ardhi ililipima eneo lililokuwa likitumiwa na
wananchi wa Chwaka, Tumbe linalowahusu wananchi wa Kijichame. Aidha Mjumbe huyo
wa Baraza aliendelea kuieleza Kamati kuwa eneo hilo lilipimwa bila ya kuwapa
taarifa wananchi waliokuwa wanayatumia maeneo hayo kwa muda mrefu.
Mjumbe huyo pia aliieleza Kamati kuwa mwaka 2010,
Kamati ya Mawasiliano ya Baraza la Wawakilishi ilitembelea eneo hilo na kutoa
agizo kuwa wananchi waliokuwa wanalitumia eneo hilo wapatiwe asilimia 70 ya
eneo lililopimwa na kueleza kuwa Wizara ilikubali kuwapatia wananchi sehemu ya
eneo hilo
Kamati ilipewa orodha ya watu waliopewa maeneo huko
ambao ndani yake wamo viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mikoa miwili
ya Pemba, Maafisa Wadhamini, Maafisa Tawala Wilaya na Mikoa, Pemba, Wakuu wa
Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu wa Mabaraza ya Mji na Halmashauri, Pemba,
Wajumbe wa Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi na watu wengine mbali mbali ambao
orodha yao inaambatanishwa na ripoti hii kama Kiambatanisho Nam. KTA 34A
Kamati ilielezwa kuwa baada ya wananchi hao
kulalamika, Wizara ya Ardhi ilikubali kukaa nao pamoja kuwasikiliza. Aidha
Kamati pia ilielezwa kuwa Idara ya Ardhi ilikubaliana na Kamati ya Mawasiliano
ya Ujenzi ya Baraza la Wawakilishi kutenga viwanja kwa ajili ya wananchi wa eneo
la Tumbe wakati wa maeneo hayo yatakapopimwa kwa awamu nyengine.
Kamati ilielezwa kuwa katika kikao hicho, Wizara ya
Ardhi iliongozwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo kwa wakati huo. Kutokana na
kikao hicho Idara ya Ardhi ilitoa barua ya tarehe 12/05/2010 ambayo
iliwahakikishia wananchi hao kutengewa asilimia 70% ya viwanja vitakavyopimwa
katika awamu ya pili. Barua hiyo pia iliwahakikishia wanakijiji hao kupata haki
ya fidia ya vipando vyao katika viwanja vilivyopimwa awamu ya mwanzo, isipokuwa
kwa wale tu waliopatiwa viwanja hivyo.
Aidha katika barua hiyo wananchi hao wamehakikishiwa
kupatiwa viwanja hivyo ndani ya siku 60 kuanzia tarehe ya barua hiyo. Nakala ya
barua hiyo ambayo kamati ya Mawasiano na Ujenzi ya Baraza la Wawakilishi
ilinakiliwa inaambatanishwa na ripoti hii kama kiambatanisho namba KTA 35.
Viwanja vyote vilivyopimwa katika awamu ya pili ni
109, ambapo viwanja 106 ni vya makaazi. Kamati Teule ilielezwa kuwa, Wanakijiji
wa Kijichame walitakiwa kupeleka orodha ya majina ya wanaohitaji kupatiwa
viwanja hivyo, orodha ilipelekwa na kuonekana na majina mengi kuliko idadi ya
viwanja vilivyopo na Idara iliirudisha orodha hiyo na kutaka orodha sahihi.
Orodha nyengine iliwasilishwa ambayo nayo ilionekana
kutokuwa na uhusiano wowote na ile orodha ya awali. Kwa mujibu wa Idara ya
Ardhi, hatimaye makubaliano yalifikiwa. Hata hivyo, utaratibu ulihitajika wa
wananchi hao kujaza fomu ya maombi, na vitambulisho vya ukaazi na Tsh.
200,000/= ambapo kwa mujibu wa maelezo ya Wizara wananchi wemeshindwa kukamilisha
kwa kushindwa malipo hayo.
Vile vile, wanakijiji hao walilalamika mbele ya Kamati
Teule kuwa maeneo wanayokusudiwa kupewa katika awamu ya pili ya viwanja hivyo
hayapo katika mazingira mazuri, ni maeneo ya maji maji na ujenzi wake ni mgumu
kwa watu wa kipato cha chini.
Kamati ilipatiwa nakala ya hati za matumizi ya ardhi
kwa watu mbali mbali ambayo imejumuisha viongozi mbali mbali. Nakala ya hati
hizo za matumizi ya ardhi pamoja na barua za kuombwa viwanja hivyo kwa viongozi
hao zinaambatishwa kwa pamoja kama kiambatanisho namba KTA 36.
Kwa kuwa baadhi ya nakala za hati za matumizi ya ardhi ambazo kamati
ilipatiwa hazikuwa na saini za waliopewa na baadhi saini za waliopewa
kutoonekana vizuri, kamati iliomba kupatiwa uthibitisho kutoka Wizara ya Ardhi,
endapo watu waliotajwa walipatiwa hati hizo.
Wizara ilithibitisha kuwa hati hizo zote zilichukuliwa
na wahusika waliopewa maeneo hayo na barua hiyo ya uthibitisho inaambatanishwa
na ripoti hii kama kiambatanisho namba KTA
37.
Sehemu ya pili ya mgogoro huu, unahusu wananchi wa
Tumbe, katika eneo la Mwanasoza kwa Mzigua, ambao wanadai kuwa Idara ya Ardhi,
imeyapima maeneo yao bila ya ridhaa yao na kuwapa watu wenye uwezo kujenga.
Wananchi hao wa Tumbe waliieleza Kamati
Teule kuwa ardhi hiyo ni yao tokea asili. Mkuu wa Idara ya Upimaji na Ramani,
aliieleza Kamati Teule kuwa wakati wakipima eneo hilo hakukuwahi kuwa na
malalamiko ya umiliki kwa kuwa ni shamba la Serikali.
MAONI
YA KAMATI
Kamati inashauri Wizara inayohusika na ardhi
kutekeleza majukumu yake kwa kuongozwa na sheria na kanuni.
Kamati inashauri kuwa ni vyema Wizara ikakutana na
wananchi wa maeneo hayo ya Tumbe na kusikiliza kilio chao na hatimaye kuwapa
haki ya kutumia maeneo hayo ambayo wamekuwa wakiyatumia kwa muda mrefu ili waendelee
na shughuli zao za kujiletea maendeleo.
HADIDU REJEA NAM. 6
Mgogoro wa maeneo ya ardhi ya wananchi
yaliyonyang’anywa na kufanywa vitega uchumi, Makangale.
Namna ilivyoshughulikiwa na
Kamati
Wakati kamati teule inafuatilia hadidu rejea hii
iliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini na watendaji wake, Watendaji wa Wizara
ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati na Mheshimiwa Rufai Said Rufai ambaye ndiye
aliyetowa hoja katika Mkutano wa Baraza.
Kamati ilipata maelezo kutoka kwa Mheshimiwa Rufai na
wananchi walalamikaji kuwa mgogoro huo umeanza tokea mwaka 2004 baada ya Idara
ya Ardhi kulipima eneo hilo, kwa nia ya kupewa mwekezaji, eneo ambalo wananchi
hao wanadai kulimiliki wakiwa na nyaraka ya umiliki.
Nakala ya nyaraka hiyo inayodaiwa kuthibitisha haki ya
walalamikaji juu ya eneo hilo inaambatanishwa na ripoti hii kama kiambatanisho
namba KTA 38. Kamati ilielezwa kuwa
wananchi hao walilalamika hatua ya kupimwa eneo hilo na malalamiko yao
waliyafikisha kwa Mkuu wa Wilaya ya Micheweni ambaye aliwaahidi kulitafutia
suluhu.
Kamati ilielezwa na walalamikaji kuwa Mkuu wa Wilaya
ya Micheweni aliwaahidi kuwa watalipwa Tsh. 15 milioni ambazo hawajalipwa mpaka
sasa. Wananchi hao wamesisitiza kuwa hawapo tayari kwa hivi sasa kupokea kiasi
hicho cha fedha kwa vile thamani yake imepunguwa tokea 2005 hadi hivi sasa.
Walichokuwa wanakitaka sasa ni kurejeshewa eneo lao ili wauze kwa bei muafaka
wanayoitaka.
Wizara ya Ardhi ilithibitisha kukodishwa eneo hilo kwa
kampuni ya Mpapindi Holiday and Diving Company tangu tarehe 24 Machi, 2004 na
kuipatia Kamati nakala ya Hati ya Makubaliano ya Ukodishaji wa eneo hilo ambayo
inaambatanishwa na ripoti hii kama Kiambatanisho
nam. KTA 39.
Hata hivyo Wizara ilithibitisha kuwa Kampuni hiyo
iliyokodishwa eneo hilo ambayo ilipaswa kulipa dola za Kimarekani 9,230 kwa
mwaka, toka mwaka 2007 haijawahi kulipa fedha hizo hadi sasa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Micheweni aliieleza
Kamati kuwa aliwahi kufanya mazungumzo na walalamikaji wa eneo hilo na
kukubaliana kuwa walalamikaji hao wamuachie mwekezaji huyo aendelee na shughuli
zake kwa ahadi ya walalamikaji hao kupatiwa TZS 15,000,000/- ambazo ZIPA
walielezwa kuwa wangesimamia upatikanaji wa fedha hizo. Mkuu wa Wilaya
aliwasilisha nakala ya barua walizowasiliana na taasisi za serikali katika
kadhia hiyo pamoja na kumbu kumbu za kikao cha pamoja na walalamikaji ambazo
kwa pamoja zinaambatanishwa na ripoti hii kama Kiambatanisho nam. KTA 40.
Aidha kamati ilipata nakala ya barua kutoka Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba iliyosainiwa tarehe 7 Machi, 2007 ambayo
ilimtaka Afisa Mdhamini wa ZIPA huko Pemba kusimamia upatikanaji wa haki za
walalamikaji kutoka kwa muekezaji. Barua hiyo inaambatanishwa na ripoti hii
kama kielelezo namba KTA 41.
Mnamo tarehe 18/9/2011 walalamikaji walimuandikia
barua Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kuwa bado hadi
wakati huo walikuwa hawajalipwa fidia hiyo. Nakala ya barua hiyo
inaambatanishwa na ripoti hii kama kiambatanisho namba KTA. 42.
MAONI YA KAMATI
Kwa mujibu wa kifungu cha 56 cha sheria ya Ardhi,
Waziri anaweza kufuta haki ya matumizi ya Ardhi. Isipokuwa katika ufutaji huo,
atapaswa kuzingatia masharti yafuatayo. Kwanza ni sharti kuwa ufutaji huo uwe
kwa maslahi ya umma na pili fidia kwa bei ya soko ilipwe.
Serikali kupitia ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Micheweni
na Mkoa wa kaskazini Pemba, ilikubali haki ya fidia kwa wananchi wa makangale
waliodai kuwa na haki katika eneo hilo, kutokana na kumbukumbu za kikao baina
ya Mkuu wa Wilaya na wananchi hao na pia kutokana na barua ya Mkuu wa Mkoa wa
Kaskazini, Pemba aliyomuandikia Afisa
Mdhamini wa ZIPA, Pemba kumtaka ofisi yake isimamie upatikanaji wa haki za
wananchi kutoka kwa muwekezaji.
Kamati inaamini kuwa Serikali ilipaswa kulipa fidia
kwa walalamikaji kwa wakati kama ambavyo walikubali suala la kuwalipa fidia kwa
kumbukumbu zilizotajwa hapo juu kama yalivyo masharti ya sheria.
Kuchelewa kulipa fidia kwa muda mrefu toka mwezi
Disemba, 2005 wakati walalamikaji walipokubaliana na serikali ya Wilaya,
kunapelekea uchocheaji wa migogoro ya ardhi isiyo ya lazima.
Ofisi ya Mkuu wa Wilaya baada ya kukubaliana na
walalamikaji, ilipaswa kusimamia kwa umakini makubaliano hayo kwa kuwasiliana
na mamlaka nyingine za serikali ili malipo hayo yafanyike kwa haraka.
Kamati inapendekeza kuwa Serikali ilipe fidia kwa
walalamikaji hao katika eneo la Makangale ili kumaliza mzozo huo na kwa kuwa
kiwango cha shilingi milioni kumi na tano (Tzs 15,000,000/-) kilikubalika mwaka
2005, takriban miaka minane iliyopita, ni vyema serikali ikafanya mapitio ya
kiwango hicho hasa kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 56 cha sheria ya
Ardhi kinachoelekeza fidia kulipwa kwa thamani ya soko (market value)
Aidha kamati inapendekeza marekebisho ya sheria ili
kuweka muda maalum wa kulipa fidia kwa mwananchi ambaye umiliki wa eneo
umefutwa kwa ajili ya maslahi ya umma ili kuepuka athari ya thamani ya fedha
kushuka kutokana na muda na hivyo kukaribisha mgogoro.
HADIDU REJEA NAM. 7
Mgogoro wa Ardhi kati ya wananchi na viongozi wa
serikali, Mchangamle, Kizimkazi
Namna ilivyoshughulikiwa na
Kamati
Kamati ilifuatilia hadidu rejea hii kwa kufika huko
Kizimkazi na kukutana na wananchi wa Mchangamle Kizimkazi.
Kamati ilipokea taarifa ya wananchi hao ambayo
hatimaye ilieleza kuwepo kwa kesi iliyofunguliwa mahakamani kuhusiana na kadhia
ya mgogoro huo baina ya wananchi na hoteli ya The Residence.
Kamati kupitia kwa Katibu wa Baraza la Wawakilishi,
iliandika barua Mahakama Kuu ya Zanzibar kutaka ufafanuzi kuhusu uwepo wa kesi
hiyo na hatua iliyofikia. Barua hiyo iliandikwa tarehe 12/02/2013.
Kamati Teule haikuweza kuendelea na hadidu rejea
ikisubiri majibu kutoka Mahakama Kuu kwa kuwa kwa mujibu wa Kanuni za Baraza la
Wawakilishi, toleo la mwaka 2012 chini ya kanuni ya 108(17), Kamati haipaswi
kushughikia suala linalosubiri maamuzi ya mahakama.
Mahakama Kuu ilijibu kwa barua ya tarehe 15/07/2013 na
kueleza kuwa kesi hiyo ilifunguliwa tarehe 24/11/2011 ambayo hata hivyo
ilifutwa tarehe 24/04/2013 kwa maombi ya Mdai. Barua hiyo ya Mahakama
inaambatanishwa na ripoti ya Kamati hii kama Kiambatanisho nam. KTA 43.
MAONI YA KAMATI
Kamati ilisita kushughulikia hadidu rejea hii kwa
mujibu wa masharti ya kanuni ya 108(17) ya Kanuni za Baraza la Wawakilishi,
Toleo la Mwaka 2012
HADIDU REJEA NAM. 8
Mgogoro wa Ardhi kati ya wananchi, Vitongoji Makaani.
Namna ilivyoshughulikiwa na
Kamati
Kamati ilifuatilia suala hili kwa kutembelea eneo la
Vitongoji Makaani na kukutana na wananchi wa eneo hilo pamoja na masheha wa
eneo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba,
Mkurugenzi wa Ardhi na Usajili, Afisa Mdhamini wa Wizara ya Ardhi, Makaazi,
Maji na Nishati na watendaji wengine wa Wizara hiyo.
Katika kikao hicho Kamati ilielezwa na wananchi wa
maeneo hayo kuwa kiini cha mgogoro huo ni maeneo waliyokuwa wakiyatumia kwa
shughuli za kilimo kuchukuliwa na kupimwa viwanja na kugaiwa makundi mbali
mbali wakiwemo wafanyabiashara, viongozi na watendaji wa serikali na wanasiasa
bila ya kuwazingatia wakaazi wa vitongoji ambao walikuwa wakiyatumia maeneo
hayo kabla ya ugawaji wa viwanja hivyo.
Aidha wananchi hao waliieleza Kamati kuwa baadhi ya
wananchi waliomba kupimiwa maeneo hayo kwa mujibu wa taratibu za maombi ya
viwanja lakini hawakujibiwa maombi yao na baadhi yao walilipa fedha kwa ajili
ya upimaji kupitia kwa sheha wa eneo ambazo zilielezwa kutofika katika wizara
inayohusika na ardhi. Hata hivyo Kamati ilielezwa kuwa sheha huyo tayari
alishafariki. Kamati ilitaka Wizara inayoshughulikia masuala ya Ardhi
kuwasilisha nakala za hati za matumizi ya ardhi zilizotolewa katika maeneo
hayo. Pamoja na vielelezo vyengine vinavyohusika katika zoezi la utoaji wa haki
ya matumizi ya ardhi.
Hata hivyo Wizara hiyo iliwasilisha fomu moja tu ya
maombi ya haki ya matumizi ya ardhi ya Bw. Seif Suleiman ambayo haikuwa imekamilika
kwa kuwa ilijazwa na Sheha pekee na haikuidhinishwa na taasisi za ardhi kama
inavyopaswa kufanywa kwa mujibu wa sheria.
Fomu hiyo ya maombi inaambatanishwa na ripoti hii kama
kiambatanisho namba KTA. 44.
Aidha katika fomu hiyo, Bw. Seif Suleiman alieleza
madhumuni ya kuomba eneo hilo ni ujenzi wa hoteli ya kitalii. Hata hivyo
hakukuwa na ushahidi wowote kuonyesha kuwa muombaji alipitia taratibu za sheria
za uwekezaji kama sheria ya Matumizi ya Ardhi chini ya kifungu cha 39(7).
Pamoja na kasoro hizo, muombaji alipewa haki ya matumizi ya eneo hilo.
Aidha eneo hilo la Vitongoji ambalo wizara ya Ardhi
iliithibitishia Kamati kuwa eneo la Vitongoji ni eneo lililopangwa kwa ajili ya
uwekezaji, lakini hata hivyo, miongoni mwa maeneo yaliyotolewa, maeneo matano
yalitolewa kwa ajili ya kilimo. Nakala za hati hizo zilizotolewa katika eneo
hilo zinaambatanishwa kwa pamoja kama kiambatanisho namba KTA. 45.
MAONI YA KAMATI
Sheria ya Matumizi ya Ardhi ya mwaka
1992 imeeleza kuwa Mzanzibari anaweza kupewa ardhi sehemu yoyote ndani ya
Zanzibar. Hata hivyo, sheria hiyo chini ya kifungu cha 39 imeweka masharti ya
Mzanzibari kupatiwa ardhi mbili tu za makaazi, ambapo ardhi moja atapatiwa
katika eneo alilozaliwa na nyengine ni ardhi ya makaazi mbali na eneo alilozaliwa.
Aidha Mzanzibari anastahili kupata ardhi
moja kwa ajili ya kilimo. Kamati pia inatambua kuwepo kwa haki kwa mzanzibari
kupatiwa ardhi kwa ajili ya matumizi ya biashara au shughuli za viwanda kwa
mujibu wa kifungu cha 39(3), (5) na (7). Hata hivyo kifungu cha 39(7) kinataka
eneo litakalotolewa kwa madhumuni ya biashara au shughuli za viwanda kufuata
utaratibu wa sheria inayohusika na uwekezaji.
Kamati imebaini kuwa baadhi ya watu
walipatiwa viwanja zaidi ya kimoja katika eneo hilo kwa madhumuni ya huduma.
Hata hivyo, Kamati ilipohoji matumizi ya viwanja hivyo vilivyotolewa kwa ajili
ya huduma, wizara haikuwa ikifahamu matumizi ya viwanja hivyo kwa kuwa ni
muombaji mmoja tu ndiye aliyejaza fomu kuomba eneo hilo kwa mujibu wa vielelezo
ambavyo wizara ya Ardhi iliviwasilisha mbele ya Kamati, hivyo kuonyesha kuwa
utaratibu wa sheria inayohusika na uwekezaji haukutekelezwa.
Kamati imebaini kuwa hatua hiyo ya
Wizara siyo sahihi kwa vile imekwenda kinyume na Sheria ya Matumizi Ardhi No.12
ya Mwaka 1992. Aidha viwanja vilivyotolewa katika eneo hilo la Vitongoji,
vimetolewa kwa madhumuni tofauti ambapo baadhi vimetolewa kwa matumizi ya
kilimo wakati eneo hilo limepangwa kwa ajili ya uwekezaji jambo ambalo ni
kinyume na utaratibu. Hivyo kutoa ardhi hiyo kwa matumizi ya kilimo na makaazi
ni kwenda kinyume na mpango uliowekwa.
Kamati inapendekeza kuwa wizara
inayoshughulikia masuala ya ardhi isimamie kwa dhati mipango ya miji na vijiji
kama inavyopangwa kwa mujibu wa sheria ili kuyaweka maeneo ya Zanzibar katika mpangilio
mzuri.
Kamati inapendekeza kuwa upimaji na
ugawaji wa maeneo ya ardhi ambapo tayari kumekuwa na manung’uniko kutoka kwa
wananchi, uzingatie masharti ya sheria ya ardhi ili kuepusha migogoro ya ardhi.
Aidha Kamati inashauri kuwepo mfumo
unaoeleweka wa upimaji na ugawaji wa viwanja utakaokuwa wa uwazi na haki
utakaowapa fursa wananchi wanaoshi maeneo yanayopimwa nao kupatiwa viwanja
hivyo.
HADIDU
REJEA NAM. 9
Mgogoro wa Ardhi baina ya wanakijiji na
Muekezaji, Pwani Mchangani.
Namna
ilivyoshughulikiwa na Kamati
Katika kufuatilia hadidu rejea hii, kamati ilifuatana
na Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “A”, watendaji wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji
na Nishati pamoja na Mheshimiwa Kazija Khamis Kona, aliyewasilisha malalamiko
ya wananchi hao Barazani.
Kamati ilikutana na wanakijiji wanaolalamika, ambao
walieleza kamati kuwa kuna mwekezaji aliyefahamika kwa jina la Bw. Majura
ambaye amejenga ukuta wa kuzungushia hoteli yake ambao umebana njia ya wapita
kwa miguu na sehemu ya uwanja wa mpira.
Wananchi pia walieleza kuwa Mwekezaji huyo ameuziwa
eneo na kupimiwa mipaka yake ambayo inatambulikana kwa alama maalumu (beacons)
ambazo anadaiwa kuzivuka hadi kuibana njia ya wapita kwa miguu, imeelezwa kuwa
watu wa upimaji ndiyo walioweka alama hizo (beacons) ambazo mwekezaji huyo
amezivuka.
Serikali ya Wilaya iliieleza Kamati kuwa haikuwahi
kuelezwa kuhusu mgogoro huo.
Ingawa watu wa Wizara ya Ardhi walikuwapo hawakuweza
kutoa ufafanuzi wowote wa usahihi wa mipaka iliyopimwa katika eneo hilo. Kamati
ilitaka kupata maelezo ya Mwekezaji huyo ambaye bahati mbaya yupo nje ya
Zanzibar na jitihada za kumpata mwakilishi wake hazikuzaa matunda.
Aidha kamati iliitaka Wizara ya Ardhi,
Makaazi, Maji na Nishati kuipatia kamati nakala ya kielelezo chenye kuonesha
uhalali wa matumizi ya eneo hilo kwa Bw. Majura pamoja na “site plan”. Pamoja
na jitihada za kamati kuikumbusha Wizara hiyo kuhusu kielelezo hicho, Wizara
hiyo ilishindwa kufanya hivyo hadi wakati wa kuwasilisha ripoti hii (tafadhali rejea kiambatanisho namba KTA. 9)
ambayo ni barua ya kamati kwa Wizara inayohusika na Ardhi ya tarehe
22/10/2013.
MAONI
YA KAMATI
Katika kadhia hii Kamati ilihitaji vielelezo kadhaa
ili kuweza kufanya uchambuzi sahihi. Miongoni mwa vielelezo ambavyo Kamati
ilivihitaji kutoka Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati ni nyaraka ya
uhalali wa matumizi ya eneo hilo kwa Bw. Majura, ‘’site plan’’ ya eneo hilo na
nyaraka zinazoonyesha hatua mbali mbali za uombaji wa eneo hilo.
Pamoja na hatua mbali mbali zilizochukuliwa na Kamati
katika kuhakikisha kuwa inapatiwa vielelezo hivyo, ikiwa ni pamoja na
kuiandikia wizara barua mara kadhaa, wizara imeshindwa kuipatia Kamati
vielelezo hivyo hadi wakati wa kuwasilisha ripoti hii.
Kamati imesikitishwa na hatua ya wizara kushindwa
kuwasilisha vielelezo hivyo wala kutoa maelezo yoyote kuhusu kadhia hiyo licha
ya kukumbushwa kwa barua juu ya wajibu wao wa kuwasilisha vielelezo hivyo.
HADIDU REJEA NAM. 10
Mgogoro wa Ardhi baina ya wananchi na viongozi wakuu
wa juu wa serikali, Tondooni
Namna ilivyoshughulikiwa na
Kamati
Kamati ilipokuwa inaifanyia kazi hadidu rejea hii
ilifuatana na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba na watendaji wake, Watendaji
wakuu wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati na Mheshimiwa Ali Salum Haji
Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi ambaye ndiye aliyetoa hoja hiyo wakati wa
Mkutano wa Baraza.
Mjumbe huyo aliieleza Kamati kuwa akiwa na baadhi ya
wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Baraza ya Kusimamia Ofisi za Viongozi wakuu wa
Kitaifa, alipokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa Tondooni wakati Kamati
ilipokuwa ikipita eneo hilo, kuwa eneo lao limechukuliwa na viongozi wa
serikali.
Baada ya kuhojiwa na Kamati ili abainishe viongozi
wanaodaiwa kuchukua eneo hilo, Mjumbe aliieleza Kamati kuwa Kiongozi
aliyeelezwa na wanachi kuhusika na uchukuaji wa eneo hilo ni Mkuu wa Mkoa wa
Kaskazini Pemba Bw. Dadi Faki Dadi.
Wananchi, walalamikaji, walipopata fursa ya kuzungumza
na kamati teule walieleza kuwa malalamiko yao yanahusu shamba ambalo Mkuu wa
Mkoa wa Kaskazini Pemba, Bw. Dadi Faki Dadi amewanyang’anyanya. Walidai kuwa
Bw. Dadi alikuja akawataka wakulima hao kuliachia eneo hilo kwa vile kuna
mwekezaji ambaye anaisaidia Serikali anayetaka kuwekeza katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa huyo, alieleza kamati
kuwa yeye siye anayemiliki eneo hilo kama inavyodaiwa na anayemiliki eneo hilo
ni mwekezaji aitwaye Ronit.
Anachohusika yeye ni kule kusimamia malipo
yaliyotolewa na mwekezaji huyo ambayo aliagizwa na Mheshimiwa Mansoor
(aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati) kuyasimamia, kwa vile
mwekezaji huyo alishapoteza fedha nyingi ambazo hazikuwa zikiwafikia walengwa.
Kwa mujibu wa maelezo ya Wizara ya Ardhi, Makaazi,
Maji na Nishati, kupitia Mkurugenzi wake wa Ardhi na Usajili, aliieleza kamati
kuwa eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 4.4 limekodishwa kwa mwekezaji aitwaye
Ronit Hershkovitz, raia wa Israel, kuanzia tarehe 28/2/2008 kwa mkataba wa
miaka 66, kwa malipo ya dola za Kimarekani 11,500. Wizara iliipatia Kamati hati
ya Mkataba wa Ukodishaji wa eneo hilo kwa Ndg. Ronnit na hati hiyo
inaambatanishwa na ripoti hii kama Kiambatanisho
nam. KTA 46.
Aidha Wizara iliieleza Kamati kuwa wananchi wa eneo
hilo walilipwa jumla ya Tsh.50 milioni kama fidia zao na aliyewawakilisha kwa
Hati ya Uwakala (Power of Attorney) kwenye malipo hayo ni Ndg. Shaame, na
kueleza kuwepo kwa orodha ya waliolipwa licha ya orodha hiyo kutowasilishwa
mbele ya Kamati. Kamati ilielezwa kuwa waliosimamia malipo hayo, pamoja na Ndg.
Shaame ni Ndg. Msellem na Ndg. Nassor Mmanga.
Walalamikaji waliiambia kamati kuwa uthibitisho wao wa
umiliki wa mashamba hayo ni urithi kutoka kwa wazee wao ambao walikuwa
wakiyatumia maeneo hayo kwa kilimo.
Aidha wananachi hao walifungua kesi katika Mahkama ya
Ardhi dhidi ya Ndugu Faki Dadi Faki pamoja na Mkuu wa Idara ya Ardhi Pemba
wakidai kutotendewa haki kwa kushurutishwa kuachia maeneo waliyokuwa
wakiyatumia kwa malipo kidogo. Kesi hiyo namba 50 ya 2010 iliamualiwa kwa
kuwapa haki katika eneo hilo walalamikaji Ndg. Mpogwe Juma na wenzake saba (7).
Nakala ya hukumu na mwenendo wa kesi hiyo inaambatanishwa na ripoti hii kama
kiambatanisho namba KTA. 47.
MAONI YA KAMATI
Kwa kuzingatia maamuzi na mwenendo wa kesi
iliyofunguliwa katika mahakama ya Ardhi, Pemba baina ya Mpongwe Juma Simba na
wenzake dhidi ya Dadi Faki Dadi na Mkuu wa Idara ya Ardhi, Pemba, kesi namba 50
ya 2010 mahakama iliamua kuwa eneo hilo kurejeshwa mikononi mwa walalamikaji
Mpongwe Juma na wenzake 7. Maamuzi ya kesi hii yalitoka tarehe 17/11/2011 na
hakuna kumbukumbu yoyote ya kutenguliwa kwa maamuzi ya mahakama hii.
Aidha kwa mujibu wa mwenendo wa kesi hii, Ndg. Dadi
Faki Dadi ambaye alifunguliwa kesi hii kwa dhamana yake ya Mkuu wa Mkoa
kaskazini Pemba na kupitia kwa mwanasheria wa ofisi ya Mkoa wake, aliiomba
mahakama kuondoa shauri hilo kutokana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kutoshiriki kwa
namna yoyote katika suala hilo na kuieleza mahakama kuwa Bw.Dadi Faki Dadi
ushiriki wake katika kadhia hiyo ulikuwa wake binafsi na si kupitia ofisi yake.
Kamati inaamini kuwa suala hili halikupaswa kuwa la
kibinafsi kwa kuwa mwekezaji wa eneo hilo alipatiwa mkataba wa ukodishwaji wa
eneo hilo na taasisi ya serikali na serikali ya mkoa imekiri kuhusika katika
kufanikisha suala hilo.
Kwa maana nyingine kama Mkuu wa mkoa hakushiriki
katika suala hilo la kusaidia kwa ajili ya kupatikana kwa eneo hilo kwa mujibu
wa wadhifa wake, inaweza kumaanisha kuwa serikali haikulipa fidia kwa wananchi
waliokuwa na vipando vyao katika eneo hilo.
Kamati imebaini kuwa utaratibu uliotumika katika
kulipa fidia ulikuwa wa kienyeji na haukufuata taratibu za kiserikali kwa
mujibu wa kifungu cha 56 cha Sheria ya Matumizi ya Ardhi ya mwaka 1992.
Kamati inashauri kuwa hasa kwa kuzingatia maamuzi ya
mahakama ya Ardhi serikali iwalipe fidia wananchi hao kabla ya kuchukuliwa eneo
hilo kwa mujibu wa thamani ya soko.
Kamati pia inashauri serikali kuandaa utaratibu maalum
wa fidia na kuiachia taasisi moja ya serikali kusimamia ulipaji wa fidia na utaratibu
huo uwekwe wazi na kujulikana kwa wanaotaka kuwekeza ili kuepuka mianya ya
rushwa.
HADIDU REJEA NAM. 11
Mgogoro wa ardhi baina ya Idara ya Upimaji na Ramani
na Wizara ya Kilimo, Tumbe, mgogoro ambao umepelekea wananchi kulivamia eneo
hilo.
Namna ilivyoshughulikiwa na
Kamati
Kamati iliishughulikia Hadidu Rejea hii kwa kufanya
kikao cha pamoja katika eneo la Tumbe, kilichowashirikisha Maafisa wadhamni wa
wizara husika ambao ni wa wizara ya Kilimo na Maliasili na wizara ya Ardhi,
Makaazi, Maji na Nishati, Katibu Mkuu wa Wizara inayoshughulikia ardhi, Naibu
Katibu Mkuu na ambaye kwa wakati huo alikuwa akikaimu nafasi ya Katibu Mkuu wa
wizara ya Kilimo na Maliasili, Mkurugenzi wa Ardhi na Usajili, Mkuu wa wilaya
ya Micheweni, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini
Pemba, Sheha wa eneo hilo na watendaji wa wizara ya ardhi, Makaazi, Maji na
Nishati.
Kamati ilielezwa na Afisa Mdhamini wa wizara ya Kilimo
kuwa wizara hiyo ilikuwa ikimiliki shamba katika eneo hilo la Tumbe ambalo
lilianza kuvamiwa na kufanywa makaazi na wananchi kwa kushirikiana na watendaji
wasio waaminifu na waliokuwa wakisimamia shamba hilo. Maafisa Wadhamini wa
wizara ya Kilimo na Maliasili na wa wizara ya Ardhi waliieleza Kamati kuwa kwa
wakati huo ambao Kamati inafanya kikao hicho, hakukuwa na mgogoro baina ya
wizara hizo mbili kufuatia makubaliano rasmi yaliyofanywa na wizara hizo mbili
tarehe 13/07/2012. Nakala ya barua ya makubaliano hayo inaambatanishwa na
ripoti hii kama kiambatanisho namba KTA
48.
Katika makubaliano hayo, Wizara ya Kilimo na Maliasili
walikubali kutoa eneo walilokuwa wakilitumia kwa shughuli za kilimo na ambalo
lilishavamiwa na wananchi na wizara hiyo kuwapa wizara ya ardhi ili wakate
viwanja kwa ajili ya ujenzi na wizara ya Ardhi nayo kwa upande wake ilitoa
shamba walilokuwa wakilimiliki karibu na shamba la wizara ya Kilimo na
kuwapatia wizara ya Kilimo shamba hilo.
Hata hivyo wizara ya Kilimo ilishindwa kuanza
kulitumia eneo walilokubaliana kupatiwa na wizara ya Ardhi kutokana na
kuonyeshwa mipaka isiyo sahihi ambayo ilijumuisha eneo la mwananchi aliyepatiwa
eneo hilo kwa mujibu wa sheria. Hadi wakati Kamati inafuatilia suala hili
hakukuwa na muafaka uliofikiwa kuhusu eneo linalomilikiwa na mwananchi huyo
ambalo pia ni sehemu ambayo wizara ya Kilimo walipatiwa na wizara ya Ardhi.
Kwa upande wake wizara ya Ardhi ilieleza kuwa wana
mipango ya kuwahalalishia wananchi waliovamia maeneo yaliyokuwa yakimilikiwa na
wizara ya Kilimo, kwa madhumuni ya ujenzi wa makaazi.
MAONI YA KAMATI
Katika kufuatilia mgogoro huu, Kamati imebaini
kutokuwepo kwa udhibiti wa kutosha wa maeneo ya serikali na kukosekana kwa
uaminifu miongoni mwa watendaji wa serikali wanaopewa dhamana ya kusimamia
maeneo hayo.
Kitendo cha mtendaji wa serikali aliyefahamika kwa
jina la Mselem ambaye alipewa dhamana ya kusimamia maeneo ya kilimo huko Tumbe,
Pemba kuyatoa maeneo hayo kwa wananchi bila ya kufuata taratibu za sheria, ni
cha aibu, kinachorudisha nyuma mipango ya maendeleo ya nchi na kukaribisha
migogoro ya ardhi isiyo ya lazima. Hivyo Kamati inapendekeza serikali kuchukua
hatua.
Aidha kutokana na jambo hili kuchukua muda mrefu
katika kufikia makubaliano baina ya wizara ya Ardhi na ile ya Kilimo na hivyo
kusababisha wananchi wengi kuvamia maeneo ya serikali, Kamati inapendekeza kuwa
taasisi za serikali zinapobaini mapungufu katika utekelezaji wa shughuli zao,
zichukue hatua haraka ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
HADIDU REJEA NAM. 12
Mgogoro wa ardhi baina ya wananchi na muwekezaji,
shehia ya Mzwardini, Bwejuu.
Namna ilivyoshughulikiwa na
Kamati
Katika kufatilia hadidu rejea hii kamati iliambatana
na Serikali ya Wilaya, watendaji wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati
na Mheshimiwa Hamza Hassan Juma, ambaye amewasilisha hoja hiyo Barazani.
Mheshimwia Hamza alifahamisha kamati kuwa mzozo wa
eneo hilo ulianza kwa mwekezaji mzalendo Bw. Khatib Jecha Zidi, ambaye amejenga
nyumba eneo la ufukwe ambayo imeziba njia ya wapita kwa miguu kuelekea pwani.
Wananchi waliokutana na kamati walieleza kuwa njia
hiyo imekuwa ikitumika na wanakijiji kuelekea pwani kwa shughuli zao za
kutafuta riziki.
Kwa mujibu wa maelezo ya serikali ya Wilaya waliagizwa
na Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa, kushughulikia na
kuchukua hatua ya kuvunja ukuta huo. Serikali ya Halmashauri ilichukuwa hatua
kwa kuwaita wahusika wote na kuwasikiliza.
Kabla ya kutolewa notisi ya kuvunja ukuta huo,
ilitolewa notisi nyengine kutoka Idara ya Mazingira, kwa barua ya tarehe
14/3/2012, ikimtaka Bw. Khatib Jecha kuchukuwa hatua ya kuvunja ukuta huo na
kuacha njia ya kupita wananchi. Barua hiyo inaambatanishwa na ripoti hii kama
kiambatanisho namba KTA. 49.
Kwa notisi hiyo, Serikali ya Halmashauri ilishindwa
kuendelea kuchukua hatua kwa vile tayari notisi ya Idara ya Mazingira
ilitangulia.
Kamati imefahamishwa kuwa Bw. Khatib Jecha alikaidi
maagizo hayo kwa madai kuwa jirani yake aliyejenga mwanzo, Bw. Abdulsatar ndiye
ameongeza ukuta wake hadi kwenye eneo lake.
Kamati ilielezwa kuwa, Serikali ya Wilaya ilipomwita
Bw. Abdulsatar, alikuwa na vielelezo vyote vya umiliki wa eneo lake na wala
Serikali hiyo ya Wilaya haikuwahi kupokea malalamiko ya Bw. Khatib Jecha dhidi
ya Bw. Abdulsatar.
Aidha Bw. Khatib Jecha alipotakiwa atoe vielelezo
vyake vinavoonyesha uhalali wa haki yake ya matumizi ya ardhi, alishindwa
kufanya hivyo.
Kamati iliitaka Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na
Nishati kuwasilisha mbele ya kamati vielelezo vinavyoonesha uhalali wa matumizi
ya maeneo yanayotumiwa na Bw. Khatib Jecha na Bw. Abdulsatar lakini hadi wakati
wa kuwasilisha ripoti hii, Wizara hiyo imeshindwa kuwasilisha vielelezo hivyo.
Tafadhali rejea kiambatanisho namba KTA.
9 ambayo ni barua ya kamati kwa Wizara ya
Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati ilikumbushia kupatiwa vielelezo mbali mbali
vikiwemo nyaraka za hati za matumizi ya Ardhi pamoja na “site plan” kwa Bw.
Khatib Jecha Zidi na Bw. Abdulsatar.
MAONI YA KAMATI
Kamati imebaini kuwepo kwa usimamizi
usioridhisha wa sheria za ujenzi na sheria ya ardhi no.12/1992 kwa taasisi
zinazohusika na usimamizi wa sheria hizo. Sheria ya Umiliki Ardhi No.12/1992,
imeweka sharti kwenye kifungu cha 5(1) kwa mtu yeyote anayekaa karibu na eneo
la bahari, kuacha njia ya wapita kwa miguu angalau mita kumi.
Hata hivyo utaratibu huu wa sheria
unaonekana hausimamiwi ipasavyo kutokana na kuwepo kwa tatizo la njia katika
eneo hilo. Kumeonekana mapungufu ya Mamlaka husika kushindwa kuchukuwa hatua za
haraka za kuzuwia ujenzi usiozingatia Sheria.
Sheria ya Umilikaji Ardhi No.12/1992
kifungu cha 6D, imetowa uwezo kwa hatua kuchukuliwa kwa yeyote atakayevunja
agizo la sheria ya Ardhi. Pamoja na kifungu hicho cha 5(1) cha sheria ambacho
kinaelekeza haki ya njia kukiukwa, mamlaka husika zimeshindwa kuchukua hatua za
haraka.
Kamati inashauri kuchukuliwa kwa hatua
kwa mtu yeyote anayekiuka sheria wakati wa ujenzi.
Aidha watendaji wa Halmashauri ya Wilaya
husika walipoitwa mbele ya Kamati pamoja na watendaji wa Idara ya Mazingira,
walikubali kuwa na mamlaka ya kuchukua hatua na kwamba wangelifanyia kazi suala
hilo.
Aidha Kamati inapendekeza ujenzi katika
eneo hilo uzingatie sheria kwa kuondosha sehemu isiyoruhusiwa ili kupisha njia.
Hata hivyo, kamati iliomba kupatiwa nyaraka mbali mbali zikiwamo hati ya
umiliki wa eneo hilo na ‘site plan’ lakini hadi wakati wa kuwasilisha ripoti
hii, Wizara imeshindwa kuwasilisha vielelezo hivyo mbele ya kamati.
Hitimisho:
Mheshimiwa Spika,
Baada
ya kumaliza zake, Kamati Teule inatoa mapendekezo yafuatayo.
1.
Wananchi kuelimishwa kuhusu dhana ya ardhi
kuwa mali ya Serikali.
Mheshimiwa Spika,
Ipo
haja kubwa kwa wananchi kuelimishwa juu ya dhana ya ardhi kuwa mali ya Serikali
kwa kuwa Kamati imebaini dhana hiyo kutofahamika vyema miongoni mwa
wananchi. Wananchi wengi ambao kwa namna
fulani wamekuwa wakiyatumia baadhi ya maeneo, bila ya kuwa na nyaraka yoyote ya
kuthibitisha haki walizonazo katika ardhi hizo, wamekuwa wakidhani kuwa wana
haki zote katika maeneo hayo na kwamba Serikali haina mamlaka yoyote katika
maeneo hayo. Kamati inapendekeza
kuchukuliwa kwa jitihada kubwa katika kuwaelimisha wananchi juu ya dhana hiyo
ili kuepusha migogoro. Aidha ni vyema
pia wananchi wakaelimishwa juu ya umuhimu wa kutafuta nyaraka zenye
kuthibitisha haki walizonazo katika ardhi kupitia taasisi husika za Wizara ya
Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati ili kuepuka migogoro ya ardhi.
2.
Watendaji
wa Wizara inayohusika na Ardhi na Watendaji wengine wa Serikali kuelimishwa
Sheria za Ardhi.
Mheshimiwa Spika,
Wakati
wa kutekeleza majukumu yake Kamati ilibaini mapungufu mengi miongoni mwa
watendaji wa Wizara inayoshughulikia ardhi lakini pia miongoni mwa Watendaji
wengine wa Serikali. Mapungufu hayo
yametokana na Sheria za Ardhi kushindwa kusimamiwa ipasavyo na hivyo kuwa
chanzo cha migogoro mingi ya ardhi hapa Zanzibar. Kamati inapendekeza kutolewa mafunzo ya kina
kwa watendaji wa Wizara inayosimamia
masuala ya ardhi, Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Ofisi za Wakuu wa Wilaya, Idara ya
Mazingira, na Watendaji wengine wa Serikali wanaohusika katika taratibu za
utoaji wa maeneo ya ardhi pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. Mafunzo
hayo yatasaidia Watendaji hao kutekeleza majukumu yao kwa kujiamini zaidi na
kwa kuzingatia Sheria.
3.
Sheria
za ardhi zisimamiwe vyema.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana
na mapungufu mengi ya Kisheria na Kikanuni yaliyoonekana wakati Kamati
ikitekeleza majukumu yake, Kamati inapendekeza kuchukuliwa hatua madhubuti za
kusimamia Sheria za Ardhi na Sheria nyengine za Nchi zinazohusiana na masuala
hayo ya ardhi. Miongoni mwa hatua
zinazopaswa kuchukuliwa ni pamoja na kutungwa kwa Kanuni kwa kila Sheria
inayohitaji kutungwa kwa Kanuni. Kamati
ilibaini kutotungwa kwa Kanuni nyingi zinazohusiana na masuala ya ardhi na
hivyo kusababisha utekelezaji wa baadhi ya mambo kuwa na hitilafu kutokana na
kukosa muongozo wa Kanuni. Aidha Kamati inapendekeza watendaji wote wa serikali
waliopewa dhamana ya kusimamia utekelezaji wa sheria zinazohusiana na ardhi
watekeleze wajibu wao kwa mujibu wa sheria hizo.
4.
Serikali
iongeze kasi ya utambuzi wa ardhi (Land Adjudication).
Mheshimiwa Spika,
Kutokana
na migogoro mingi iliyopo maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba ambayo wananchi
wamekuwa wakidai kuyamiliki maeneo hayo, Serikali haina budi kuongeza jitihada
katika zoezi la utambuzi wa ardhi (Land Adjudication) kama njia mojawapo ya
Wazanzibari kupata haki ya matumizi ya ardhi kwa mujibu wa kifungu cha 7 cha sheria ya Matumizi ya Ardhi ya mwaka 1992. Pamoja na kutambua juhudi za Serikali kwa
kuanza zoezi hilo kwa baadhi ya maeneo, Kamati inapendekeza kuwa Serikali
iwekeze fedha na rasilimali nyengine zaidi ili zoezi hilo liende kwa haraka
zaidi kwa maeneo yote ya Unguja na Pemba na kuwatambua wenye haki ya maeneo
husika na kuwapatia nyaraka zinazohusika. Kamati inaamini zoezi hilo la
utambuzi litakapokamilika litaondoa migogoro mingi ya ardhi hapa Zanzibar.
5.
Mpango
wa matumizi ya ardhi (Land Use Plan).
Mheshimiwa Spika,
Kamati
inapendekeza kuharakishwa kwa mapitio ya mpango wa matumizi ya ardhi kwa Unguja
na Pemba ili kuifanya miji yetu kuwa na haiba na pia kuepusha migogoro
inayoweza kujitokeza. Aidha Kamati
inapendekeza kusimamiwa ipasavyo kwa mpango huo wa matumizi ya ardhi kwa kuwa
kumekuwepo na tatizo kubwa katika usimamizi wa mpango uliopo ambapo baadhi ya
maeneo yamekuwa yakitolewa kwa watu mbali mbali kinyume na mpango wa matumizi
ya maeneo hayo.
6.
Sheria
zote na Sera za Ardhi zifanyiwe mapitio.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana
na matatizo mengi yaliyojitokeza katika suala la ardhi, Kamati inapendekeza
kufanyiwa mapitio ya kina ya Sheria zote za ardhi pamoja na Sera ziliopo ili
kubaini mapungufu yaliyopo na kurekebisha au kuandika upya Sheria hizo pale
itakapolazimu. Kamati inapendekeza kuwa zoezi hilo lifanywe kwa umakini mkubwa
kwa madhumuni ya kuondosha kabisa tatizo hilo badala ya utaratibu wa sasa wa
kuleta miswada ya marekebisho ya baadhi ya vifungu kwenye sheria hizo za ardhi.
7.
Sheria
ya “Fore Shore Decree” sura ya 105 itekelezwe ipasavyo.
Mheshimiwa Spika,
Kamati
inapendekeza kuwa Sheria ya “Fore Shore Decree” sura ya 105 inayohusu usimamizi
wa maeneo ya fukwe isimamiwe ipasavyo.
Katika kuisimamia Sheria hii, Kamati inapendekeza kupitiwa upya kwa
mikataba yote inayohusu maeneo ya fukwe ili kuzingatia ni kwa kiasi gani mikataba
hiyo imefuata masharti ya Sheria.
8.
Uimarishaji
wa Mahakama ya Ardhi.
Mheshimiwa Spika,
Mahakama
ya Ardhi Zanzibar iliundwa kwa madhumuni ya kupunguza kwa kiasi kikubwa
migogoro ya ardhi kwa kuiweka Mahakama maalum itakayosikiliza mashauri
yanayohusu ardhi pekee na hivyo Mahakimu wa Mahakama hiyo kupata muda wa
kutosha wa kusikiliza mashauri hayo ya ardhi.
Hata hivyo dhamira hiyo bado haijazaa matunda kwa kiasi kikubwa kutokana
na Mahakama hiyo kushindwa kuhimili kesi hizo na kufanya mashauri mengi ya
ardhi kuchukua muda mrefu.
Kutokana
na uzito wa suala hili la ardhi, Kamati inapendekeza kuwa Serikali ifanye
mapitio ya kina ya Sheria ya Kuanzisha Mahakama ya Ardhi ili kubaini mapungufu
na hatimaye kuifanyia marekebisho au kutungwa kwa sheria mpya kadri mapitio
hayo yatakavyokuwa. Aidha Kamati inashauri kuwa baada ya mapitio ya sheria ya
mahakama hiyo, Serikali iwekeze rasilimali za kutosha katika Mahakama hii ili
iweze kuwa na Mahakimu wa kutosha kwa kila Mkoa Unguja na Pemba na watendaji
wengine wa Mahakama, majengo yenye nafasi ya kutosha na yenye hadhi ya mahakama
pamoja na rasilimali nyengine muhimu zinazohitajika katika kuifanya Mahakama
hii itekeleze majukumu yake ipasavyo.
9.
Uratibu
kwa taasisi za Serikali zinazohusika na ukodishwaji wa ardhi.
Mheshimiwa Spika,
Kamati
ilibaini pia kutokuwepo kwa uratibu (Coordination) miongoni mwa taasisi za
Serikali zinazohusika katika maswala ya ukodishwaji wa ardhi ambapo taasisi
mbali mbali za Serikali zimekuwa zikikinzana katika hatua wanazochukuwa. Jambo hili linadhoofisha utendaji na
kukosesha kupatikana kwa ufanisi miongoni mwa taasisi hizo na pia kupelekea
migogoro ya ardhi isiyo ya lazima. Hivyo
Kamati inapendekeza kuwepo kwa uratibu madhubuti miongoni mwa taasisi za
Serikali kwa kuweka kituo kimoja (One Stop Centre) kitakachoratibu maswala ya
ardhi hasa katika kushughulikia mikataba ya ukodishwaji wa ardhi, ambacho
kitawahusisha watendaji wa taasisi mbali mbali za Serikali ambao watakuwa na
ufahamu wa aina moja (common understanding) juu ya masuala ya ardhi
wanayoyashughulikia.
10.
Kuwepo
kwa Database ya kuhifadhi kumbukumbu za ardhi.
Mheshimiwa Spika,
Kamati
imebaini mapungufu kadhaa ya kukosekana kwa kumbukumbu za maeneo ya ardhi
yaliyotolewa kwa watu mbali mbali.
Kasoro hii imechangia kwa kiasi kikubwa kuibuka kwa migogoro ya ardhi
hapa Zanzibar ikiwemo kutolewa hati zaidi ya moja kwa eneo moja, kutolewa
maeneo ya ardhi kinyume na mpango wa matumizi ya ardhi kwa eneo husika na
kadhalika. Hivyo Kamati inapendekeza
kuwepo kwa “database” hiyo itakayohifadhi kumbukumbu zote za maeneo
yaliyotolewa Unguja na Pemba na taarifa nyengine muhimu.
11.
Viongozi
na Watendaji wa Wizara ya Ardhi kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu masuala ya
ardhi.
Mheshimiwa Spika,
Kamati
imebaini kuwa wananchi wengi wa Zanzibar hawana taarifa za kutosha kuhusu mambo
mbali mbali yanayohusiana na ardhi jambo ambalo linachangia katika kuibuka kwa
migogoro ya ardhi. Miongoni mwa taarifa hizo ni masharti muhimu ya kuzingatiwa
kwa wananchi kupata haki ya matumizi ya ardhi ikiwa ni pamoja na sharti la
kuendeleza eneo ndani ya kipindi cha miaka miwili baada ya kupewa hati ya muda
ya matumizi ya ardhi, kuomba hati ya kudumu ya matumizi ya ardhi baada ya
kuendeleza eneo na kadhalika, mambo ambayo yamekuwa hayafahamiki miongoni mwa
wananchi wengi. Hivyo Kamati inaunga mkono kauli ya Mheshimiwa Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein iliyonukuliwa
katika gazeti la Zanzibar Leo la Novemba 12, 2013, aliyoitoa mbele ya Viongozi
na Watendaji wa Wizara ya Ardhi wakati wa kujadili ripoti ya utekelezaji wa
Wizara hiyo hivi karibuni ya kuitaka Wizara hiyo kutoa taarifa kwa wananchi
kuhusu mipango mbali mbali inayotekelezwa na Wizara hiyo.
12.
Ufutaji wa Haki ya Matumizi ya Ardhi ufuate
misingi ya Katiba na Kifungu cha 56 cha Sheria ya Matumizi ya Ardhi
Kamati Teule inashauri kuwa Serikali inapotaka kufuta
hati ya haki ya matumizi ya ardhi ni vyema ikafanya hivyo kwa kufuata masharti
ya kifungu cha 17 cha katiba ya Zanzibar
ya mwaka 1984, pamoja na masharti ya kifungu cha 56 cha Sheria ya Umiliki Ardhi
No.12/1992.
Kifungu cha 17 cha Katiba ya Zanzibar 1984, kinaeleza
kuwa:-
“hakuna mali ya mtu yeyote itakayochukuliwa kwa nguvu
na hakuna maslahi au haki yoyote inayotokana na mali hiyo itakayochukuliwa kwa
nguvu isipokuwa pale ambapo masharti yafuatayo yametimizwa” yaani:
a) Kumilikiwa au kuchukuliwa
kwa mali hiyo ni muhimu sana kwa ajili ya ulinzi, usalama wa wananchi,
mazingira ya afya, kuimarisha maendeleo ya upangaji wa mji pamoja na kuendeleza
mambo ambayo yataleta faida kwa wananchi kwa ujumla;
b) Umuhimu wa kuchukuliwa
kitu hicho ni mkubwa sana hata kwamba unahalalisha uchukuaji wake hata kama
utampa ugumu na matatizo mwenye mali hiyo; na
c) Sheria imewekwa kuhusiana
na umilikaji au uchukuaji huo kwa kutoa fidia inayolingana.
Aidha kifungu cha 56 cha sheria No. 12/1992 kinaweka
sharti la namna ya uchukuwaji wa haki ya matumizi ya ardhi. Kifungu hicho
kinaitaka Serikali iwapo inataka kufuta haki ya matumizi ya ardhi kwa maslahi
ya umma lazima ithibitishe kwenye mahakama ya ardhi uwepo wa sababu za msingi
za kuchukuwa ardhi hiyo.
Mbali na kuthibitisha huko, sheria inaelelekeza fidia
ya thamani ya soko ilipwe kwa ardhi hiyo inayotaka kuchukuliwa kwa maslahi ya
umma.
Mheshimiwa Spika,
Mwisho
Kamati inapenda kushuruku Uongozi wa Baraza chini yako wewe Mheshimiwa Spika na
Katibu wa Baraza kwa kuipa mashirikiano Kamati hii ambayo yameiwezesha Kamati
kutekeleza majukumu iliyopewa kwa ufanisi.
Aidha Kamati inapenda kumshukuru Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Makaazi,
Maji na Nishati pamoja na watendaji wote wa Wizara yake, Wakuu wa Mikoa na
Wakuu wa Wilaya pamoja na watendaji wa Ofisi zao na watendaji wengine na
wananchi wote waliotoa ushirikiano mkubwa kwa Kamati hii. Pia Kamati inawashukuru Wajumbe mbali mbali
wa Baraza la Wawakilishi ambao walikubali kushirikiana na Kamati kwa kuipatia
ufafanuzi wa hoja walizozitoa ndani ya Baraza.
Kabla ya hatujamaliza, ni vyema tukatambua kuwa Kamati
hii ndio Kamati pekee iliyoridhiwa na Wajumbe wa Baraza wote na Serikali kwa
kauli moja na hapa Kamati inaomba kunukuu maneno yako Mheshimiwa Spika wakati
unaitangaza Kamati Teule siku ya tarehe 10 Ogasti, 2012 ambapo ulisema:-
‘’ lakini jambo lenyewe tayari limeshakubalika
Waheshimiwa Wajumbe walisema na Mheshimiwa Waziri akasema kwa kweli na mimi naona
nisaidiwe, yaani nakubali hiyo Kamati Teule iundwe. Kwa maana hiyo, kulikuwa na
consensus kwa pande zote mbili kwa upande wa serikali pamoja na Waheshimiwa
Wajumbe’’
Vile vile mheshimiwa Spika naomba nimnukuu mheshimiwa
Waziri wa Ardhi wakati wa majumuisho wa taarifa ya serikali kuhusu ripoti ya
ZECO katika mkutano wa Baraza wa kumi na tatu ambapo alisema na namnukuu;
‘’ mimi naomba kwamba hii ripoti nipewe nafasi kwenda
kuifanyia kazi. Itakapopokelewa hapa nitapata nguvu ya kwenda kuifanyia kazi
hii ripoti. Ikikataliwa nitaifanyia kazi lakini nitakuwa naifanyia kazi tu,
lakini nitajua sina support, maana yake ni ripoti yetu hii lazima niifanyie
kazi mimi, itanisaidia hii na ile ripoti ya ardhi ile naomba iletwe alau nipate
kuifanyia kazi.’’
Mheshimiwa Spika,
Mwaka 1980 wakati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Aboud Jumbe analizindua Baraza la Wawakilishi,
alisema Baraza la Wawakilishi ni ngome. Mheshimiwa Spika naomba nimnukuu Waziri
Kiongozi Brigedia Ramadhan Haji, muasisi wa mapinduzi, katika hotuba yake ya
mwisho mwezi Disemba, 1983 ambapo alitoa tafsiri ya nini maana ya Baraza la
Wawakilishi ni ngome ambapo alisema na naomba nimnukuu;
‘’Maana ya Baraza la Wawakilishi ni ngome maana yake
ngome ya kuwatetea wanyonge wapate haki sawa. Tangu mwaka 1964 hadi mwaka 1979
ngome ilikuwa katika Baraza la Mapinduzi. Kimapambano unaweza kusema kuwa makao
makuu tu ndio yaliyohamishwa kutoka eneo fulani la vita kwenda eneo jengine.
Sasa makao makuu ni Baraza la Wawakilishi.’’
Mheshimiwa
Spika, mimi Ali Mzee Ali nikiwa Mwenyekiti wa Kamati hii, kwa niaba ya Kamati
ninayoiongoza, naiomba ngome hii ya Baraza ambayo ni sauti na kimbilio la
wananchi wetu waichangie na waichambue ili tumkabidhi Mheshimiwa Waziri wa
Ardhi akaifanyie kazi kama alivyoomba. Tunaamini Mheshimiwa Ramadhan Abdalla
Shaaban ambaye ni miongoni mwa askari wa mwanzo wa ngome hii mwaka 1980,
ataifanyia kazi kwa dhati ili turudishe hadhi ya ardhi ya nchi hii na kuondosha
migogoro ya ardhi na kuifanya rasilimali hiyo kuwafaidisha wananchi wote.
Mheshimiwa Spika,
Naomba
kutoa hoja.
Mheshimiwa Ali Mzee Ali,
Mwenyekiti,
Kamati Teule ya Kushughulikia
Migogoro ya Ardhi,
Baraza la Wawakilishi,
Zanzibar.
Kaka nashkuru sana kwa kutuchapishia ripoti hii inayoelezea pamoja na mambo mengine historia ya ardhi , umiliki pamoja na migogoro yake.
ReplyDeleteHata hivyo nna wasi wasi tu kwamba jamii yetu ya kiz'bari si yenye kupenda kusoma na hivyo ripoti hii inaweza kubaki tu kama machapisho mengine!
Ardhi ni rasilimali muhimu inanyolinda uhai wetu kama wanadamu na kama taifa lkn. kwa kweli SMZ bado haijawa na mikakati madhubuti ktk kusimamia rasilimali hii. zaidi ya kueleza historia!
Suluhisho pekee la kunusuru ardhi ya visiwani ni kuigawa ktk sehemu mbili, bila kujali mmiliki, hasa kwa vile kikatiba ardhi ni mali ya serikali. nazo ni
1) Ardhi ya kilimo
2) Ardhi ya makaazi
Baada ya hapo asiruhusiwe mtu yeyote kutumia ardhi kwa matumizi yasiyoruhusiwa, na kwa maeneo yatakayotajwa kua ni ya makaazi mmiliki asiruhusiwe kuuza bila ruhusa na usimamizi wa wizara husika.
Hii inaweza kua rahisi zaidi kwa wamiliki wa mashamba ya 'Eka' ambao kwa sasa wanayauza ovyo-ovyo bila idhini ya serikali na hivyo kusababisha ujenzi holela.