Na Masanja Mabula,Pemba
KILO 231,049 za samaki zenye thamani ya
shilingi 549, 419,000, wamevuliwa katika kipindi cha mwezi Januari mwaka huu
wilaya ya Wete kisiwani Pemba.
Afisa Uvuvi wilaya hiyo, Vuai Othman
Haji, amebainisha hayo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Kipangani.
Alisema samaki aina ya jodari na nduaro
ndio waliovuliwa kwa wingi.
Alisema katika kipindi hicho, jodari
waliovuliwa walikuwa kilo 67,050 wakiwa na thamani ya shilingi 236,724,000 na
nduaro kilo 56,214 wenye thamani ya
188,756,000.
Aidha alisema samaki aina ya kangaja,
vibua na dagaa waliovuliwa walikuwa na kilo
45,268 wakiwa na thamani ya shilingi 39,672,800 huku pweza na ngisi walikuwa na kilo 4,320
sawa na thamani ya shilingi 15,444,000.
Hata hivyo, alisema mafanikio hayo
yamekuja kutokana na ushirikiano uliopo kati ya Idara ya uvuvi, kamati ya
wavuvi na wavuvi wenyewe.
kwa upande mwengine, alisema vitendo vya
uvuvi haramu wa kutumia zana zisizoruhusiwa vimepungua na kuwataka wavuvi
kuendeleza uvuvi unaozingatia hifadhi ya mazingira ya bahari.
Mwenyekiti wa kamati za wavuvi wilaya
hiyo, Mohammed Kombo, alisisitiza haja
kwa wavuvi kuendeleza ushirikiano na Idara hiyo.
No comments:
Post a Comment